Ijumaa, 28 Novemba 2025

JAJI MKUU AWATUNUKU VYETI WAHITIMU 813 KATIKA MAHAFALI YA 25 IJA

  •  Awataka Wahitimu hao kuleta tija kwa jamii kupitia elimu waliyopata
  • Awasisitiza kujibidiisha kuendana na mabadiliko ya Ki-TEHAMA
  • Awatahadharisha juu ya matumizi ya Akili Unde kwamba itumike kwa uangalifu, kusaidia fikra,  kujifunza na siyo kuchukua nafasi ya matumizi ya akili zao
  • Akitaka Chuo kuhakikisha kuwa, elimu wanayopata wanafunzi inakuwa ya vitendo zaidi kuliko nadharia pekee
  • Awashauri Wahitimu kila mmoja kwa imani yake kumtanguliza Mungu katika maisha ya kila siku
  • Awasihi kutopuuza mchango wa Walimu, Wahadhiri, Wazazi na Walezi katika kila hatua ya maisha yao

Na MARY GWERA, Mahakama-Lushoto

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju ametoa rai kwa Wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kutumia elimu waliyoipata katika Chuo hicho kwa kuisaidia jamii kwa kutenda haki na kuleta mabadiliko chanya popote watakapokuwa.

Akizungumza leo katika Mahafali ya 25 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yaliyofanyika katika Ukumbi wa Nyalali uliopo Chuoni hapo, Mhe. Masaju amesema Fani ya Sheria waliyoichagua Wahitimu hao ni fani ya kutenda haki.

“Nawasihi mkawe watenda haki kwani haki huinua Taifa. Na hili nalielekeza si tu kwa wale watakaoajiriwa Mahakamani au kwenye utumishi wa umma bali linamgusa kila mmoja wenu kwani haki ni suala linalogusa kila eneo la maisha ya mwanadamu,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amewataka pia Wahitimu hao kuwa, pamoja na ujuzi wa kitaaluma walioupata Chuoni hapo, Watanzania wanaamini wahitimu hao wamejengwa vilivyo kwenye misingi ya maadili mema.

 

“Kama ilivyoelezwa katika hotuba zilizotangulia, Chuo hiki kimejizolea sifa ya kuzalisha wahitimu wenye ujuzi wa hali ya juu kitaaluma lakini pia kuzalisha wahitimu wenye maadili bora na hivyo kuwa Chuo cha mfano katika hilo,” amesema Jaji Mkuu.

 

Amewakumbusha Wahitimu hao kuwa, mafanikio na ubora wao katika Fani ya Sheria waliyoingia yatategemea kuyashika na kuyatumia maarifa mliyoyapata Chuoni hapo lakini zaidi kujitofautisha na wengine kwa kuwa na maadili mema ambayo pia wamefundishwa vizuri katika Chuo hicho.

Mhe. Masaju amewaeleza Wahitimu hao kwamba, pamoja na mafunzo ya maadili waliyopata, ni vyema wakazingatia kile anachokiita ‘software’ nane za vitendea kazi muhimu vitakavyowaongoza katika kazi, masomo na maisha yao ya kila siku ambavyo ni Uadilifu (Integrity), Uwezo wa kutekeleza majukumu (Competency), Kuwiwa kuona haki inatendeka (Sensitivity to justice), Uwajibikaji (Accountability).

Ameongeza kuwa, vitendea kazi vingine ni Ubunifu (Creativity), Uchukuaji hatua kwa mapema ( Proactivity), Uzalendo wa Kitaifa (National Patriotism) na Uhalisia/ukweli usioegemea upande wowote (Objectivity).

 

“Tukiachia vitendea kazi tulivyozoea kama vile kompyuta, karatasi, kalamu nk., zipo software nane za vitendea kazi zitakazowaongoza katika majukumu yenu. Naziita “software” kwa sababu hizi ni kama mfumo wa ndani (internal operating system) unaoongoza namna mtu anavyofikiri, kufanya maamuzi, na kutenda kila siku kama ilivyo kwa kompyuta. Endapo mtavitumia ipasavyo, mtakuwa mfano wa kuigwa katika jamii,” amesisitiza.

 

Kadhalika, Jaji Mkuu amewausia wahitimu hao ni kujibidiisha ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea kwa kasi katika zama hizi za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.

 

“Katika zama hizi, njia za kiasili za utendaji wa shughuli mbalimbali, ikijumuisha shughuli za Serikali na binafsi, zimechukuliwa na njia za kielektroniki za utekelezaji wa shughuli hizo, hususani Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ni imani yangu kwamba mmefundishwa masomo yahusuyo matumizi ya TEHAMA kwa upana wake. Ninawasihi sana elimu hiyo isiishie hapa Chuoni tu kwa kufaulu masomo yenu pekee, bali mjibidiishe kujielimisha zaidi kwenye eneo hilo na muwe tayari kutumia maarifa na ujuzi mlionao kwenye majukumu yenu yajayo kwani huko ndiko Taifa na Dunia nzima inakoelekea kwa sasa kama si imeshafikia,” ameeleza.

 

Hata hivyo, Mhe. Masaju amewatahadharisha wahitimu hao kuwa waangalifu katika matumizi ya Akili Unde, ambapo amesema, “Ninajua kwamba baadhi yenu mmewahi kutumia au mnatumia programu za Akili Mnemba (Artificial Intelligence) katika masomo yenu au kazi zenu. Akili Mnemba ni sehemu ya matumizi ya TEHAMA lakini mnapaswa kutumia teknolojia hii kwa uangalifu mkubwa mno kwani inaweza kudumaza uwezo wenu wa kufikiria na kuchambua mambo.”

 

Amesema, Akili Unde ina manufaa ikitumika vizuri kusaidia njia za asili za kujifunza na kutafakari na siyo kuondoa njia hizo za asili na badala yake kutegemea Akili Unde kupita kiasi ambayo itadumaza ukuaji wa maarifa na ujuzi wa mtumiaji.

 

Hali kadhalika, Jaji Mkuu amewatahadharisha Wahitimu hao kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii hasa katika ulimwengu huu wa utandawazi.

 

“Wengi wetu ni mashuhuda kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii ambayo yamesababisha vijana wengi kuiga au kupata ushawishi wa watu kutoka nje ya nchi na matokeo yake ni kwamba wahanga wakubwa wa matumizi hayo mabaya ya mtandao ya kijamii wamekuwa ni vijana. Hivyo ninawasihi sana wahitimu mtumie TEHAMA na mitandao ya kijamii kwa masuala yenye tija kwenu na kwa Taifa kwa ujumla,” amesisitiza.

 

Aidha, Jaji Mkuu amekitaka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kuwa sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambapo amesema, “Itakumbukwa kwamba mwaka huu Tanzania imezindua Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, wote tunafahamu kwamba ni muhimu kwa kila Taasisi ya Umma kupanga mipango yake na kuelekeza utendaji wake kwenye kufikia malengo ya Dira hiyo. Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”


Mhe. Masaju ameeleza kuwa, Dira hiyo ina Nguzo Tatu, Nguzo ya pili inahusu Uwezo wa Watu Na Maendeleo a Jamii ambapo moja ya maeneo ya kipaumbele katika nguzo hii ni ‘Jamii iliyoelimika, yenye Ujuzi na Inayopenda Kujifunza’ amesema, “kipaumbele hiki kimejikita kwenye umuhimu wa kuendelea kuimarisha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia sambamba na ongezeko la idadi ya wanafunzi katika Taasisi za Elimu.”

 

Ameongeza kwamba, Dira hiyo inaelekeza kuwa ni muhimu kuendelea kuboresha mfumo wa elimu na mafunzo nchini ili kuendana na mabadiliko ya wakati ili kuwaandaa wahitimu kukabiliana na ushindani katika dunia inayobadilika kwa kasi, hivyo Chuo kinapaswa kuzingatia kikamilifu maelekezo hayo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ili kuwezesha Taifa kufikia malengo ya Dira hiyo ifikapo mwaka 2050.

Akizungumzia kuhusu uanzishaji wa Programu mpya chuoni, Jaji Mkuu amesisitiza kwamba, wakati Chuo hicho kinaendelea kutekeleza mkakati huo wazingatie pia malengo ya uanzishwaji wa Chuo hicho ili wasitoke nje ya malengo hayo bali wazidi kuyatekeleza kwa upana zaidi na kwa kuwafikia walengwa wengi zaidi kwakuwa Mahakama ya Tanzania na Wadau wa Sekta ya Sheria wana imani kubwa na Chuo hicho na wanakitegemea kama chombo cha kuendesha mafunzo yatakayoboresha utendaji kazi wa Mahakama na mfumo mzima wa utoaji haki nchini.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amekiri kuwa, Mahakama ya Tanzania inajivunia utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho na kusema kuwa, “Nimefurahi kusikia kuwa Chuo kimeendelea kufanya vizuri katika kutekeleza majukumu ambayo kimepewa na Sheria iliyokianzisha. Nawapongeza sana kwa hilo, Mahakama ya Tanzania inatambua nafasi muhimu na ya kipekee ya Chuo hiki ambayo imebainishwa vema kwenye Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya mwaka 2019 kuwa ni chombo cha kutoa mafunzo na kufanya tafiti kuhusu mafunzo ya kujengea uwezo watumishi wa Mahakama.

 

Jaji Mkuu amesema, Mahakama ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kama ambavyo imekuwa ikifanya siku zote na itajitahidi kutatua kero na changamoto mbalimbali za Chuo ili kukiwezesha Chuo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwani ufanisi wa Chuo ndiyo ufanisi wa Mahakama ya Tanzania.

 

Hata hivyo, Mhe. Masaju amesisitiza kwamba, Chuo kisijikite tu katika kutoa mafunzo kwa Majaji, Mahakimu au Wanasheria pekee, bali kitoe mafunzo kwa Kada zote za watumishi wa Mahakama. Hiyo ni kwa sababu huduma bora kwa mwananchi hutokana na mchango wa kila kada, kuanzia Walinzi, Wasaidizi wa Ofisi, Waandishi Waendesha Ofisi, Maafisa TEHAMA, Wahasibu, Madereva na wengine.

 

Sambamba na kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama, Jaji Mkuu ameeleza kuwa, ni wakati sasa Chuo kuhakikisha kuwa, elimu wanayopata wanafunzi inakuwa ya vitendo zaidi kuliko nadharia pekee.

 

“Katika kutekeleza mpango huo wa kuwapatia wanafunzi elimu ya vitendo, nawahimiza kutumia rasilimali zilizopo karibu na Chuo. Chuo kiendelee kuandaa utaratibu wa kuwapeleka wanafunzi kufanya mafunzo ya vitendo katika Mahakama ya Wilaya ya Lushoto na Mahakama ya Mwanzo Dochi, ambazo ziko karibu na Chuo, ili kupata fursa ya kujifunza moja kwa moja kuhusu uendeshaji wa shughuli za kimahakama,” amesema Jaji Mkuu.


Mhe. Masaju amesema kuwa, anatambua changamoto zilizopo kwa sasa katika Mahakama hizo ambapo Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Lushoto lina ofisi mbili tu za Mahakimu na ukumbi mmoja wenye uwezo wa kuchukua watu 30 pekee. Vivyo hivyo, Mahakama ya Mwanzo Dochi ina ofisi mbili na ukumbi mmoja wenye uwezo wa kuchukua watu wasiozidi 50. Miundombinu hii, kwa hali ilivyo, haina uwezo wa kuhimili idadi kubwa ya wanafunzi wa IJA, ambao hufikia takribani 800 kwa mwaka.

 

“Hivyo basi, napenda kusisitiza umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Lushoto. Nimejulishwa kuwa mkandarasi tayari amesaini mkataba na ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi Desemba mwaka huu. Hapa nisisitize ujenzi wa kumbi za Mahakama uzingatie uhitaji mkubwa wa wanafunzi wa Chuo hiki kufanya mafuzo kwa vitendo, Jengo hilo litakapokamilika, litaongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kuwahudumia wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo na hivyo kuboresha zaidi ubora wa mafunzo hayo,” amesisitiza.

 

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mhimili wa Mahakama, amewashauri Wahitimu hao kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika maisha yao ya kila siku kwani ndiye atakayewafungulia milango ya neema na mafanikio na pia kuwaongoza pale wanapokutana na changamoto mbalimbali za kimaisha au kitaaluma.

 

“Ninawaomba muwe watu wa ibada na kushika neno la Mungu kwani hilo litawasaidia kuwa na maarifa zaidi na maadili mema na hivyo kupata mafanikio katika kazi zenu au katika masomo ya elimu ya juu. Maandiko Matakatifu ya Biblia na Quran yamezungumzia umuhimu wa kumcha Mungu katika maisha yetu ya kila siku. Biblia Takatifu katika kitabu cha Mithali 1:7 inasema: “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, bali wapumbavu hudharau hekima na adabu,” ameeleza Mhe. Masaju.

 

Ameongeza huku akirejea Kitabu cha Quran Tukufu katika Sura ya 65 Aya ya 3 inasema:“Na anayemcha Mwenyezi Mungu, Humtengenezea njia ya kuokoka na Humpa riziki kwa mahali asipotazamia.” Amesema Aya hizo za Vitabu Vitakatifu zinaonyesha umuhimu wa kumcha Mwenyezi Mungu katika maisha ya mwanadamu.


Katika Mahafali hayo jumla ya wahitimu wa 286 wa Astashahada ya Msingi ya Sheria wametunukiwa vyeti, Wahitimu 241 wa Astashahada ya Sheria pamoja na Wahitimu 286 wa Stashahada ya Sheria wametunukiwa vyeti.

Aidha, Jaji Mkuu amewatunuku zawadi za fedha na vyeti wanachuo bora wanne kitaaluma kwa mwaka wa masomo 2024/2025 ambapo kwa upande wa Astashahada ya Msingi ya Sheria ni Bw. Jofrey Mtimbuka (1) na Bw. Gidion Nyamhanga (2).

Kwa upande wa Stashahada ya Sheria, wa kwanza ni Bw. Justine Sundi na wa pili ni Bw. Boniface Malobo huku Bw. Wenselaus Zacharia akitunukiwa zawadi ya Jaji Mkuu fedha taslimu kiasi cha Tshs. 1,000,000/= kwa kupata wastani wa daraja ‘A’ katika masomo ya mwenendo wa mashauri ya madai na jinai.

Wageni mbalimbali wamehudhuria mahafali hayo wakiwemo Majaji wa Rufani, Majaji Wafawidhi Tanga na Moshi, Mtendaji Mahakama Kuu Tanga, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tanga na wengine kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali, Taasisi binafsi, Viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na Viongozi wa Dini.

Meza Kuu ikiongozwa na Mgeni Rasmi ambaye ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) katika Mahafali yaliyofanyika Chuoni hapo leo tarehe 28 Novemba, 2025. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Mary Caroline Levira, wa pili kulia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo, wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mjumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Gerson Mdemu na wa kwanza kulia ni Makamu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Bw. Goodluck Chuwa.

Jaji Mkuu wa 
Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza na Wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) katika Mahafali ya 25 ya Chuo hicho yaliyofanyika leo tarehe 28 Novemba, 2025 chuoni hapo.

Makundi mbalimbali ya Wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 28 Novemba, 2025 wakati wa Mahafali ya 25 ya Chuo hicho.



Wageni mbalimbali pamoja na sehemu ya Watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha) wakati wa Mahafali ya 25 ya Chuo hicho yaliyofanyika leo tarehe 28 Novemba, 2025 kwenye ukumbi wa Nyalali Wilayani Lushoto.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira akizungumza wakati wa Mahafali ya 25 ya Chuo hicho leo tarehe 28 Novemba, 2025 wilayani Lushoto mkoani Tanga.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo akizungumza na Wahitimu wa Chuo hicho 
wakati wa Mahafali ya 25 ya Chuo hicho leo tarehe 28 Novemba, 2025.


Maandamano kuelekea ukumbi wa Nyalali tayari kwa ajili ya kusherehekea Mahafali ya 25 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) leo tarehe 25 Novemba, 2025.

Sehemu ya Wahadhiri wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakiwa katika Mahafali ya 25 ya Chuo hicho leo tarehe 28 Novemba, 2025.

Bw. Wenselaus Zacharia alitunukiwa zawadi ya Jaji Mkuu fedha taslimu kiasi cha Tshs. 1,000,000/= kwa 
kupata wastani wa daraja ‘A’ katika masomo ya mwenendo wa mashauri ya madai na jinai.


Jaji Mkuu wa 
Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akiwapatia zawadi Wanafunzi bora waliohitimu katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa mwaka 2024/2025.

Furaha ya kuhitimu.


















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni