Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hamidu Mwanga amewataka Wafungwa na Mahabusu wa Gereza la Mahabusu Mkuza Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani kuzingatia maneno yaliyopo katika wimbo wa Taifa na kuyafanyia kazi ili kuepukana na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Mhe. Mwanga aliyasema haya hivi karibuni alipofanya ziara ya ukaguzi
gerezani hapo.
Jaji Mwanga alisema kwa kuzingatia maneno yaliyopo katika wimbo huo, huenda Polisi wakatafutiwa kazi nyingine ya kufanya badala ya kushughulika na Wahalifu ambayo hawatakuwepo kwa wakati huo.
Wafungwa hao na Mahabusu walimkaribisha Mhe. Mwanga pamoja na timu ya Wadau wa Haki Jinai kwa wimbo wa Taifa na wimbo wa ‘Tanzania nakupenda kwa moyo wote’ ambapo Jaji Mwanga alisema nyimbo hizo zinachochea uzalendo na watu kuipenda Nchi na kutofanya vitendo vya kihalifu.
Mhe. Mwanga ameupongeza Uongozi wa Gereza la Mahabusu Mkuza kwa kuwafundisha uzalendo Mahabusu na Wafungwa wa Gereza hilo.
Ziara hiyo ya Jaji Mwanga imeibua kero nyingi kwa mahabusu hasa wanapokuwa katika Vituo vya Polisi na kubainika kuwa wamekuwa wakikaa vituoni zaidi ya mwezi mmoja wakisubiri upelelezi kukamilika ambavyo ni kinyume na sheria.
Akijibu swali aliloulizwa, Mwakilishi wa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Pwani, Mrakibu wa Polisi, Hawa Juma alisema utaratibu wa mtuhumiwa kukaa Kituo cha Polisi ni kwa saa 24 pekee.
Jaji Mwanga aliwataka Polisi watoe dhamana kwa watuhumiwa ili upelelezi uendelee wakiwa na dhamana ya Polisi na pia amewataka Polisi kutumia nafasi za kisheria kutatua matatizo ikiwa ni pamoja na kutoa dhamana ya Polisi.
Katika kikao hicho Mahabusu na Wafungwa wa Gereza hilo waliainisha changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo upande wa mashtaka kutoleta mashahidi kwa wakati mpaka wapate msukumo wa Mahakama, kufutwa kwa shauri na kukamatwa tena, kudhulumiwa mali zao wawapo Polisi kama vile simu na pesa.
Akitoa majibu kuhusu changamoto hizo, Jaji Mwanga alisema kuhusu
kutoleta mashahidi mahakamani Hakimu anayo mamlaka ya kufuta shauri, hivyo
kuwataka Mahakimu kuchukua hatua kwa mashauri ambayo mashahidi hawafiki
Mahakama kutoa ushahidi.
Akizungumza kuhusu suala la kutoleta mashahidi, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka – Pwani, Bw. Charles Magai alisema kutokana na sitofahamu baada ya uchaguzi washahidi wengi ni Polisi wapo kwenye kazi maalum hivyo wanashindwa kufika mahakamani.
“Lakini kuna utaratibu ambao wameuweka na Mahakama kusikiliza mashauri ambayo yana zaidi ya miezi sita kwa mfululizo (session) ili kuepuka mlundikano lakini pia kuwatendea haki washtakiwa,” alisema Bw. Magai.
Naye Mkuu wa Gereza la Mkuza, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Ibrahim Nyamka amesema kuwa wanaendelea na mchakato wa ujenzi wa Selo za Wahalifu wa kike na kukarabati Selo za Wahalifu wa Kiume na fedha za Mradi huo wameshaletewa, pia ujenzi wa Chumba cha Mahakama Mtandao (virtual court) unaendelea na upo katika hatua ya kupiga lipu na tayari jengo hilo limeshapauliwa.
Akijibu maswali aliyoulizwa na Jaji Mwanga, S/SGT Timothy ambaye ndie Mhandisi wa jengo hilo alisema hatua iliyofikia ni asilimia 65% ya ujenzi na matarajio ya kukamilika ni Januari, 2026 na vifaa vyote viko tayari, mara baada ya ujenzi wa jengo hilo kukamilika vifaa hivyo vitafungwa.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mwanga pamoja na wadau wa Haki Jinai walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Gereza hilo ikiwemo maeneo linapojengwa jiko la kisasa, kunakopikwa chakula cha Wafungwa na Mahabusu, katika Mabweni lakini pia walitembelea na kuona ujenzi wa chumba cha Mahakama Mtandao (Virtual Court) katika Gereza hilo ambapo jengo hilo litatumika kusikiliza mashauri ya jinai kwa njia ya video.
Katika ukaguzi huo wa robo ya pili ya mwaka uliofanywa na Jaji Mwanga aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Livin Lyakinana, Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Regina Samwel na Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Herrieth Challe.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Hamidu Mwanga (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja baada ya ukaguzi katika Gereza la Mkuza. Kutoka kushoto ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe Emmael Lukumai, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Livin Lyakinana na kutoka kulia ni Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe Regina Samwel na Mkuu wa Gereza la Mkuza Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Ibrahimu Nyamka.


.jpg)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni