Na SHARIFU MWAYA-Mahakama, Mtwara
Mahakama ya Tanzania
katika Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, hivi karibuni iliendesha mafunzo kwa
wajumbe wa Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata ili kuimarisha uelewa na uwezo wa watendaji
katika jamii kwenye utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Nanyumbu, Mhe. Asifiwe Jembe aliendesha mafunzo hayo kwa kushirikiana na Mahakimu Wakazi, Mhe. Delphina Charles, Lemister Mtoni na Aloyce Makendi
Wajumbe walioshiriki
kwenye mafunzo hayo walitoka Kata ya Mangaka na Kilimanihewa na Mabaraza ya
Usuluhishi ya Jumuiya za Kidini, Wasaidizi wa Kisheria, Ofisi ya Ustawi wa
Jamii na Jeshi la Polisi – Dawati la Jinsia.
Akizungumza kwenye mafunzo
hayo, Mhe. Jembe alisisitiza umuhimu wa kuzingatia taratibu za kisheria katika
usuluhishi wa migogoro ya ndoa, pamoja na uelewa sahihi wa namna ya ujazaji wa nyaraka
kwa Mabaraza hayo na kujikita katika majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni
na miongozo iliyowekwa.
Alisisitiza pia umuhimu
wa ushirikiano kati ya Mahakama, vyombo vya dola, Viongozi wa Dini na Wadau
wengine katika kutoa suluhu za hiari, kuimarisha imani ya wananchi katika
mifumo ya utatuzi wa migogoro na kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani.
Mafunzo haya yalilenga kuimarisha uelewa na uwezo wa watendaji wa usuluhishi katika ngazi ya jamii ili kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa haki, weledi, mapema ipasavyo na kwa njia ya amani.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Nanyumbu, Mhe. Asifiwe Jembe (kushoto) akizungumza na Wadau katika mafunzo yaliyoongozwa na Mahakimu wa Mahakama hiyo.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mangaka,
Mhe. Aloyce Makendi (kushoto) akiendelea na mafunzo kwa jopo la washiriki.
Mahakimu wa Mahakama za Wilaya ya Nanyumbu katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mabaraza na Wadau mbalimbali.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA- Mahakama, Dodoma



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni