Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Menejimenti
ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa imefanya kikao kwa njia ya Video ili
kutathmini utendaji kazi wa masuala mbalimbali ya Mahakama katika Kanda hiyo.
Mkutano
huo ulifanyika jana tarehe 03 Desemba, 2025 na kuhudhuriwa Wajumbe kutoka
Mahakama Kuu Iringa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa na Mahakama ya Hakimu
Mkazi Njombe ambapo Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa ni Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru.
Akizungumza
wakati wa kikao hicho, Mhe. Ndunguru aliwasisitiza Mahakimu wa Kanda hiyo kubaini
mashauri ya Mlundikano huku akiwataka Mahakimu wapange mikakati ya kumaliza
mashauri hayo pamoja na kuainisha sababu za kwanini mashauri hayo yamekuwa ya
mlundikano.
Kadhalika,
Jaji Mfawidhi huyo alisisitiza umuhimu wa kutumia matumizi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hasa kwa upandishaji wa Mashauri ya Majaji
kwenye mfumo wa TanzLII ambapo alisema, “huu ni mwezi wa mwisho wa mwaka
inatakiwa mashauri yote yaliyosomwa
hukumu yapandishwe kwenye Mfumo wa TanzLII.”
Pamoja
na hilo, Jaji Ndunguru alizungumzia kuhusu suala la uthibiti wa vitu vitakavyoleta hatari ambapo ni mchakato
wa kutambua, kutathmini na kuchukua hatua ili kupunguza au kuthibiti hatari
zinazoweza kuathiri utendaji kazi.
Kadhalika,
Mwenyekiti wa Kikao hicho, Mhe. Ndunguru aligusia suala la mashauri ya Mahakama
ya Rufani kwa kuyafanyia kazi haraka pindi taarifa ya kusudio la kufungua rufaa
litakapowasilishwa Mahakamani.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu
kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa alizungumzia tukio la Maadhimisho ya miaka
20 ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa ambalo maandalizi yake yanaendelea kufanyika
pamoja na uwepo midahalo ya elimu ya sheria kuanzia tarehe 08 -12 Desemba, 2025
kwa njia ya Redio na Vyombo mbalimbali vya Habari.
Amesema
kilele cha maadhimisho hayo itakuwa tarehe 15 Desemba, 2025 ambapo Mgeni Rasmi
anatarajiwa kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.
Katika
kikao hicho taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu ziliwasilishwa,
taarifa hizo ni pamoja na taarifa ya Mkoa Njombe iliyosomwa na Mtendaji wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Richard Mbambe, taarifa ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa iliyosomwa na
Afisa Utumishi wa Mahakama hiyo, Bw. Noel Shayo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (katikati) akizungumza na wajumbe waliohudhuria kwenye kikao cha Menejimenti ya Kanda hiyo (hawapo
katika picha) kilichofanyika jana tarehe 03 Desemba, 2025. Kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi.
Melea Mkongwa na kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Bernazitha Maziku.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru (aliyeketi mbele kushoto) pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa wakisikiliza hoja zilizokuwa zinaibuliwa na wajumbe wakati wa kikao cha Menejimenti ya Mahakama Kanda ya Iringa kilichofanyika jana tarehe 03 Desemba, 2025.
Mtendaji wa Mahakama ya Mkoa Njombe, Bw. Richard Mbambe (aliyeketi mbele kushoto) karibu na video akisoma taarifa ya utekelezaji wa kazi za Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe. Walioketi pamoja naye ni Wajumbe walioshiriki katika kikao hicho wakisikiliza taarifa hiyo.
Picha ya juu na chini ni wajumbe
wa Kikao cha Menejimenti kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Iringa na Mahakama ya
Hakimu Mkazi Mkoa wa Njombe wakiwa
kwenye kikao hicho wakijadiliana mambo mbalimbali kwa kutumia mfumo wa TEHAMA
yaani njia ya Mkutano mtandao (Video Conference) katika kuwasilisha hoja mbalimbali zilizokuwa zinatolewa.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni