- Yaridhishwa na hatua za Miradi ya Ujenzi wa Mahakama inayoendelea mkoani humo
Na NAUMI SHEKILINDI, Mahakama-Simiyu
Kamati
ya Jaji Mkuu inayoshughulika na masuala ya maboresho imefanya ziara mkoani
Simiyu hivi karibuni yenye lengo la kukagua miradi minne inayoendelea Mkoani humo.
Kamati hiyo iliongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe.Mustapha Ismail ambaye aliongozana na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Deo Nangela, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Mariam Mchomba na Naibu Msajili Kitengo cha Maboresho ya Mahakama (JDU), Mhe. Hamza Adam.
Kamati
hiyo ilitembelea miradi yote na kujionea maendeleo ya miradi hiyo pamoja na
kutoa maoni yao ya nini kifanyike ili kuboresha majengo hayo kuwa ya kisasa
zaidi na kuanza kutumika mapema.
Aidha,
kamati iliridhishwa na shughuli za ujenzi zinazoendelea na kusisitiza kuwa
dosari ndogondogo zinazosababisha jengo lisianze kutumika mapema zirekebishwe
kwa uharaka ili majengo yaanze kufanya kazi.
Mhe.
Ismail alisisitiza wahusika wa utawala kuangalia motisha za watumishi kwa namna
watakavyoona inafaa ili kuendana na hadhi pamoja na upya wa jengo, lengo likiwa ni kuwaongezea ari
ya kazi watumishi wa Mahakama.
Mkoa
wa Simiyu una jumla ya miradi minne inayoendelea ikiwa ni Mradi wa Ujenzi wa
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) ambayo imefikia asilimia 94 kukamilika,
Mahakama ya Mwanzo Nyalikungu, Mhango na Lagangabilili ambayo ipo asilimia 100
ya ukamilishwaji.
Kwa
upande wake, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu Bw. Gasto Kanyairita aliwashukuru
kwa ujio wa Kamati hiyo na kuushukuru Uongozi wa Mahakama kwa ujumla kwa kuleta
miradi ya ujenzi wa Mahakama Mkoani humo yenye manufaa kwa wananchi wa Simiyu
pamoja na watumishi.
Ziara ya Kamati hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa kuimarisha miundombinu, kuendeleza matumizi ya teknolojia na kuhakikisha utoaji wa haki unafanyika mapema ipasavyo, kwa uwazi na kwa gharama nafuu.
Kamati ya Jaji Mkuu inayoshughulika na masuala ya maboresho ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe.Mustapha Ismail (wa pili kulia) wakisiliza taarifa ya maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Simiyu kutoka kwa Mkandarasi wa Mradi huo wakati walitembelea mradi huo kwa lengo la kuukagua.
Kamati ya Jaji Mkuu inayoshughulika na masuala ya maboresho ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe.Mustapha Ismail (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Simiyu baada ya kulikagua. Wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Deo Nangela, wa pili kulia ni Jaji wa Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Mariam Mchomba, wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita, wa kwanza kushoto ni Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga. Waliosimama nyuma ni sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni