Jumatatu, 17 Novemba 2025

JAJI MFAWIDHI, MAJAJI, NAIBU MSAJILI KIGOMA WAWANOA MAHAKIMU WAKAZI WAPYA

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile hivi karibuni aliongoza kikao cha kuwafunda Mahakimu Wakazi wapya waliopangwa kufanya kazi ndani ya Kanda hiyo ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kigoma ambapo pamoja na mambo mengine Mahakimu hao walipewa wosia wa jinsi ya kutekeleza majukumu yao inavyotakiwa.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Rwizile alisema, Leo nitaongelea kanuni 15 za Hakimu zilizoandikwa na Jaji Mkuu wa Tanganyika enzi za Ukoloni, Sir. William Alison Russell wakati huo ambazo zinamtaka Hakimu kutumia mamlaka yake vizuri akiwa katika kiti chake, kwamba yeye ndio muamuzi katika mgogoro ulioletwa mbele yake, ambapo kanuni hizi zinakupa kuelewa nini ufanye, nini unapaswa kufanya, kipi usifanye na kwa wakati gani ili kuifanya kazi ya Hakimu kuwa ya heshima, kulinda amani katika eneo lake na kulinda heshima ya Mhimili wa Mahakama kupitia shughuli zake za kila siku.

Mhe. Rwizile aliwataka wote kusoma kanuni hizo na kuzielewa pamoja na kuziishi ili kuwa Mahakimu bora katika kizazi cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). 

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo aliwasisitiza Mahakimu hao juu ya matumizi ya TEHAMA katika shughuli zao kwakuwa ndio muelekeo wa Mahakama kwa sasa ili kujiimarisha vema na kuendelea kuongeza weledi katika mabadiliko ya kila siku ya sheria mbalimbali, ambazo Hakimu hapaswi kupitwa na muda.

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza aliwataka Mahakimu wapya kuhakikisha katika maisha yao ya uhakimu wazingatie weledi, uadilifu, uchapakazi na kuzingatia kutunza afya zao kwa njia ya mazoezi na yote hayo yajengwe katika ushirikiano na watu watakaofanya kazi nao katika vituo vyao. 

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa alimshukuru Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju kwa kuiona Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na kuongezewa nguvu ya Mahakimu sita ambao wanaenda kuleta tija katika Kanda hiyo.

Mhe. Mbelwa aliongeza kuwa, Mahakimu hao wataongeza kasi ya kumaliza mashauri ambayo kwa takwimu za Mahakama za Mwanzo zinaonyesha yapo maendeleo mazuri ambapo ujio wao utaleta ufanisi mkubwa katika Kanda hiyo.

Mahakimu hao wapya sita ni kati ya Mahakimu Wakazi walioajiriwa na Mahakama ya Tanzania hivi karibuni.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akisisitiza jambo hivi karibuni wakati alipokuwa akizungumza jambo na Mahakimu wapya kwenye ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kigoma.

Jaji  wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akitoa wosia kwa Mahakimu wapya sita waliopangiwa kufanya kazi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (kushoto) pamoja na Jaji  wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza wakiwa kwenye mazungumzo na Mahakimu wapya waliopangiwa Kanda ya Kigoma.

Sehemu ya Mahakimu wapya walipangiwa Kanda ya Kigoma wakisikiliza kwa makini maelekezo ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (hayupo katika picha).


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma na Mahakimu Wakazi wapya sita waliopangiwa kazi katika Kanda hiyo. Wa pili kushoto ni Jaji  wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi, wa pili kulia ni Jaji  wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa na wa kwanza kushoto ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Eva Mushi.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni