Na. INNOCENT KANSHA- Mahakama
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno amesema
Mahakama ya Tanzania haifanyi kazi peke yake, bali wakati wote hushirikiana na
wadau wengine katika kufikia lengo lake Kuu la utoaji wa haki.
Akisoma hutuba kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mhe. Hamza Johari wakati wa Kilele cha Siku ya Sheria Nchini leo tarehe 2
Februari, 2026 katika Viwanja vya Makoa Makuu ya Mahakama jijini Dodoma Mhe.
Maneno ameongeza kuwa, miongoni mwa wadau wakubwa wa Mahakama ni Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na taasisi zilizo chini yake, ambazo ni
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya
Mwandishi Mkuu wa Sheria zimeendelea kutekeleza majukumu yake katika
kuhakikisha kuwa wananchi na wadau wote wanaifikia haki kwa wakati na hivyo
kuchochea ustawi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Maneno asisitiza kuwa mafanikio ya ustawi na
maendeleo ya Taifa letu yanategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa mfumo imara wa
utoaji haki ulio fanisi, unaoaminika, wenye kufikika na unaozingatia muda. Mahakama
ya Tanzania pekee haiwezi kutimiza lengo hilo. Kwa kushirikiana na wadau wote
wa haki, itaendelea kubaki kuwa nguzo muhimu katika ustawi wa taifa na nyenzo muhimu katika kufikia maendeleo endelevu na jumuishi.
“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, daima tutaendelea
kushirikiana na Mahakama katika kuhakikisha si tu tunaisaidia Mahakama kufikia
maamuzi, lakini pia kuwahudumia watu wote kwa weledi, ubora, uadilifu na
uaminifu ili kiu ya kila anayeikimbilia haki ikatimie kwa wakati. Aidha,
tutaendelea kushirikiana na wadau wengine wote wanaohusika na utoaji haki ikiwa
ni pamoja na Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanzania (TLS) ili huduma za
kisheria tunazozitoa zimfikie kila mtu...
...Milango yetu iko wazi wakati wote na kwa yeyote.
Matamanio yetu makubwa ni kuona Mahakama na wadau wake wote, tukiwamo sisi, hatuwi
kikwazo kwa namna yoyote ile bali, tunaitumia sheria kama nyenzo muhimu kufikia
Taifa lenye ustawi na maendeleo tunayoyataka,” amefafanua Naibu Mwansheria Mkuu
wa Serikali.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Maneno ameongeza
kuwa Mahakama ni mhimili muhimu katika mnyororo mzima wa utoaji haki. Ufanisi
wake una mchango mkubwa katika ustawi wa jamii yetu, kuvutia uwekezaji wa ndani
na nje ya nchi, kuimarisha biashara, na kulihakikishia Taifa maendeleo ya
kiuchumi kupitia uimarikaji na uboreshaji wa mifumo ya haki, na kudumisha usawa
na uwajibikaji katika jamii na taifa. Kwa hakika, katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,
Mahakama ina nafasi muhimu katika kujenga uchumi shindani,
jumuishi na endelevu. Uko usemi maarufu katika sheria unaosema kuwa; “Justice
delayed is justice denied” ikimaanisha
haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa. Lakini kwa muktadha wa shughuli ya
Siku ya Sheria kuna usemi unaofahamika kuwa; “Justice delayed is development
denied” ikimaanisha haki iliyocheleweshwa ni maendeleo yaliyonyimwa,”
amesisitiza Mhe. Maneno.
“Kwa ufupi niyataje machache yanayotekelezwa na
yanayoendelea kutekelezwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama ifuatavyo; upekuzi wa mikataba ambao
umesaidia kuhakikisha mikataba inatekelezeka na inazingatia misingi yote ya sheria,
katika mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya mikataba 3,436 na hati za makubaliano
729 zilifanyiwa upekuzi na Ofisi yangu,” ameongeza Naibu Mwanasheria Mkuu wa
Serikali,
Aidha, Mhe. Maneno ameongeza kuwa, mageuzi ya kimuundo
katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo yameleta ufanisi na tija
kubwa katika mnyororo mzima wa utoaji na usimamizi wa haki;
Uanzishaji wa Kamati za Ushauri wa Kisheria na Kliniki za
sheria katika mikoa na wilaya mbalimbali Nchini. Kliniki hizo, zimetoa huduma
za kisheria kwa wananchi wengi na hivyo kupunguza wingi wa mashauri na kuokoa
gharama za kifedha na muda wa Mahakama na wananchi ambazo zingetumika iwapo mashauri
husika yangeendeshwa Mahakamani.
“Hadi sasa Kamati hizi zimezinduliwa katika mikoa mitano
ya Dodoma, Kilimanjaro, Manyara,
Singida na Mwanza. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2024, Kamati zimehudumia zaidi ya wananchi 2,252 kupitia Kliniki za Sheria ambazo
zinaendeshwa na Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea na watoa huduma
za kisheria wengine. Katika kutekeleza jukumu hili, Ofisi yangu itaendelea
kushirikiana kwa karibu na wadau wote, ikiwemo Wizara ya Katiba na Sheria,
Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanzania (TLS), Chama cha Mawakili wa
Serikali (TPBA), Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika kushughulikia na kutatua
malalamiko ya wananchi yenye mwelekeo wa kisheria kwa wakati na kwa haki,”
amesisitiza Mhe. Maneno.
Mhe. Maneno amesema kwamba Ofisi ya Mwasheria Mkuu wa Serikali
inaendelea kufanya urekebu wa maboresho na ufasili wa sheria mbalimbali ambao
umesaidia kupata rejea za sheria kirahisi. Katika mwaka wa fedha 2024/2025,
miswada 16 ya sheria iliandaliwa, sheria ndogo 1,018 ziliandaliwa na sheria 446
zilifanyiwa urekebu.
“Kwa sasa, tuko katika hatua za mwisho za kukamilisha toleo
la ufasili wa sheria, na zaidi ya sheria 446 zimetafsiriwa kwa lugha ya
kiswahili. Baada ya kukamilika, toleo hili litatolewa bure kwa wananchi, ikiwa
ni utekelezaji wa maelekezo yako katika kuhakikisha wananchi wanazifahamu na
kuzifikia haki zao,” amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mhe. Maneno ameongeza kuwa, mfano mzuri ni mabadiliko ya
sheria mbalimbali Na. 8 ya mwaka 2018 ambayo yamerekebisha Sheria ya Mahakama
ya Rufaa, Sura 141 kwa kuweka kanuni iitwayo “overriding objective” au “oxygen
principle”. Kanuni hii inasisitiza Mahakama kutenda haki pasipo kufungwa na
mambo ya kiufundi (technicalities) pasipo sababu za msingi ili kuendana na
malengo ya Ibara ya 107A (2) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa, Ofisi
yake kwa kushirikiana na Mahakama, na wadau wengine wapo katika hatua za mwisho
za uandaaji wa Muswada utakaoimarisha
vyombo vya kinidhamu kwa Maafisa Mahakama na Muswada wa kuyaingiza Mabaraza ya Ardhi
na Nyumba katika mfumo rasmi wa Mahakama.
Akiendelea kufafanua mikakati mbalimbali ya Ofisi hiyo,
Naibu Mwansheria Mkuu wa Selikali Mhe. Maneno amesema ili kukabiliana na kasi
ya mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya utoaji huduma, Ofisi ya
Mwanansheia Mkuu wa Serikali imejielekeza katika matumizi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Kwa kuanzisha mifumo rahisi kama OAG-MIS ambayo
imeunganishwa na mifumo ya taasisi nyingine za utoaji haki. Mifumo hiyo,
imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi katika kupata huduma na kuzifikia kwa
urahisi sheria mbalimbali.
“Hatua hii pia imehusisha uboreshaji wa huduma za maktaba
za kisheria, usimamizi na upekuzi wa mikataba pamoja na utoaji wa ushauri wa
kisheria kwa njia za kidijitali, kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na
uwajibikaji na tija,” amesema Mhe. Maneno.
Mikakati mingine iliyotekelezwa ni ongezeko kubwa la Mawakili
wa Serikali katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa
Sheria. Ujenzi wa majengo ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya
Taifa ya Mashtaka katika mikoa mbalimbali Nchini, na ufunguaji wa Ofisi ya
Taifa ya Mashtaka katika jumla ya mikoa yote na wilaya 118 nchini. Kuwezesha majadiliano
na usuluhishi wa mashauri nje ya Mahakama;
Vilevile Mhe. Maneno kuwa, Ofisi yake inaendelea kuwekeza
katika ujenzi wa Maktaba Mtandao, uanzishaji wa Kituo cha Huduma kwa Wateja,
pamoja na mifumo ya kisasa ya usimamizi wa mikataba kwa njia ya mtandao. Aidha,
mafunzo ya ndani na nje ya nchi yanaendelea kutolewa kwa Mawakili wa Serikali
ambao pia ni Maafisa wa Mahakama, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa
weledi na ubora unaoendana na matakwa ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na wadau wengine, inaendelea kufanya tafiti na mapitio ya kisheria yanayolenga kuboresha mifumo ya utatuzi wa migogoro nje ya Mahakama. Hatua hizi zinalenga kupunguza msongamano wa mashauri mahakamani, kuongeza ufanisi wa utoaji haki na kuweka mazingira bora ya uwekezaji na hivyo kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi, amesisitiza Mhe. Maneno.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno akisoma hutuba kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari wakati wa Kilele cha Siku ya Sheria Nchini leo tarehe 2 Februari, 2026 katika Viwanja vya Makoa Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Sehemu
ya Viongozi wa Serikali na wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki sherehe za kilele cha
kuadhimisha siku ya sheria nchini.
Sehemu ya wanakwaya wa Kwaya ya Mahakama ya Tanzania walioshiriki sherehe za kilele cha kuadhimisha siku ya sheria nchini.
Sehemu ya Wajummbe wa Kamati ya Maandalizi ya siku ya sheria nchini wakiwa kwenye picha ya pamoja kwenye siku ya kilele cha kuadhimisha ya siku ya sheria nchini.














Hakuna maoni:
Chapisha Maoni