Alhamisi, 29 Januari 2026

MAHAKIMU MBEYA WATOA ELIMU KWA UMMA KUPITIA KITUO CHA RADIO CHA KIJAMII

Na. MUKSINI NAKUVAMBA - Mahakama Mbeya.

Mahakimu Wakazi wa Mahakama mkoani Mbeya wametoa elimu kupitia Kituo cha Radio Baraka Fm ikiwa ni sehemu ya kuuelisha Umma juu ya masuala mbalimbali ya kisheria na uwepo wa maadhimisho ya siku ya sheria nchini kwa mwaka 2026.

Elimu hiyo ilitolewa tarehe 28 Januari, 2026 na Mahakimu Wakazi wawili, Wasaidizi wa Sheria wa Majaji kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambao ni Mhe. Alvin Juae, Mhe. Adriano Mtafya na Mhe. Ayubu Shelimo.

Akizungumzia Kaulimbiu ya siku ya sheria nchini Mhe. Ayubu Shelimo alisema mwaka huu Mahakama inatumia kaulimbiu isemayo “Mchango wa Mahakama katika ustawi na maendelelo ya Taifa” itakayotumika siku ya sheria nchini na siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini kwa mwaka 2026, ambayo maadhimisho hayo yatafanyika siku ya Jumatatu ya tarehe 02 Februari, 2026.

Aidha, Mhe. Shelimo aliongeza kuwa, kabla ya kufikia kilele cha siku ya sheria nchini Mahakama Mkoa wa Mbeya umeandaa matukio kadhaa yatakayoambana na siku hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya matendo ya huruma kwa kutembelea Kituo cha kulelea Watoto yatima cha NURU kilichopo Uyole Mbeya, tukio litakalofanyika siku ya tarehe 30 Januari 2026.

Aliongeza kuwa, kutakuwa na Bonanza la michezo mbalimbali linalotarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi tarehe 31 Januari, 2026 katika viwanja vya Chuo Kikuu TEKU na hatimaye sherehe rasmi za kilele cha siku ya sheria nchini siku ya tarehe 02 Februari, 2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu Mbeya.

Vilevile, Mhe. Shelimo aligusia Mikakati ya Mahakama ya Tanzania katika kufikia lengo Kuu la Dira ya Maendeleo ya Taifa ambayo inaenda sambamba na kusogeza huduma za Mahakama hadi ngazi ya Kata, kuboresha miundombinu ya TEHAMA, kuimarisha uwazi na uwajibikaji, kufanya maboresho ya sheria ngumu zilizopitwa na wakati na kuboresha huduma za Mahakama kupitia mpamgo wa matumizi ya Mahakama inayotembea.

Kwa upande wake, Mhe. Adriano Mtafya alizungumzia kuhusu matumizi ya TEHAMA yalivyosaidia kuborsha shughuli mbalimbali za Mahakama na kuchochea maendeleo ya Taifa, akifafanua kuhusu faida za TEHAMA alisema inarahisisha ufunguaji wa mashauri na usikilizwaji wa mashauri kupitia njia ya mtandao na pia aligusia matumizi ya Mahakama Inayotembea katika kuboresha shughuli za Mahakama ambapo kwa Kanda ya Mbeya zaidi ya mashauri 100 yamefunguliwa na kusikilizwa hadi kumalizika kupitia Mahakama inayotembea kwa mwaka 2025.

Naye, Mhe. Alvin Juae aliongeza kuwa, mchango wa Mahakama ya Tanzania katika kuboresha maendeleo na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambapo alisema kuwa maboresho ya shughuli mbalimbali za kimahakama zinawawezesha wanachi kufuatilia mashauri yao kwa njia ya mtandao na kutokupoteza muda mwingi mahakamani.

Mara baada ya Mahakimu hao kumaliza kutoa elimu hiyo kuhusu Siku ya Sheria nchini, kipindi kilihitimishwa kwa Mtangazaji kuruhusu kuuliza maswali, ambapo wasikilizaji waliuliza maswali mbalimbali kuhusiana na elimu iliyotolewa ili kupata ufafanuzi wa kina hoja mbalimbali.

Mahakimu Wakazi wa Mahakama Mbeya wakiwa Studio za Baraka FM Mbeya, wakitoa elimu kwa umma, kushoto ni Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Mbeya Mjini Mhe. Ayubu Shelimo na kulia ni Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Alvin Juae ambaye pia ni msaidizi wa sheria.

Mahakimu Wakazi wa Mahakama Mbeya wakiwa njie ya Studio za Baraka FM Mbeya, Kushoto ni Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Mbeya Mjini Mhe. Ayubu Shelimo, Katikati ni Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Adriano Mtafya ambaye ni msaidizi wa sheria na Kulia ni Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Alvin Juae ambaye pia ni msaidizi wa sheria.

Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Alvin Juae ambaye pia ni msaidizi wa sheria akifafanua jambo wakati wa kutoa elimu hiyo.
Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Adriano Mtafya ambaye ni msaidizi wa sheria akijibu hoja za wasikilizaji.


Mahakimu Wakazi wa Mahakama Mbeya wakiwa Studio za Baraka FM Mbeya wakitoa elimu kwa umma, kushoto ni Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Mbeya Mjini Mhe. Ayubu Shelimo, kulia ni Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Adriano Mtafya ambaye ni msaidizi wa sheria na katikati ni Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Alvin Juae ambaye pia ni msaidizi wa sheria.

Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Mbeya Mjini Mhe. Ayubu Shelimo kimwaga madini ya kisheria wakati wa utoaji elimu kwa umma.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni