Na EUNICE LUGIANA & ZAKIA ALLY, Mahakama-Kibaha
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani amewaongoza mamia ya waombolezaji katika ibada ya kuaga na maziko ya Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Emillian Matata Ezekiel Mushi aliyefariki dunia tarehe 24 Januari, 2026.
Ibada hiyo ilifanyika jana tarehe 29 Januari, 2026 nyumbani kwa marehemu Mwendapole Kibaha Mkoa wa Pwani.
Akitoa salamu za pole kwa familia, ndugu na jamaa, Mhe. Dkt. Siyani alisema maisha ya marehemu Jaji Mushi aliyaishi maisha yake kama sehemu ya maandalizi ya Maisha ambayo sasa ameyaanza.
Jaji Kiongozi alisema kwa wale wanaomjua marehemu Jaji Mushi alikuwa mtu muadilifu mwenye hekima na imani, na ndio maana Majaji na watu mbalimbali walifika ikiwemo wanafunzi aliowafundisha na aliofanya nao kazi wamesafiri kuja kumuaga, hali hiyo inaonesha jinsi gani aliweza kuishi na watu vizuri.
Aidha, Mhe. Dkt. Siyani alisema kwa upande wa Mahakama na tasnia ya Sheria kwa ujumla, Mhe. Mushi alichangia kwa kiasi kikubwa katika kutafsiri sheria kupitia maamuzi mbalimbali ambayo yataendelea kuwepo hata baada ya kuwa yeye amepumzika.
Aliongeza kuwa, maamuzi ambayo aliyatoa yameleta mchango ambao umewasaidia wengi kufahamu haki na namna ambavyo wanaweza kuziendea Mahakamani. “Mhe Mushi alikuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza taaluma za vijana wa kitanzania alipohudumu kama Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambapo alifundisha wengi na wengi wataendelea kumkumbuka.
“Hadhi hizo za kuishi kwake kwa faida na mchango aliokuwa nao kwa jamii zimewaachia funzo waliobaki hususani wale wanaotumikia umma katika nafasi mbalimbali, ni lazima wajiulize siku yao ikifika kama ambavyo Mhe. Mushi ameifikia watakumbukwa kwa jambo gani?,” alihoji Jaji Kiongozi.
Mhe. Dkt. Siyani alisema pamoja na hadhi yake ya Ujaji, Mhe. Mushi aliendelea kushikilia imani yake kwa Mungu.
Jaji Kiongozi alisema, wanapata faraja wakiyakumbuka maneno ya Mungu yasemayo, “Heri wafu wafao katika Bwana maana watapata kupumzika.”
Mhe. Dkt. Siyani alikiri kwa kusema, “nimepata funzo kupitia maisha ya Jaji Mushi hakuwabagua watu waliomzunguka aliwaunganisha akiwa hai lakini leo pia katika kumuaga ametuunganisha watu wa imani tofauti.
Alisema, funzo wanalopaswa kulichukua Watanzania kupitia maisha ya Jaji Mushi ni kushikamana na kutokubaguana kwa sababu ya dini, kabila, cheo, mamlaka au mali na fedha. Pamoja na tofauti ambazo wanazo kama binadamu wanapaswa kushikamana na kuendelea kuitunza amani ya Nchi yetu.
Naye Padri Chikawe aliyeongoza Misa takatifu ya Ibada ya maziko ya Marehemu Jaji Mushi alisema, “Ndugu yetu amelala katika kristo na ni njia mbayo kila mmoja wetu atapita.Tuiombee familia ili iangalie jambo hili katika Imani na waendelee kumkumbuka kwa Imani.”
Padri Chikawe aliongeza kuwa, Marehemu alipenda kutoa haki na katika kuhudumu kwake katika sheria alitoa Haki kwa anayestahili haki hiyo.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA),
Mhe. Dkt. Paul Kihwelo naye alitoa salamu zake kwa kusema kuwa, wamepokea
taarifa ya kifo cha Jaji Mushi kwa masikitiko makubwa kwa sababu ya historia
Chuo hicho.
“Marehemu Jaji Mushi alikuwa na mchango mkubwa kwani amefundisha na kuwajengea uwezo na ujuzi wanafunzi na watumishi wengi wa Mahakama na waliopo katika Sheria. Anakumbukwa na Wanafunzi pia wanajamii kwa namna ambavyo aliishi nao vizuri kwa upendo,” alieleza Mhe. Dkt. Kihwelo.
Kwa upande wake, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Noel Chocha alitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Majaji Wastaafu na kusema wako hapo kujifunza kupitia maisha ya Marehemu Jaji Mushi, ambapo funzo la kwanza alieleza kuwa, kuna kustaafu, fundisho la pili kuna kustaafu bila kujali kama ulikuwa Mtumishi kumbuka kuna siku utafariki na kwamba hatua ya kustaafu sio mwisho wa kuishi na badala yake kuna maisha baada ya kustaafu.
Mwakilishi kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Faraja Mangula alisema, msiba wa kuondokewa kwa Wakili na Jaji Mstaafu, Mhe. Mushi umeacha pengo kubwa kwa watu ambao mpaka sasa walikuwa wanategemea huduma kutoka kwake.
Marehemu Jaji Emilian Matata Ezekiel Mushi alizaliwa tarehe 20 mwezi Julai 1948 katika Kijiji cha Kimanganuni, Uru Wilaya ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro akiwa mtoto wa sita kati ya watoto tisa. Marehemu Jaji Mushi ameacha mjane na Watoto wanne.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt Mustapher Mohamed Siyani akitoa hesima za mwisho kwenye mwili wa Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Marehemu Emillian Mushi jana tarehe 29 Januari, 2026 nyumbani kwa marehemu Mwendapole Kibaha Mkoa wa Pwani.
Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa wamebeba mwili wa Marehemu Jaji Emillian Matata Ezekiel Mushi, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuelekea eneo la maziko nyumbani kwake Mwendapole-Kibaha mkoani Pwani.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Mustapher Mohamed Siyani akitoa salamu za pole kwa Mjane wa Marehemu, Bi. Lucia Libori Kiwia alipowasili nyumbani kwa Marehemu Mwendapole-Kibaha mkoani Pwani.
Jeneza lililobeba mwili wa Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Marehemu Jaji Emillian Mushi likishushwa kaburini.
Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Noel Chocha akiweka shada la maua katika kaburi la Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Mhe. Emillian Mushi.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




.jpg)


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni