Jaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Majaji na Mahakimu nchini kuzingatia
vitendea kazi nane katika utekelezaji wa majukumu yao hatua itakayochangia
kufikia azma ya Mahakama ya Utoaji Haki sawa kwa wote mapema ipasavyo.
Mhe. Masaju ameyasema hayo leo tarehe 15
Januari, 2026 katika hafla ya kufunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mahakimu na
Majaji Tanzania (TMJA) Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
“Naomba
niwakumbushe azma ya kumaliza
mashauri mapema ipasavyo, kila mmoja wenu atekeleze jukumu hili na viongozi
wote imarisheni usimamizi, katika kuyafanya haya, niwaongezee vitendea kazi nane ambazo naziita (software) ambavyo vitawasaidia kwenye kufikia
malengo tuliyojiwekea, katika kuongeza ufanisi wa kazi za kila siku. Tukiachia
vitendea kazi tulivyozoea kama vile kompyuta, karatasi, kalamu nk., mambo hayo
nane muhimu ni Uadilifu (Integrity),
Uwezo (Competency), kuwiwa kuona haki inatendeka (Sensitivity to justice).....,” amesema
Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu ameongeza kuwa, vitendea kazi vingine ni pamoja
na Uwajibikaji (Accountability), Ubunifu (Creativity),
Uchukuaji hatua kwa mapema kujituma (Proactivity), Uzalendo (National Patriotism)
na Uhalisia/ukweli usioegemea upande wowote (Objectivity).
Aidha, Mhe. Masaju ameeleza kuwa, Vitendea kazi hivyo vimetajwa pia katika kifungu cha 6 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma [Sura ya 398 R.E. 2023] ambapo Mahakimu na Majaji ni miongoni mwa Viongozi wa Umma wanaotajwa katika Sheria hiyo, wakiwa ni watumishi wa Serikali kwa mujibu wa Ibara 142 ya Katiba.
“Vitendea kazi vyote hivi vimefungamanishwa katika masharti ya uwajibikaji kwa mujibu wa Ibara ya 25 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.
Aidha, Jaji Mkuu amewapongeza Majaji na Mahakimu kwa jitihada za kuendelea kughulikia mashauri yote yaliyofunguliwa kwenye mahakama za ngazi mbalimbali nchini.
“Tarehe 22 Desemba, 2025 nilifanya Mkutano na Wasajili na Naibu Wasajili wote wa Mahakama, ambapo pamoja na mambo mengine nilisisitiza kuyapatia kipaumbele mashauri yote ya mirathi, ardhi, migogoro ya kazi na yale mashauri ya kiuchumi,” ameeleza Mhe. Masaju.
Amesisitiza kwa kuwakumbusha Maafisa Mahakama hao kwamba, katika kutekeleza wajibu wao wanapaswa pia kukumbuka matakwa ya Ibara ya 107A(2)(a)(b) ya Katiba na Sheria za nchi kwa madhumuni ya kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii, kiuchumi na kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi.
Amesema Serikali inaendelea na jitihada za usogezaji wa Huduma za Mahakama kwa wananchi ambapo amebainisha kuwa kwa sasa kuna Majengo mapya ya Mahakama Kuu: Masjala mpya ya Simiyu, Katavi, Lindi, Njombe, Singida, Songwe huku ujenzi ukiendelea Songea na Geita inatarajiwa kukamilika tarehe 01 Februari 2026.
"Masjala mpya ambayo tayari imeanza kazi ni Simiyu. Katavi na Njombe nazo zinaweza kuanza kazi mapema mwaka huu, nyingine zitasubiri hadi mwezi Machi, 2026," ameeleza Jaji Mkuu.
Aidha, amesema katika vituo hivyo vipya ni mashauri mapya tu yatasikilizwa hakutakuwa na uhamishaji wa mashauri kutoka vituo vingine. Pia watumishi wa kuanzia hawatatoka Kanda za zamani ili kuondoa dhana ya muendelezo wa changamoto kutoka vituo vya zamani ambapo amesema lengo ni kupima ufanisi wa uanzishwaji mpya na kupunguza msongamano wa mashauri.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amewakumbusha Wanachama hao wa TMJA kuwa ni jukumu la Chama kuongeza na kuendeleza ujuzi, maarifa na uelewa wa Majaji na Mahakimu kuhusu majukumu yao ya kimahakama kupitia tafiti endelevu na elimu ya kitaaluma.
Ameongeza kuwa, kupitia Mkutano huo Chama kimetekeleza jukumu la kuwajengea wanachama wake uwezo kupitia mada mbalimbali zikiwemo za kibenki, Uhifadhi wa wanyamapori, Masuala ya Kodi na Misitu.
“Hapa Mmekumbushwa juu ya mabadiliko yaliyoletwa na teknolojia kuhusu masuala ya mikopo, madhara ya hukumu zetu katika masuala ya kibenki, na umuhimu wa kujielimisha zaidi katika masuala ya dhamana ya mikopo mikubwa (letters of credit),” amesema Mhe. Masaju.
Jaji amesema, kupitia mada zilizotolewa wamepata maarifa yatakayowazesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
“Kwenye maliasili, wote tumekumbushwa, faida na changamoto za uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu, ikiwemo upelelezi, ukamataji, utunzaji wa vielelezo na utoaji wa adhabu na nini kifanyike katika kuimarisha ulinzi wa uhifadhi. Aidha, mmekumbushwa kuwa ninyi ni wahifadhi. Jukumu lenu kubwa ni kuzingatia Sheria na Kanuni za utoaji wa adhabu kwa watuhumiwa wa ujangili na waharibifu wa misitu, ili kuzuia na kupunguza au kukomesha uhalifu huu kabisa. Ninawashauri kutembelea hifadhi ili kujifunza, kuona vivutio vilivyopo na kuona namna bora ya kuhifadhi rasilimali zetu,” amesema Jaji Mkuu.
Kuhusu mada ya Mifuko ya kijamii, Mhe. Masaju amesema, Wanachama wote wamekumbushwa faida ya kushughulikia migogoro ya mifuko na hali ilivyo sasa. Hii imesaidia kufahamu, mchango wa Mahakama katika utatuzi wa migogoro ya Mifuko ya Kijamii. Vilevile, Dhana ya Kodi, imewekwa bayana, namna ukuaji wa uchumi unavyokuwa kwa kutegemea uchumi imara unaotokana na kodi.
“Kwa mada zilizowasilishwa, ni bayana kila taasisi, imeonyesha umuhimu wa Mahakama katika kuleta maendeleo ya kila sekta. Vivyo hivyo kunyamaza kwa Mahakama katika mambo ya muhimu, huleta maafa na uangamivu wa rasilimali zetu. Utawala wa Sheria ni nguzo imara kwa sekta zote,” ameeleza Jaji Mkuu.
Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amewasisitiza Wanachama wa TMJA kuchangamkia fursa za masomo kwa Kozi za muda mfupi na muda mrefu nchini India.
“Jana tarehe 14 Januari, 2026 nilikutana na Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Bishwadip Dey. Pamoja na mambo mengine tulizungumzia kuhusu ushirikiano baina ya Mahakama ya Tanzania na India. Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi alinijulisha uwepo wa fursa za ufadhili wa masomo na kozi mbalimbali za muda mfupi na mrefu. Alieleza kuwa yapo masomo ya muda mfupi kuanzia wiki mbili, mwezi mmoja hadi mwaka, na pia yapo masomo ya muda mrefu kama vile shahada za kwanza, shahada za uzamili na shada za uzamivu (PhD),” amebainisha Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju amesema mujibu wa Balozi huyo, Tanzania imepewa nafasi kubwa ya ufadhili kwa kozi mbalimbali kwa kila mwaka kwa fani mbalimbali zikiwemo za Sheria. Baadhi ya kozi za sheria zinazofadhiliwa ni pamoja na; (International Tax Law, Competition Law), (Mergers and Acquisitions Law), (Arbitration Law), (Maritime Law), (Environmental Law), (Private International Law), (Investment Law). Kozi nyingine ni pamoja na (Artificial Intelligence) na (Data Analytics).
Ameongeza kuwa, Ubalozi wa India uko tayari kutoa fursa ya kozi za muda mfupi katika maeneo mahsusi ambayo yana manufaa kwa Mahakama, na vilevile Balozi huyo ameahidi kuipatia Mahakama ya Tanzania vitabu vya sheria inavyohitaji ambavyo vimeandikwa na waandishi kutoka India.
Aidha, Jaji Mkuu ameahidi kuwa, Mahakama itaendelea kutoa fursa ya Chama kutekeleza majukumu yake mengine ikiwemo, kudumisha hadhi, heshima na tamaduni za Majaji na Mahakimu, kutetea maslahi na ustawi wa Wanachama wake, kutoa taarifa na machapisho mbalimbali kuhusu masuala yenye tija au yanayowahusu wanachama, kushirikiana, kujiunga na vyama au taasisi nyingine zenye malengo yanayofanana na Chama hicho.
Katika hatua nyingine Jaji Mkuu amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufungua Mkutano huo na kwa maelekezo muhimu yanayohusu uimarishaji wa uhuru wa Mahakama na kuifanya Mahakama kuwa yenye hadhi duniani na utayari wa Serikali kufanyia kazi ushauri wetu katika masuala kadhaa tuliyowasilisha kwake kama alivyoelekeza katika hotuba yake ya ufunguzi kama ambavyo pia inavyodhihirishwa katika Taarifa kwa vyombo vya Umma ilivyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Kwa upande mwingine, Mhe. Masaju ameupongeza Uongozi wa TMJA na Kamati ya Maandalizi kwa kuandaa Mkutano huo, na kuwasihi Wanachama wote kuendelea kutekeleza madhumuni ya kuanzishwa kwa Chama hicho ambayo ni pamoja na kuandaa makongamano na mikutano ya wanachama, na kudumisha mahusiano ya karibu kadri inavyowezekana, kukuza na kulinda uhuru wa Mahakama kama sharti la msingi na la Kikatiba la utekelezaji wa majukumu ya kimahakama na kadhalika.
Mkutano huo uliobeba Kaulimbiu isemayo: ‘Jukumu la Mahakama Huru Katika Utoaji Haki’ umefanyika baada ya Miaka 41 na umekutanisha jumla ya Wanachama 1,200.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni