Na MARY GWERA & HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma
Jaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju ametoa rai kwa Majaji, Mahakimu
Watumishi wote wa Mahakama, Mawakili na Wadau wengine wa Sekta ya Sheria nchini
kuzingatia wajibu wao wa kikatiba wa kusimamia haki bila ubaguzi na kuhakikisha
kwamba kila mwananchi anapata haki sawa mapema ipasavyo ili kudumisha ustawi na
maendeleo ya Taifa.
Mhe.
Masaju ametoa rai hiyo leo tarehe 02 Februari, 2026 katika Viwanja vya Makao Makuu
ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria
Nchini, ambayo yanaashiria kuanza kwa mwaka mpya wa Kimahakama. Hii ni mara
yake ya kwanza kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria akiwa Jaji Mkuu.
Mhe.
Masaju amesema kuwa, Mahakama inachangia ustawi wa maendeleo na jamii kwa
kutekeleza majukumu yake ya kikatiba pamoja na masharti mengine ya kikatiba
kama inavyoelezwa katika Ibara ya 4, 107A na 107B ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, majukumu ambayo yanaunda usalama, amani, maadili na umoja
wa kitaifa.
“Kwa
hiyo watumishi wa Mahakama hususani waamuzi, yaani Majaji na Mahakimu,
tunapoishi viapo vyetu vya ofisi na uadilifu kwa kuzingatia Katiba, Sheria na
maadili ya utumishi wetu, tunawezesha Mahakama kuchangia ipasavyo katika ustawi
na maendeleo ya Taifa letu,” amesema Jaji Mkuu.
Amesema
kuwa, Mahakama inachangia kudumisha amani, kujenga undugu wa wananchi, hali
inayowezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kijamii, kiuchumi na kisiasa
kwa weledi jambo linalochangia kusonga mbele katika ustawi na maendeleo ya Taifa,
huku ikizingatia utoaji wa haki na kueleza kuwa haki ni uamuzi unaofanywa na
Mahakama kwa kuzingatia masharti ya Katiba na sheria za nchi kwa mujibu wa ushahidi
unaosikilizwa mahakamani.
Mhe. Masaju ameongeza kuwa, mambo makuu yanayounda ustawi na maendeleo ya Taifa yametajwa katika Ibara ya 6-11 ya Katiba. Mambo hayo ndiyo yanayounda masharti mengineyo yote katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na kwa sababu hiyo, mambo hayo yamesisitizwa na kulindwa katika Ibara ya 19(3) na 30(2) ya Katiba. Hata Mahakama huru inapokuwa inatekeleza jukumu lake la kutoa haki inawajibika kuzingatia, kutia maanani na kutekeleza masharti hayo ipasavyo kama ambavyo Ibara ya 7(1) na 107B ya Katiba zinavyoelekeza.
Aidha,
Mhe. Masaju ameipongeza Serikali kwa hatua ya ujenzi wa Mahakama za ngazi zote
nchini hatua inayokuza mchango wa Mahakama katika ustawi na maendeleo ya Taifa
kwa sababu wananchi wenye uhitaji wa masuala ya kisheria wanaifikia Mahakama
kwa ukaribu na wale wote wanaokiuka Sheria wanawajibishwa mapema ili kuendelea
kulinda amani na ustawi wa jamii.
“Tunaipongeza
Serikali kwa hatua ya ujenzi wa Mahakama za ngazi zote nchini, hatua hii
inachochea, kuongeza na kukuza mchango wa Mahakama katika ustawi na maendeleo
ya Taifa kwa kuwa wananchi wenye migogoro wanaifikia Mahakama kwa ukaribu na
wanaokiuka Katiba na Sheria wanawajibishwa mapema kwa mujibu wa Ibara ya 26 ya
Katiba,” ameongeza Jaji Mkuu.
Aidha,
Mhe. Masaju amebainisha kuwa, ili Mahakama iweze kutekeleza jukumu na wajibu
wake katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuchangia
ipasavyo katika ustawi na maendeleo ya Taifa kwa mujibu wa majukumu yake kikatiba amesema, “sisi
watumishi wote wa Mahakama ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
mbali na kuzingatia Katiba, Sheria, Viapo, Maadili ya Utumishi wa Umma, Mila na
Desturi za Mahakama tunalazimika na tutalazimika kuzingatia na kuishi vitendea
kazi vya kiakili, kiroho na kimwili yaani tabia ambayo ni kama ‘software’
katika utendaji kazi wetu.”
Jaji
ametaja vitendea kazi hivyo kuwa ni pamoja na Kuwiwa kuona haki inatendeka
(Sensitivity to Justice), Uadilifu, Ubunifu, Uzalendo, Uwezo wa kumudu
utekelezaji wa majukumu ipasavyo, Uhalisi/ukweli usioegemea upande wowote
pamoja na Uwajibikaji.
Akizungumza
kuhusu uimarishaji wa usimamizi wa utoaji haki, Jaji Mkuu amesema kwamba
kuanzia tarehe 15 Juni, 2025 hadi tarehe 15 Desemba, 2025 Mahakama imetunga
jumla ya kanuni 11 pamoja na utungaji na urekebishaji wa kanuni huku
ikiimarisha haki ya watuhumiwa wenye stahili ya kisheria kupata dhamana,
kuanzia Mahakama za Mwanzo na kwamba kwa sasa dhamana inapatikana kwa
watuhumiwa na washtakiwa wote katika Mahakama za Mwanzo.
Amesisitiza
kuwa, Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya, na Mahakama za Mwanzo zinawajibika
kuhakikisha kuwa dhamana inatolewa kwa washtakiwa kwa mashauri yote ya jinai
yenye dhamana isipokuwa kama kuna sababu ya msingi, huku akielewa kuwa maamuzi
ya dhamana yanapaswa kutolewa siku ya kuwasilisha ombi la dhamana linapowasilishwa mahakamani, jambo ambalo
litasaidia kupunguza mianya ya rushwa pia kuwezesha haki ya dhamana kupatikana
mapema ipasavyo.
Mhe.
Masaju ameongeza kwamba, hatua hiyo inawawezesha wananchi wanaotuhumiwa kwa
makosa ya jinai kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii huku
wakihudhuria mahakamani kutokea nyumbani hadi mashtaka dhidi yao yanapokuwa
yametolewa maamuzi mahakamani.
Kwa upande wa uchumi, Jaji Mkuu ameeleza mwaka 2025
Mahakama katika baadhi ya mashauri ya kiuchumi yaliyosikilizwa kwa mujibu wa
Hati za Madai na Hati za Rufaa, yalifikia thamani ya TShs 50,441,708,274,962/=.
“Miongoni mwa fedha hizo Tshs 13 trilioni ikiwa ni kwa
mashauri yaliyosikilizwa na kumalizika mwezi Oktoba hadi Desemba, 2025. Bila
shaka kwa fedha zilizoingia katika matumizi na biashara mara baada ya mashauri
hayo kuhitimishwa Mahakamani zimechangia kukuza biashara na uwekezaji (Uchumi)
na hivyo ustawi na maendeleo ya Taifa,” ameeleza.
Katika
hatua nyingine, Jaji Mkuu amesema kuwa, Mahakama inaendelea na uimarishaji na
matumizi ya TEHAMA katika shughuli zake ili kuimarisha ufanisi, ameeleza kuwa
hivi sasa Mahakama inajenga mfumo unaotumia Akili Unde kwa kurekodi mwenendo wa
kumbukumbu za mashauri na hukumu Mahakamani, mfumo huo unatafsiri lugha inayotumika
na kuandika kwa lugha inayokuwa imechaguliwa kuandikwa.
Aidha
Mhe. Masaju ameeleza kuwa Dira ya Mahakama ni Haki sawa kwa wote mapema
ipasavyo ambayo msingi wake ni Ibara ya 107A(1((2)(a)(b) na Ibara ya 107B ya
Katiba, ambayo imebeba nguzo ya kutoa huduma zinazomlenga mwananchi, ndio maana
Serikali inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Mahakama za ngazi zote nchini ikiwemo
Mahakama za Mwanzo kila Kata ili kusogeza huduma za kimahakama karibu zaidi na
mwananchi ikizingatia kwamba asilimia 70 ya mashauri yote yanayofunguliwa mahakamani
ni yale ya Mahakama za Mwanzo.
“Dira
ya Mahakama ni Haki Sawa kwa Wote Mapema Ipasavyo, msingi wa Dira hii ni Ibara
ya 107A(1)(2)(a)(b) na Ibara ya 107B ya Katiba, mojawapo ya nguzo za Dira ya
Mahakama ni huduma zinazomlemga mwananachi,” ameeleza Jaji Mkuu.
Vilevile,
Mhe. Masaju amesema kuwa, Mahakama inaendelea na zoezi la ugatuzi wa Mahakama
ya Rufani ili iweze kuwepo katika baadhi ya Kanda za Mahakama nchini ambazo
tayari zina Masjala ndogo.
Jaji
Mkuu ameeleza kwamba, lengo la ugatuzi ni kusogeza huduma za Mahakama karibu na
wananchi ili kuwezesha haki kupatikana mapema ipasavyo na kwamba katika ugatuzi
huo baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani watafanya kazi wakiwa katika Masjala
za Kanda kama Arusha, Mwanza, Mbeya, Tabora na Dar es Salaam ambayo pia
itahudumia Zanzibar kabla ya kuanzishwa kwa Masjala nyingine ya kudumu
Zanzibar.
Siku ya Sheria nchini ya mwaka huu 2026, imebeba Kauli Mbiu isemayo: “Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa.”
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akisisitiza jambo wakati wa hotuba yake leo tarehe 02 Februari, 2026 kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi (kulia) akiteta jambo na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini yaliyofanyika leo tarehe 02 Februari 2026 katika viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Meza kuu ikiongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Meza kuu ikiongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Sheria Nchini wakiwa katika picha ya pamoja na Meza kuu baada ya kukamilika kwa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini yaliyofanyika leo tarehe 02 Februari 2026 katika viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe.
George Masaju akikagua Gwaride la Heshima leo tarehe 02 Februari, 2026 mara
baada ya kukamilika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini
Dodoma.

















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni