Na ASHA JUMA -Mahakama Morogoro
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro hivi karibuni ilifanya zoezi la ukaguzi wa mashauri ya mirathi katika Mahakama za Mwanzo ili kuharakisha utoaji wa haki na kuyashughulikia yaliyochukua muda mrefu bila kumalizika.
Zoezi hilo, katika Operesheni Funga Mirathi,’ lilianza tarehe 18 Novemba, 2025 chini ya usimamizi wa Kamati Maalum iliyoanzishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim.
Kamati hiyo yenye wajumbe kumi iliongozwa na Mhe. Irene Lyatuu (Mwenyekiti), akisaidiwa na Mhe. Lameck Mwamkoa (Katibu) na Mhe. Asha Lukwele (Naibu Katibu) na Mratibu wa Kamati, Mhe. Janeth Kinyage.
Katika utekelezaji wake, Kamati ilitembelea Mahakama za Mwanzo Mikongeni, Ludewa, Mtibwa, Mvomero, Turiani, Magole na nyinginezo, ambapo walifanya mazungumzo na watumishi wa Mahakama pamoja na wananchi waliofika mahakamani kwa ajili ya kufuatilia mashauri yao.
Wakati wa ukaguzi huo, Kamati ilibaini changamoto mbalimbali zilizokwamisha mashauri ya mirathi kufungwa, ikiwemo mashauri yaliyopo Baraza la Ardhi, matatizo ya kiafya kwa baadhi ya wahusika kama ajali, makosa ya majina katika vyeti vya warithi, kutokuwa na elimu ya umuhimu wa kufunga mirathi na mengine kuwa katika hatua ya mwisho ya utekelezaji.
Ili kushughulikia changamoto hizo, Kamati iliweka mikakati ikiwemo kuwaita wahusika kupitia Serikali za Mitaa, kuwapigia simu moja kwa moja, pamoja na kubandika matangazo katika maeneo ya huduma kwa jamii, kama hospitalini.
Aidha, wananchi walipatiwa elimu ya kina kuhusu taratibu sahihi za kisheria zinazohusu mirathi pamoja na umuhimu wa kufunga mashauri hayo kwa wakati, ili kuhakikisha haki inapatikana kwa usawa, haraka na kwa ufanisi.
Wananchi waliohudhuria waliishukuru Mahakama kwa elimu waliyopata, wakieleza kuwa sasa wana uelewa mzuri kuhusu mchakato wa mirathi kwa mujibu wa sheria.
Zoezi hilo limetamatishwa rasmi jana tarehe 27 Novemba, 2025 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Janeth Kinyage, kwa kufanya ziara ya ukaguzi katika Mahakama za Mwanzo Msowelo, Masanza na Mahakama Kilosa Mjini.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha zoezi hilo Mhe. Kinyage aliwaasa Mahakimu wanao shughulikia mashauri ya mirathi kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi, kwa sababu yamebeba haki za watu
“Tuhakikishe tunamaliza mashauri haya kwa wakati kwa sababu yamebeba haki za watu.”
Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Irene Lyatuu akitoa elimu kwa wananchi.
Picha ya wananchi
waliopatiwa elimu ya mirathi.
Picha ya pamoja ya
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro,
Mhe. Janeth Kinyage, mratibu wa kamati (katikati) na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo
Kilosa mjini.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA- Mahakama, Dodoma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni