Na HALIMA MNETE-Mahakama, Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema kuwa Mahakama ya Tanzania ni Mhimili
muhimu katika kuchochea maendeleo na ustawi wa Taifa kupitia utekelezaji wa
haki, utawala wa sheria na kulinda misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Mhe. Dkt. Nchimbi ameyasema hayo leo tarehe 02 Februari,
2026 katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, yenye kauli mbiu isemayo “Mchango
wa Mahakama katika Maendeleo na Ustawi wa Taifa”, yaliyofanyika katika viwanja
vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye
aliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Rais, Mhe. Dkt. Nchimbi alisema
Mahakama ina mchango mkubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya
2050 kwa kuendelea kulinda haki, misingi ya Katiba na kuhakikisha migogoro ya
kiuchumi, kibiashara na kijamii inatatuliwa kwa haraka na kwa haki.
Aliongeza kuwa Mahakama imekuwa ikijenga imani kwa wananchi
na wawekezaji kupitia mifumo thabiti ya kisheria, sambamba na kukuza
uwajibikaji, nidhamu katika utumishi wa umma na sekta binafsi, pamoja na
kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa ambao ni msingi wa maendeleo endelevu.
Mhe. Dkt. Nchimbi alibainisha pia kuwa Mahakama ina wajibu
wa kulinda haki za makundi maalum wakiwemo wanawake, watoto na watu wenye
mahitaji maalum, pamoja na kuzuia migogoro inayoweza kusababisha mgawanyiko wa
kijamii na kisiasa.
Maadhimisho hayo yalifanyika mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. George Masaju, viongozi wa serikali, viongozi wa dini, wawakilishi wa
vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya sheria.
Kwa ujumla, Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini yamekuwa
jukwaa muhimu la kutafakari na kuimarisha nafasi ya Mahakama katika kuhakikisha
utawala wa sheria unazingatiwa kama nyenzo ya msingi ya maendeleo na ustawi wa
Taifa.
Sehemu nyingine ya Wageni na wananchi [juu na chini] wakimsikiliza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni