Na RAMADHANI RUGEMALIRA, Mahakama-Kinondoni Dar es Salaam
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi – Kivukoni, Mhe. Ishaq Kuppa ametoa rai kwa Mahakimu chini ya Mahakama hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu, huku wakimtanguliza Mungu mbele.
Mhe. Kuppa ameyasema hayo leo tarehe 30 Januari, 2026 alipokuwa akiongoza kikao kazi cha Mahakimu waliopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Mahakama ya Wilaya Kinondoni na Mahakama zote za Mwanzo, zilizopo Wilaya ya Kinondoni.
Mfawidhi huyo amewaasa Mahakimu hao pia kujiepusha na mambo yote yanayoweza kuichafua taswira ya Mahakama mbele ya Wadau.
Vile vile amewaasa Mahakimu hao kupendana na kutokuwa na chuki na husuda miongoni mwao.
Katika kikao hicho, Mahakimu wamekumbushwa majukumu yao ya kazi ikiwa ni pamoja na kupewa elimu juu ya uendeshwaji wa mashauri mada iliyotolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Mhe. Hawa Magesa, huku wajumbe wote wa kikao hicho wakichangia kwa kutoa michango na maoni yao.
Katika kikao hicho, Wajumbe pia wamekumbushwa kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini (Law Day) yatakayofanyika Jumatatu ijayo ya tarehe 02 Februari, 2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu - Kanda ya Dar es Salaam.
Matukio katika picha Kikao Kazi cha Mahakimu Wakazi-Kivukoni Dar es Salaam.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi – Kivukoni, Mhe. Ishaq Kuppa (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Mahakama ya Wilaya Kinondoni na Mahakama zote za Mwanzo, zilizopo Wilaya ya Kinondoni walioshiriki katika kikao hicho kilichofanyika leo tarehe 30 Januari, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Mhe. Hawa Magesa akitoa mada katika kikao hicho kilichofanyika leo tarehe 30 Januari, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni