Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Geita, imeibuka kinara kwenye Tuzo 16 zilizoandaliwa na kutolewa na Chama
cha Mahakimu na Majaji Tanzania [TMJA] jana tarehe 15 Januari, 2026 kwa matawi mbalimbali
ya Mahakama ya Tanzania.
Tuzo hizo zilitolewa kwa
washindi kwenye chakula cha jioni kilichoandaliwa na TMJA kwenye ukumbi wa
Mabeyo jijini Dodoma, baada ya kutambua mchango waliouonesha kwa Chama hicho
kwa mwaka 2024 na 2025.
Mahakama Kanda ya Geita
iling’ara kwenye tukio hilo baada ya kuzoa jumla ya Tuzo nne, ikiwemo ya Mlezi
Bora, ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina.
Tuzo ya kwanza Kanda hiyo
kunyakua ilihusu utambuzi wa kuwa Mahakama ya mfano na ya kwanza Tanzania kwa
kuachana na matumizi ya karatasi [paperless court] kwenye shughuli zote za
kimahakama.
Aidha, Kanda ya Geita
ilikabidhiwa pia Tuzo ya tawi bora katika michezo, nyingine ya tawi bunifu kwa ujumla
na Tuzo ya tawi bora zaidi kwa mwaka 2025.
Kwa upande mwingine, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, nayo ilikabidhiwa Tuzo maalum kwa ubunifu
wa kuendesha mafunzo mengi nchi nzima kupitia ufadhiri wa wadau mbalimbali.
Tunzo nyingine
zilizotolewa na matawi ya Mahakama kwenye mabano ni tawi bora katika mafunzo [Mbeya],
tawi bora katika ubunifu wa vyanzo vya fedha [Arusha] na tawi bora katika utalii
[Morogoro].
Utoji wa Tuzo hizo kwa
matawi hayo ulitanguliwa na Tuzo maalum zilizotolewa kwa Viongozi Wakuu wa
Mahakama ya Tanzania. Tuzo ya kwanza katika kundi hilo maalum ilitolewa kwa
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju.
Tuzo ya pili ilitolewa
kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed
Siyani, ya tatu kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel na Tuzo ya nne ikatolewa kwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Eva Nkya.
Wakati wa hafla hiyo, zilitolewa
pia Tuzo za mwaka 2024, Songwe kama tawi bora bunifu vyanzo vya fedha, Mtwara
na Lindi kama tawi bora katika mafunzo na Mahakama ya Rufani na Masjala Kuu
kama tawi bora katika michezo.
Utoaji wa Tuzo hizo
ulikuwa sehemu ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa TMJA uliokuwa unafanyika Makao Makuu
ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Mkutano huo ulifunguliwa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe
13 Januari, 2026. Jumla ya wanachama wa TMJA 1,200 walihudhuria Mkutano huo,
ambao ni wa pili kufunguliwa na Mkuu wa Nchi tangu kuanzishwa kwa chama hicho
mwaka 1984.
Chama cha JMTA ni cha
kitaaluma chenye malengo mbalimbali, ikiwemo kukuza na kulinda uhuru wa
Mahakama kama sharti la msingi na la lazima la utekelezaji wa majukumu ya
kimahakama.
Malengo mengine ni kukuza
maslahi na ustawi wa wanachama, kudumisha hadhi, heshima na tamaduni za Majaji
na Mahakimu, kuongeza na kuendeleza ujuzi, maarifa na uelewa wa Majaji na
Mahakimu kuhusu majukumu yao ya kimahakama kupitia tafiti endelevu na elimu ya
kitaaluma.
Mengine ni kutoa taarifa
na machapisho mbalimbali kuhusu masuala yenye maslahi au yanayowahusu wanachama,
kuandaa makongamano na mikutano ya wanachama na kudumisha mahusiano ya karibu
kadri inavyowezekana miongoni mwa wananchama na kushirikiana, na inapobidi,
kujiunga na vyama au Taasisi nyingine zenye malengo yanayofanana.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina [kushoto] akipokea Tuzo kwa ubunifu wa kuendesha mafunzo mengi nchi nzima kupitia ufadhiri wa wadau mbalimbali.
Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania [TMJA] je! Chama cha wasio mahakimu na Weshimiwa Majaji kinaiteje???
JibuFutayaani namanisha Non-Judiciary