Jumamosi, 7 Februari 2026

WATUMISHI WA MAHAKAMA MBEYA WATEMBELEA KITUO CHA KULEA WATOTO YATIMA CHA NURU

Na. MUKSINI NAKUVAMBA - Mahakama, Mbeya

Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Mbeya, wakiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Mbeya, Mhe. Victoria Nongwa, wamefanya ziara ya kutembelea Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Nuru. Ziara hiyo imefanyika tarehe 30/01/2026 na kuhusisha watumishi kutoka Mahakama Kuu Mbeya, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mahakama ya Wilaya pamoja na sehemu ya watumishi wa Mahakama za Mwanzo mkoani Mbeya. Aidha, ziara hiyo pia ilihudhuriwa na wadau wengine katika mnyororo wa utoaji haki, wakiwemo Jeshi la Polisi na Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mbeya.

Watumishi hao walipokelewa na Meneja wa Kituo hicho, Bi. Mary Kassim Himiri, ambaye alitoa maelezo ya utangulizi kwa kuelezea historia fupi ya Kituo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005 hadi sasa, pamoja na hali ya Kituo kwa sasa. Alieleza kuwa kwa sasa kituo kina watoto arobaini (40), ambapo wanne (04) kati yao wamehitimu elimu ya Sekondari Kidato cha Nne mwaka 2025. Aliongeza kuwa baadhi ya watoto wamechukuliwa na watu waliokuwa na nia ya kuwalea, kwa kufuata taratibu zilizowekwa na Kituo hicho kwa kushirikiana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mbeya.

Aidha, Bi. Mary Himiri alizungumzia suala la ufadhili, ambapo alisema kuwa kwa sasa kituo hakina mfadhili wa kudumu na kinategemea misaada midogo midogo kutoka kwa watu binafsi au Taasisi zinazojitolea kusaidia pale inapohitajika.

“Hapo awali tulipata ufadhili kutoka Ubalozi wa Japan ambao walitujengea majengo mawili. Hata hivyo, tangu mwaka 2016, baada ya mwanzilishi wa kituo kufariki, hatuna tena ufadhili wa kudumu. Kwa sasa, tunategemea msaada wa watu binafsi wanaoguswa na hali ya Kituo na kujitolea kusaidia,” alisema Bi. Mary Kassim Himiri, Meneja wa Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Nuru.

Kwa upande wake, Mhe. Victoria Nongwa akizungumza machache baada ya kukabidhi zawadi walizokwenda nazo kituoni hapo, ambapo alitoa shukrani na pongezi kwa uongozi wa kituo kwa kazi kubwa wanayoifanya.

“Tunatambua mchango mkubwa wa asasi hizi katika malezi ya watoto yatima na wenye mahitaji maalum. Tunatoa pongezi za dhati kwa uongozi na walezi wote wa Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Nuru kwa jitihada mnazozifanya. Kwa niaba ya wenzangu wote, tunawashukuru kwa kila hatua mnayopiga, Mwenyezi Mungu awabariki sana,” alisema Mheshimiwa Nongwa.

Ziara hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama Mkoa wa Mbeya, akiwemo Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Mbeya, Mhe. Aziza Temu; Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbeya, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mbeya Mjini, Mhe. Ayubu Shelimo, pamoja na viongozi wengine wa Mahakama Mkoa wa Mbeya.

Ziara hiyo ilihitimishwa kwa kutembelea miundombinu ya Kituo hicho na kufanya mazungumzo ya pamoja na watoto na walezi wao, ikiwa ni ishara na dhamira ya Mahakama amabayo siyo tu katika utoaji wa haki, bali pia katika kushiriki kikamilifu katika ustawi wa jamii.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe. Victoria Nongwa, akizungumza machache wakati wa ziara hiyo.

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Mbeya, Mhe. Aziza Temu (aliyeketi katikati) akiwa sehemu ya watu walioshiriki matatendo ya huruma katika ziara hiyo.

Meneja wa Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Nuru Orphans Centre, Bi. Mary Himiri (aliyesimama katikati), akitoa neno la shukrani baada ya kupokea zawadi.

Sehemu ya watumishi waliotembelea kituoni hapo.

Sehemu ya watumishi walipotembelea kituo cha Nuru Orphans Centre; kutoka kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer; anayefuatia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbeya, Mhe. Tedy Mlimba.

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Mbeya, Mhe. Aziza Temu, akikabidhi zawadi walizokwenda nazo kituoni hapo.


Watumishi wa Mahakama wakiwa kwenye picha ya pamoja na walezi wa kituo, wapili kushoto ni Meneja wa kituo, na wa nne kushoto ni mlezi mkuu wa kituo hicho.


Watumishi wa Mahakama wakiwa kwenye picha ya pamoja na walezi wa Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Nuru Orphans Centre.


Watumishi wa Mahakama wakiwa mbele ya Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Nuru (Nuru Orphans Centre) Mbeya wakati wa ziara hiyo, (kushoto) ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbeya, Mhe. Tedy Mlimba, (wa pili kushoto) ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Mbeya, Mhe. Aziza Temu na wa tatu kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Mbeya, Mhe. Victoria Nongwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni