Na. James Busanya & Arapha Rusheke–Mahakama Dodoma
Rais
wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Msomi Boniface Mwabukusi, leo
tarehe 02 Februari, 2026 ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho mengi
ambayo yamefanyika, akitoa salamu katika maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, amesema
chama hicho kinatambua na kupongeza jitihada kubwa zilizokwisha fanyika na
zinazoendelea kufanywa na Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza
katika kilele cha kuadhimisha Siku ya sheria nchini zikiashiria kuanza kwa
mwaka wa kimahakama zilizofanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Mhakama
yaliyopo Jijini Dodoma Wakili Mwabukusi amesema jitihada hizo ni za kipekee na wanajivunia jitihahada hizo.
Aidha,
akizungumzia kauli mbiu siku ya sheria Nchini 2026 inayosema, mchango
wa mahakama katika ustawi na maendeleo ya Taifa akieleza kufurahishwa
kwake na kauli mbiu ya mwaka huu ambayo imebeba uzito mkubwa unaodhihirisha
ukweli kuwa hakuna maendeleo ya kweli bila haki
“kauli
mbiu hiyo inaakisi umuhimu wa kuweka maslahi ya wananchi mbele bila upendeleo,
huku akisisitiza kuwa katika kutekeleza jukumu lake la kikatiba, Mahakama
imeendelea kutoa haki kwa uwazi, bila upendeleo na kwa wakati ili kuwawezesha
wananchi kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo.”amesema Rais wa TLS.
Wakili
Mwabukusi amesisitiza umuhimu wa Taasisi za Umma ikiwemo Mahakama, Jeshi,
Wizara na Taasisi nyingine kufanya kazi kwa uwazi na uwajibikaji kwa manufaa ya
umma.
Vilevile,
aliendelea kusema kwamba TLS inaamini katika kulinda uhuru na usalama wa Mawakili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kitaaluma, hususani wanapowatetea
wateja wanao tuhumiwa kwa makosa mbalimbali mfano, wizi, ubakaji, ufisadi na
mengineyo, akisisitiza kuwa wakosaji wana haki ya kuwakilishwa kisheria na Mawakili hao wasihusishwe na tuhuma za wateja wao.
Aidha,
ameiomba Serikali kuona umuhimu wa kushirikisha TLS katika mchakato wa uandaaji
wa miswada na marekebisho ya sheria, akieleza kuwa ushirikishwaji huo utasaidia
kuboresha mfumo wa sheria nchini.
Rais
huyo wa TLS amesema Chama hicho kinaendelea kuhimiza uwajibikaji wa wanasheria
katika majukumu yao na kusisitiza kuwa uwakili ni taaluma ya kuhudumia
wananchi.
Ameeleza
kuwa TLS kupitia Ofisi zake nchini kote imetoa huduma za msaada wa kisheria kwa
wananchi 421 ambao 270 wanaume na 151 ni wanawake, kupitia mfuko unaofadhiliwa
na michango ya mawakili wanachama wa TLS. Pia, kupitia ushirikiano wake na
Wizara ya Katiba na Sheria, TLS imewafikia wananchi 3,662,643 kwa huduma
mbalimbali za kisheria.
Kutokana
na ufinyu wa rasilimali fedha, Wakili Mwabukusi ameiomba Serikali kutenga fungu
maalum la kusaidia wananchi wenye uhitaji wa msaada wa kisheria ili TLS iweze
kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuleta usawa katika upatikanaji wa haki.
Amesema
TLS ipo tayari kushirikiana na wadau wote wa maendeleo ya Sekta ya Sheria,
akibainisha kuwa katika ushauri watashauri, katika mema watapongeza na pale
panapohitaji kukemewa watakemea.
Amepongeza
matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR) kupitia Mahakama, akisema
hatua hiyo imechangia kupunguza msongamano wa mashauri mahakamani.
Aidha,
amegusia changamoto ya kutooana kwa mifumo ya vyombo vinavyoshughulikia masuala
ya nyumba, ardhi na Mahakama, akisema wingi huo unaleta mkanganyiko na ni vyema
kupunguza utitiri huo kwa ufanisi zaidi.
Wakili Mwabukusi ameeleza tofauti za mifumo ya utoaji haki kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, akitoa mfano kuwa Zanzibar mtuhumiwa akikaa mahabusu zaidi ya miezi sita hupata dhamana, tofauti na Tanzania Bara kwa baadhi ya makosa yasiyo na dhamana. Ameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa dhamana katika mazingira kama hayo ili kuleta usawa.
Pia
amesisitiza umuhimu wa kuimarisha Shule ya Sheria kwa Vitenda (Law School of Tanzania) kwa kuweka chujio
madhubuti la kitaaluma na kimaadili ili kupata Mawakili wenye sifa stahiki,
akisema si lazima kila Msomi wa Sheria awe Wakili.
Aidha,
ameishauri Serikali kuongeza bajeti kwa ajili ya kuongeza idadi ya Mawakili wa Serikali
ili kuimarisha utoaji wa huduma za kisheria serikalini.
Wakili
Mwabukusi ametoa pongezi kwa Mahakama ya Tanzania kwa maboresho makubwa ya
miundombinu na matumizi ya TEHAMA, pamoja na juhudi za kufuatilia haki ya
dhamana katika mahakama za mwanzo ili kuwawezesha wananchi kupata dhamana kwa
mujibu wa sheria.
Amehitimisha
kwa kusisitiza umuhimu wa usawa mbele ya sheria, uwazi katika uwasilishaji wa
vielelezo vya ushahidi kuwapa fursa upande wa pili kutambua na kuvifanyia kazi na kuhimiza mshikamano katika kuendeleza
haki, usawa na ustawi wa maendeleo kwa wote.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Msomi Boniface Mwabukusi leo tarehe 02 Februari,2026 akitoa hotuba kwa niaba ya Chama hicho wakati wa Sherehe za kilele cha kuadhimisha siku ya sheria nchini zikiashiria kuanza kwa mwaka wa kimahakama, zilizofanyika kitaifa katika viwanja vya Makao makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Sehemu ya Wanafunzi wa Shule
ya Sekondari ya Wasichana Msalato wa walioshiriki sherehe za kilele cha
kuadhimisha siku ya sheria nchini.Sehemu ya watumishi wa
Mahakama ya Tanzania walioshiriki sherehe za kilele cha kuadhimisha siku ya
sheria nchini.
Makamu wa Rais ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mheshimu Balozi Dkt. Emanuel Nchimbi (wa nne kulia) akifuatilia kwa
umakini hotuba ya Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wakili Msomi
Boniface Mwabukusi.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni