Jumatano, 17 Desemba 2025

MTENDAJI MKUU AHIMIZA KUKAMILIKA MRADI WA IJC KWA WAKATI

Na.  ALLY RAMADHANI - Mahakama, Katavi

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel Jana tarehe 16 Desemba, 2025 alitembelea na kukagua Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha utoaji Haki (IJC) Katavi kwa lengo kufuatilia maendeleo ya Mradi huo.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo hilo Mhandisi Victor Vedasto ambaye ni mwakilishi wa Mkandarasi kampuni ya AZHAR Construction Co. Ltd, alisema “Mradi mzima wa Kituo cha IJC Katavi ambao unajumuisha sehemu tatu yani Jengo Kuu, Eneo la nje (Mgahawa, uzio na chumba cha walinzi) pamoja na Manzari (Land scaping) umefikia asilimia 92, huku Jengo Kuu likiwa limefikia asilimia 95 na kuongeza kuwa tayari kazi za umaliziaji wa jengo unaendelea.

Aidha, akitoa maelekezo kwa Mwakilishi wa mkandarasi wa mradi huo, Prof. Ole Gabriel alisisitiza kuwa ni muhimu mpaka kufikia tarehe 31 Desemba, 2025 Mradi uwe umekamilika. Vilevile alisema kuwa, Mahakama “Lazima tuzingatie matumizi mazuri ya muda kwa kasi ninayoiona naomba iendane na ubora ulio unaokubalika ili tupate jengo nzuri,”

Aidha, Mtendaji Mkuu akiwa katika eneo la mradi wa ujenzi wa Kituo hicho, alipata wasaa wa kusalimiana na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi.

Moja ya nguzo katika Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ni Utoaji Haki kwa wakati mapema ipasavyo. Mahakama inatekeleza Mpango huo kwa kuboresha mazingira ya utoaji haki na kusogeza huduma za utoaji haki kwa wananchi kwa kujenga miundombinu bora na wezeshi itakayochangia ufanisi mzuri wa utekelezaji wa azimio hilo.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel,  akisalimiana na baadhi ya watumishi wa Mahakama Mkoa wa Katavi, wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa IJC Katavi.

Mhandisi Victor Vedasto, akitoa maelezo kuhusu maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Katavi kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa maelekezo kwa mwakilishi wa mkandarasi wa mradi, wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa IJC Katavi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni