Na NAUMI SHEKILINDI, Mahakama-Simiyu
Hivi karibuni Watumishi wa Kituo cha
Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania wakiongozwa na Dkt. Evetha Mboya walitembelea
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Simiyu (Kituo Jumuishi cha utoaji haki) kwa
lengo la kutoa elimu kwa wadau kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Kituo
hicho pamoja na kuongeza uelewa wa wananchi juu ya taratibu za kupata haki
kupitia Mahakama ya Tanzania.
Katika ziara hiyo watumishi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Simiyu wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe.
Wilbert Chuma walikutana na timu ya Kituo cha Huduma kwa Mteja kutoka Makao
Makuu na kupatiwa elimu juu ya uelewa wa ndani kuhusu nafasi na mchango wa kituo hicho
katika kuboresha utendaji kazi, uwazi na uwajibikaji ndani ya Mahakama.
Aidha, watumishi wa Kituo cha Huduma
kwa Mteja walitembelea Gereza la Wilaya ya Bariadi lililo chini ya ACP Julius
Nachunga ambapo walitoa elimu kwa Wafungwa, Mahabusu pamoja na Askari wa Jeshi
la Magereza. Elimu hiyo ilihusu majukumu ya Kituo cha Huduma kwa Mteja, namna
ya kuwasilisha malalamiko, maoni na mapendekezo, pamoja na taratibu za kupata
taarifa mbalimbali zinazohusiana na huduma za Mahakama.
Ziara hiyo pia ilililenga kuimarisha
ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na wadau wake pamoja na kusogeza
huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi. Kupitia elimu hiyo, wadau
walihimizwa kutumia Kituo cha Huduma kwa Mteja kama njia rasmi ya mawasiliano
kati yao na Mahakama.
Kwa ujumla, ziara hiyo ni sehemu ya
utekelezaji wa mikakati ya Mahakama ya Tanzania ya kuboresha utoaji wa huduma
kwa wateja, kuimarisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo na kuongeza imani ya
wananchi kwa Mhimili wa utoaji haki nchini.

Kiongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja-Mahakama ya Tanzania, Dkt. Evetha Mboya (aliyesimama) akifafanua juu ya Kituo cha Huduma kwa Mteja kwa watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Simiyu pindi yeye pamoja na Timu kutoka Kituo hicho walipotembelea Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu hivi karibuni. Kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita na kulia ni Hakimu Mkazi na Afisa Mrejesho kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Atupele Mwanjala.
Hakimu Mkazi na Afisa Mrejesho kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Atupele Mwanjala (aliyesimama) akisisitiza jambo juu ya namna Kituo cha Huduma kwa Mteja
kinatekeleza majukumu yake. Kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita na aliyeketi katikati ni Kiongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja-Mahakama ya Tanzania, Dkt. Evetha Mboya.Sehemu ya
watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Simiyu wakiwasikiliza watumishi kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania waliotembelea Mahakama hiyo hivi karibuni.
Sehemu ya Watumishi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mahakama pamoja na baadhi ya watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki – Simiyu walipotembelea Mahakama hiyo hivi karibuni. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Simiyu, Mhe. Wilbert Chuma, wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu na Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), Mhe. Elimo Massawe, wa pili kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita, wa kwanza kulia ni Kiongozi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja-Mahakama ya Tanzania, Dkt. Evetha Mboya na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi na Afisa Mrejesho kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Atupele Mwanjala.
Watumishi wa Gereza la Wilaya Bariadi (waliosimama nyuma) wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja. Wa pili kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu na Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), Mhe. Elimo Massawe, wa kwanza kulia ni Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Bariadi, ACP Julius Nachunga na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi na Afisa Mrejesho kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Atupele Mwanjala.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni