Na FAUSTINE KAPAMA -Mahakama, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Mahakama ya
Tanzania kwa hatua mbalimbali iliyochukua, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya
miundombinu, ugatuzi wa shughuli za Mahakama ya Rufani na kuimarisha utoaji haki
nchini.
Mhe. Dkt. Samia ametoa
pongezi hizo leo tarehe 02 Februari, 2026 kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba
yake na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel
John Nchimbi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria 2026, yaliyofanyika kitaifa
katika Viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Akizungumzia utekelezaji
wa miradi ya miundombinu, Rais Samia ameeleza kuwa majengo mengi yatakamilika
mwezi Machi, 2026 na mengine mwezi Oktoba mwaka huu, hivyo akahimiza usimamizi
wa miradi hiyo ili ikamilike kama ilivyopangwa na kuhakikisha thamani ya fedha
inaonekana.
Kadhalika, Mhe. Dkt.
Samia ameonesha kufurahishwa na hatua zilizochukuliwa za ugatuzi wa shughuli za
Mahakama ya Rufani kwa kuanzia na Kanda tano za Dar es Salaam, Mwanza, arusha,
Mbeya na Tabora.
Aidha, Rais Samia
ametambua jitihada za Mahakama za kuimarisha utoaji haki nchini kwa kutunga Kanuni
mbalimbali zinazosaidia usikilizaji wa mashauri ya madai na jinai na katika
kipindi kifupi cha miezi sita, Kanuni 11 imetungwa ili kuboresha upatikanaji wa
haki hapa nchini.
‘Napendekeza jitihada hizi
ziende sambamba na usimamizi wa dhamana kwa wale watuhumiwa wenye stahiki za
kisheria kupata haki mahakamani. Hili ni muhimu kwani linawezesha watuhumiwa
kuendelea na shughuli za maendeleo wakiwa kwenye dhamana,’ ameeleza kwenye
hotuba yake.
Rais Samia ametoa rai kwa
Wadau wote wa Mahakama kuunga mkono jitihada hizo kwa ustawi wa Taifa kwa
kuzingatia kuwa zoezi hilo la dhamana linahusisha pia Taasisi nyingine.
Kadhalika, Mhe. Dkt.
Samia ameipongea Mahakama ya Tanzania kwa kuendelea kutumia Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano [TEHAMA] katika shughuli za utoaji haki na kiutawala pia.
‘Nimefurahi kusikia kuwa
Mahakama imeanza ujenzi wa mfumo wa Akili Unde kwa ajili ya kuchukua mwenendo na
kumbukumbu za mashauri mahakamani. Hii ni hatua nzuri na muhimu itakayosaidia
kuleta ufanisi katika utoaji wa haki,’ amesema.
Amebainisha kuwa ili Mahakama
iweze kuchangia kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya Taifa, haina budi
kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
Akizungumzia Kauli mbiu
ya maadhimisho hayo inayosema, ‘Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo
ya Taifa,’ Rais Samia ameeleza kuwa imebeba ujumbe muhimu unaonesha kuwa
Mahakama si tu Mhimili uliojikita katika kutoa haki pekee, bali ni guzo muhimu
ya ustawi wa jamii, maendeleo ya kiuchumi na ustawishaji wa amani ya Taifa.
‘Mahakama ndiyo Mhimili ambao
unahakikisha kuwa haki inapatikana kwa wote bila upendeleo wala uonevu wa aina
yoyote. Mahakama siyo tu chombo cha mwisho cha utoaji haki nchini, bali ni
mshirika muhimu katika safari ya maendeleo ya Taifa,’ amesema.
Ametoa mfano kwa mwaka
2025 kuwa, Mahakama ilishughulikia mashauri ya kiuchumi yenye thamani ya zaidi ya
Trioni 50 na kati ya hayo, mashauri yenye thamani ya trilioni 13 yalisikilizwa
na kutolewa uamuzi kati ya mwezi Oktoba hadi Desemba, 2025 pekee.
Rais Samia amesema kuwa Mahakama
inaposikiliza na kutoa uamuzi kwa wakati kwenye mashauri ya jinai inatoa
mchango wake wa kuimarisha amani na utulivu wa jamii na hivyo kuwezesha
kufanyika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.
‘Kwa kutambua umuhimu wa
Mahakama katika ujenzi wa Taifa, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi
katika kuimarisha uhuru wa Mahakama ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake
kikamilifu na kuchochea ustawi na maendeleo yz Taifa. Lengo kuu la hatua hizi
ikiwa ni sehemu ya kutekeleza dhamira ya Serikali ya kujenga Taifa lenye amani
na uchumi jumuishi na imara,’ amesema.
Aidha, Mhe. Samia ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, kuimarisha rasimilimaliwatu na kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama na kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi, hususan kupitia mpango wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo.













Hakuna maoni:
Chapisha Maoni