Ijumaa, 21 Novemba 2025

KAMATI YA JAJI MKUU YA MIUNDOMBINU YAFANYA ZIARA MKOANI SONGWE

Na. Iman Mzumbwe – Mahakama, Songwe

Kamati ya Jaji Mkuu wa Tanzania inayosimamia Masuala ya maendelea ya uboreshaji wa Miradi ya Miudombinu ya Mahakama tarehe 19 Novemba, 2025 imefanya ziara mkoa wa Songwe kwa madhumuni ya kukagua na kujioneo hatua za utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Kituo jumuishi cha utoaji haki (Intergrated Justice Centre IJC).

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kufuatilia maendeleo ya mradi na kufanya tathmini ya ubora wa kazi, matumizi ya rasimali, utatuzi wa changamoto za utekelezaji pamoja na kujiridhisha kama mradi unakwenda sambamba na vigezo, viwango na muda uliopangwa.

Kamati hiyo iliongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. John Ubena aliyeongozana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kanda ya Dar es salaam, Mhe. Salma Maghimbi, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, Mtendaji wa Mahakama Kuu Bw. Leonard Magacha na Naibu Msajili Kitengo cha Maboresho ya Mahakama (JDU) Mhe. John Chacha.

Kamati hiyo ilitembelea na kukagua sehemu mbalimbali za miradi zikiwemo jengo Kuu la Utawala, Kumbi za Mahakama na vyumba vya kusikilizia mashauri, sehemu ya mifumo ya TEHAMA, mfumo wa usalama, miundombinu ya nje na eneo la uzio.

Katika ukaguzi huo, Kamati ilibaini kuwa maendeleo ya ujenzi huo umefikia takribani asilimia 73 ya utekelezaji wa mradi, ambapo Mkandarasi wa mradi huo Bw. Andrew Mpangalala alisema kuwa asilimia zilizobaki kufikia tarehe 31 Disemba, 2025 zitakuwa zimekamilika na watakabidhi jengo hilo katika mamlaka husika kwa muda huo.

Kamati ilieleza kuridhishwa na kasi, ubora wa baadhi ya kazi huku ikisisitiza kuongezwa nguvu katika maeneo machache yanayoonekana kwenda polepole.  Aidha kamati hiyo ilitaja baadhi ya changamoto zinazopaswa kupewa kipaumbele ikiwemo ucheleweshaji wa upatikanaji wa baadhi ya vifaa vya ujenzi.

Kamati ya Jaji Mkuu ilitoa maagizo na mapendekezo kwa wadau wote wa mradi akiwemo mkandasi kuongeza kasi ya utekelezaji ili kufikia muda wa makabidhiano uliopangwa, msimamizi wa mradi kuimarisha usimamizi wa ubora katika shughuli zote za finishing na kazi zote zinazoonekana kuwa na changamoto zirekebishwe ndani ya muda mfupi uliyowekwa na kamati hiyo.

Kamati ya Jaji Mkuu imepongeza juhudi zinazofanywa na timu ya usimamizi wa mradi katika Mkoa wa Songwe na imetia moyo hatua ya maendeleo iliyoonekana. Kamati imesisitiza kuwa mradi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Songwe ni wa kimkakati na unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma za haki kwa wananchi, hivyo utekelezaji wake unapaswa kufanyika kwa viwango vya juu kwa uadilifu na ufanisi.

Katika ziara hiyo, Jaji Mfawidhi Mhakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga alikuwa ni mwenyeji wa Kamati hiyo ambapo aliambatana na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Judith Lyimo, na Mtendaji wa Mahakakama ya Hakimu Mkazi Songwe Bw. Sosteness Mayoka.

Kamati ya Jaji Mkuu wa Tanzania inayosimamia Masuala ya maendelea ya uboreshaji wa Miradi ya Miudombinu ya Mahakama wakiwa kwenye picha ya pamoja na timu ya wakandarasi wanaojenga jengo la kituo jumuishi cha utoaji haki mkoani songwe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akiwakaribisha Kamati ya Jaji Mkuu ya miundombinu na kutoa taarifa fupi ya mradi wa ujenzi wa kituo hicho katika Ofisi ya Hakimu Mkazi Mahakama Songwe.


Muonekana wa Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani Songwe 

Muonekana wa Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani Songwe 

Kamati ya Jaji Mkuu ya Miundombinu wakikagua eneo la ujenzi wa mradi wa kituo jumushi Songwe

Mkandarasi wa ujenzi wa mradi Bw. Andrew Mpangalala akieleza juu ya maendeleo ya ujenzi mradi huo ulipofikia 

Kamati ya Jaji Mkuu ya Miundombinu wakielekea eneo la ujenzi wa mradi wa kituo jumushi Songwe


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni