● Mwenyekiti wa Baraza atoa wito wa kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kuendeleza mafunzo endelevu
● Naye Mkuu wa Chuo IJA mpaka sasa jumla ya wahitimu 9,767 wamehitimu katika Chuo hicho tangu kuanzishwa kwake
Na MARY GWERA na HALIMA MNETE, Mahakama-Lushoto
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira, amesema Chuo kimepiga
hatua kubwa katika utoaji wa mafunzo ya Sheria na kujenga uwezo wa watumishi wa
Mahakama, hatua iliyoimarisha kwa kiwango kikubwa ubora wa huduma na weledi wa
wahitimu.
Akizungumza leo wakati wa Mahafali ya 25 ya Chuo hicho
yaliyofanyika katika Ukumbi wa Nyalali Lushoto, Mhe. Dkt. Levira amesema kuwa, Chuo kimeendelea kuwa kituo muhimu cha kitaifa kinachozalisha wataalamu wa Sheria wenye ujuzi wa kisasa, nidhamu na tija kubwa katika maeneo wanayofanyia
kazi.
Akifafanua zaidi mbele ya mgeni rasmi, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, Mhe. Dkt. Levira amesema, Chuo kimedhamiria kuanzisha programu mpya za
masomo kwa njia ya masafa na mtandao, ili kupanua wigo wa mafunzo na kuongeza
idadi ya wanachuo walioko ndani na nje ya nchi sambamba na uanzishwaji wa
mafunzo endelevu kwa watumishi wa Mahakama.
Aidha, ameeleza kuwa Chuo kinakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti, uchakavu wa majengo, miundombinu ya maji
na umeme pamoja na uhaba wa vifaa vya TEHAMA, na kuomba Wizara ya Katiba na
Sheria kuendelea kutoa ushirikiano ili kuimarisha mazingira ya utoaji elimu.
“Tunashukuru Wizara kwa msaada wa bajeti ya nyongeza, lakini
bado tunahitaji ushirikiano zaidi ili kutatua changamoto hizi na kupunguza
gharama za uendeshaji wa chuo,” amesema Jaji Levira.
Katika hotuba yake, Mhe. Dkt. Levira ameipongeza Mahakama ya
Tanzania kwa kuendelea kukiamini Chuo katika utekelezaji wa mafunzo endelevu na
kushirikiana na Taasisi za ndani na nje ya nchi katika maeneo ya mafunzo na
tafiti.
Kwa upande wa wahitimu, amewataka kutumia maarifa waliyopata
kuchochea maendeleo ya Taifa na kuwa mabalozi wazuri wa chuo popote
watakapokwenda, akiwapongeza kwa kufanikisha safari yao ya kitaaluma.
Akitoa neno la utangulizi katika Mahafali hayo, kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo amesema, Mahafali hayo ya 25 yamejumuisha jumla ya wahitimu 813, kati ya hao wanawake 410 sawa na asilimia 50.4 na 403 ni jinsi ya kiume sawa na asilimia 49.6.
“Idadi hii inahusisha wahitimu 286 wa Astashahada ya Msingi ya Sheria ambao kati yao 135 ni jinsi ya kike sawa na asilimia 47.2 na 151 ni jinsi ya kiume sawa na asilimia 52.8, kwa upande wa Astashahada ya Sheria ni 241 ambapo 131 ni jinsi ya kike sawa na asilimia 54 na 110 ni jinsi yakiume sawa na asilimia 46 na kwa upande wa Stashahada ya Sheria ni 286 ambapo 144 ni jinsi ya kike sawa na asilimia 50.3 na 142 ni jinsi ya kiume sawa na asilimia 49.7,” amesema Mhe. Kihwelo.
Mkuu huo wa Chuo cha IJA, amesema mpaka kufikia mahafali hayo, jumla ya wahitimu 9,767 wamehitimu katika Chuo hicho.
Mhe. Dkt. Kihwelo amesema, kwa mujibu wa Sera ya Mafunzo ya
Mahakama ya mwaka 2019 Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ndiyo Chuo cha kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama
na katika kutekeleza hilo Chuo kina wajibu wa
kuandaa mitaala
na kuendesha mafunzo na kufanya tafiti kuhusu njia za kuwajengea
uwezo watumishi cha Mahakama ya Tanzania.
“Chuo
kinatekeleza jukumu hilo la kuwajengea uwezo
watumishi wa Mahakama kwa
kupitia Kurugenzi ya Mafunzo Endelevu ya Kimahakama ikifanya kazi kwa karibu na Kitengo cha Mafunzo
cha Mahakama ya Tanzania katika kuandaa mafunzo,
mafunzo ya wakufunzi, warsha na makongamano mbalimbali,” amesema Jaji Kihwelo.
Amesema, katika kipindi cha tangu mahafali yaliyopita, Chuo kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kiliratibu na kuendesha mafunzo mbalimbali ikiwemo; Mafunzo Elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani na vilevile mafunzo elekezi kwa Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo, Mafunzo ya Namna Bora ya Kushughulikia Mashauri ya Uchaguzi yaliyofanyika kwa Majaji wote wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Wasajili wote na Mahakimu Wafawidhi wote wa Mahakama za Wilaya na zile za Mikoa, Mafunzo ya Kuepusha Kurejesha Majeraha kwa Manusura wa Ukatili wa Kingono katika Kanda za Dar es salaam, Dodoma, Songea na Kigoma na Lushoto kwa kushirikiana na Irish Rule of Law International (IRLI) kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini na mengine.
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kilianzishwaji miaka 25 iliyopita kwa lengo la kutoa elimu ya sheria pamoja na mafunzo ya kimahakama vile vile mafunzo endelevu kwa watumishi wa sekta ya sheria.
Pia kama zilivyo Taasisi
nyingine za elimu ya kati
na juu, Chuo hiki kina majukumu makuu
matatu ambayo ni kutoa
mafunzo, kufanya tafiti
na kutoa huduma ya ushauri
wa kitaalamu. Katika upande wa kutoa elimu ya sheria Chuo kinatoa mafunzo
ya muda.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira akizungumza wakati wa Mahafali ya 25 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) leo tarehe 28 Novemba, 2025 kwenye ukumbi wa Nyalali Chuoni hapo.
Mkuu wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo akizungumza wakati wa Mahafali ya 25 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) leo tarehe 28 Novemba, 2025 kwenye ukumbi wa Nyalali Chuoni hapo.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza wakati wa Mahafali ya 25 cha Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) leo tarehe 28 Novemba, 2025.
'Brass band' wakiongoza maandamano ya Wahitimu wa Mahafali ya 25 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) leo tarehe 28 Novemba, 2025 Wilayani Lushoto.
Sehemu ya Wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakiwa katika Mahafali ya 25 ya Chuo hicho yaliyofanyika leo tarehe 28 Novemba, 2025 kwenye ukumbi wa Nyalali uliopo chuoni hapo.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni