Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa
Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania [TMJA], uliokuwa unafanyika Makao Makuu
ya Mahakama ya Tanzania [Judiciary Square] jijini Dodoma kwa muda wa siku tatu,
umehitimishwa leo tarehe 15 Januari, 2026.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. George Masaju, amehitimisha Mkutano huo na kuwashukuru Wanachama waliohamasika kufika Dodoma na kukaa kwa gharama zao. ‘Nimefurahishwa sana na
hali hii ya kujitoa kwenu, na huu ndio uzalendo wa ndani katika kusimamia mambo
ya Chama na pia ya kitaifa,’ amesema.
Mhe. Masaju ametumia
fursa hiyo pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan, kwa kufungua Mkutano huo na kwa maelekezo muhimu
yanayohusu uimarishaji wa uhuru wa Mahakama na kuifanya Mahakama kuwa yenye
hadhi duniani.
Aidha, Jaji Mkuu
alimshukuru Rais Samia kwa utayari wa Serikali kufanyia kazi ushauri wao katika
masuala kadhaa yaliyowasilishwa kwake kama alivyoelekeza katika hotuba yake ya
ufunguzi na kama inavyodhihirishwa katika taarifa kwa vyombo vya Umma
ilivyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu tarehe 13 Januari,
2026.
Hafla ya kufunga Mkutano
huo imehudhuriwa na Viongozi wengine wa Mahakama, akiwemo Amidi wa Mahakama ya
Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.
Kabla ya hafla hiyo, Jaji
Mkuu, Jaji Kiongozi, Rais wa TMJA, Mhe. Elimo Masawe na Viongozi wengine wa
Chama hicho walishiriki kwenye zoezi la upandaji miti katika moja ya eneo linalozunguka
jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, kama ishara ya kutunza mazingira.
Wakati wa Mkutano huo,
wanachama wa TMJA walipitishwa kwenye mada kadhaa na wawezeshaji wabobezi ili
kuwajengea uelewa kwenye maeneo mbalimbali.
Mada hizo ni jukumu la
Mahakama huru katika utoaji haki; uelewa wa miamala na bidhaa mbalimbali;
changamoto zinazotolewa na sekta ya benki na fedha nchini [nafasi ya Majaji,
Wasajili na Mahakimu].
Nyingine ni mafanikio,
changamoto na mustakabali wa ulinzi wa wanyamapori Tanzania; dhana ya uhifadhi-Mamlaka
Ngorongoro; mafanikio, fursa na changamoto; mchango wa utalii kwenye uchumi na
maendeleo ya nchi; uhifadhi endelevu wa rasilimali ya wanyamapori na mchango wa
Mahakama katika uhifadhi.
Wajumbe wa Mkutano pia
katika makundi mbalimbali walipitishwa kwenye mada inayohusu umuhimu wa misitu
na changamoto za uhifadhi na uendeshaji wa mifuko ya kijamii, fursa, changamoto
na mustakabali wake.
Mada nyingine zilihusu
bidhaa ya miamala, changamoto na namna ya kuzishughulikia na mikopo kwa ujumla
wake, miamala ya biashara za kimataifa, dhamana mbalimbali za kibenki,
uwekezaji katika dhamana na hati fungani na changamoto katika utekelezaji wa
amri za Mahakama.
Kabla ya kuhitimishwa
Mkutano huo, wajumbe pia walipitishwa kwenye mada zinazohusu dhana ya kodi kwa
ujumla; usikilizaji wa migogoro ya kodi na dhana ya kodi kidijitali na
maendeleo ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano [TEHAMA] katika usimamizi
wa kodi.
Watoa mada kwenye maeneo
hayo walikuwa Mhe. Dkt. Deo Nangela, Bw. Joachim Tesha, Bw. Usaje Mwambene, Bw.
July Lyimo Bw. Frank Mukoyogo, Bw. Prosper Mwangamila, Bw. Xavery Makwi, Bi.
Juliana Kombe na Bw. Paschal Mihayo.
Wengine ni Bw. Godwin
Ngilimi, Bw. Frank Mukoyogo, Bw. Prosper Mwangamila, Bw. Xavery Makwi, Bi.
Juliana Kombe, Bw. Paschal Mihayo, Bw. David Mungo’ong’o, Dkt. Zainabu Bungwa, P.
Marina na R. Komba
Mkutano Mkuu wa Chama cha
Mahakimu na Majaji Tanzania ni jukwaa muhimu la kutathmini mwenendo wa haki
nchini na kuweka mikakati ya kuimarisha taaluma na maadili kwa maslahi mapana
ya Taifa.
Safu ya Uongozi ya Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania.
Sehemu nyingine ya Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania [juu na chini] ikifuatilia yaliyokuwa yanajiri kwenye hafla ya kufunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa chama hicho.
Sehemu ya ya tatu Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania [juu na picha mbili chini] ikifuatilia yaliyokuwa yanajiri kwenye hafla ya kufunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa chama hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni