Na EUNICE LUGIANA & ZAKIA ALLY, Mahakama-Pwani
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mhe. Yasinta Kingwala amesema usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao umewezesha kupunguza msongamano wa mashauri wilayani humo.
Mhe. Kingwala alibainisha hayo tarehe 27 Januari, 2026 alipokuwa akielezea shughuli za Mahakama kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini katika Kipindi cha Kapu kinachorushwa mubashara na Redio ya Chalinze Fm iliyopo Wilaya ya Chalinze Mkoa wa Pwani.
Mfawidhi alisema wananchi kwa sasa wamekuwa na imani na Mahakama kwakuwa huduma zimekuwa rahisi kupatikana na mashauri yanasikilizwa kwa wakati hata kwa wateja au mashahidi waliopo mbali na Mahakama husika wanasikilizwa huko walipo kwa njia ya mtandao (Virtual-Court).
Akitoa mfano wa Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo ambapo jiografia yake ni ngumu kwa wananchi wanaotoka Chalinze Mhe. Kingwala alisema, katika kubadili mitazamo hasi kutoka kwa wananchi, Mahakama imejikita katika kupeleka huduma za kimahakama karibu na wananchi kwa mfano Wilaya ya Bagamoyo mashauri ya Wilaya hiyo yanasikilizwa pia katika Kituo cha Mahakama Lugoba, kwa watu wanaotoka Chalinze ambapo mashauri yanafunguliwa na kusikilizwa badala na wadaawa kwenda Bagamoyo.
“Imani ya wananchi kwa Mahakama imekua kwa kusogeza Mahakama karibu kama ya Bagamoyo kuna kituo Lugoba,” alisema Mhe. Kingwala.
Akijibu swali aliloulizwa na mtangazaji Bi. Zainabu Ngambila kuhusu namna gani Mahakama inachangia katika ustawi na maendeleo ya Taifa, Mhe Kingwala alisema Mahakama inafanya jukumu kubwa la kutatua baadhi ya migogoro ya kiuchumi, kama vile migororo ya kodi, ujangili, ufisadi, uwekezaji na migogoro ya mtu na mtu na kwamba mashauri ya aina hiyo yakiletwa mahakamani yakasilikizwa na migogoro hiyo inapotatuliwa kwa namna moja au nyingine Mahakama inakuwa katika nafasi ya kustawisha maendeleo na uchumi wa nchi kwani watalii watakuja na kuona vivutio mbalimbali, kodi zitalipwa na wawekezaji watakuja kwa wingi kuwekeza kwani migogoro hiyo inatatuliwa kwa haki na mapema ipasavyo kupitia Mahakama.
Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Chalinze, Mhe. Hashimu Daudi alisema Mahakama inaongozwa na Dira ya Haki sawa kwa wote mapema ipasavyo na kwamba Mhimili huo umeweka utaratibu wa kumaliza Mashauri kwa wakati, kwa mfano Kwa Mahakama za Mwanzo Mashauri yanatakiwa kumalizika ndani ya kipindi cha miezi sita lakini kwa sasa shauri likifika Mahakama siku hiyo mashahidi wote wawepo isikilizwe ikiwezekana kumalizika imalizike hata kabla ya miezi sita. Hatua hii inaonesha namna ambavyo Mahakama inajitahidi kupunguza malalamiko ya ucheleweshwaji wa mashauri.
Naye, Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Chalinze, Mhe Abdul Mnolya alitoa wito kwa Wananchi kuendelea kuiamini Mahakama kwani inafanya kazi kwa weledi na migogoro inatatuliwa kwa wakati na kwa haki.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yatafanyika tarehe 02 Februari, 2026 katika ngazi za Mahakama Kuu, Mikoa na Wilaya zote. Aidha Kitaifa Maadhimisho hayo yatafanyikia katika viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Tambukareli jijini Dodoma na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ni: - ‘Mchango wa Mahakama katika Ustawi
na Maendeleo ya Taifa.’
Hakimu Mkazi-Mahakama ya Mwanzo Chalinze, Mhe. Abdul Mnolya akiwa katika kipindi cha Kapu cha Radio Chalinze kilichofanyika tarehe 27 Januari, 2026.
Picha ya Pamoja baada ya kushiriki Kipindi cha Kapu cha Chalinze Fm ambapo Mahakimu walizungumzia shughuli za Mahakama kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini. Wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mhe. Yasinta Kingwala, wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Chalinze, Mhe Hashimu Daudi, wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi- Mahakama ya Mwanzo Chalinze, Mhe Abdul Mnolya, wa kwanza kushoto ni Mtangazaji wa Radio Chalinze Fm, Bi Noela Mtavangu na katikati ni Mtangazaji wa kipindi Bi. Zabibu Ngambila.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni