Na. MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim Charles Tiganga, amewaongoza
watumishi wa Mahakama Kuu ya Kanda hiyo pamoja na wananchi wa Mbeya katika
maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kwa mwaka 2026.
Mhe. Tiganga, ambaye
alikuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo, aliambatana na Mgeni Maalum, Mkuu
wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomoni Itunda, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Mhe. Wakili Beno Marisa. Sherehe hizo zilifanyika tarehe 02 Februari,
2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya.
Akitoa salamu za Mkuu wa
Mkoa, Mgeni Maalum ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomoni Itunda,
aliipongeza Mahakama Kuu ya Mbeya kwa maandalizi mazuri ya maadhimisho hayo.
Aidha, aliwahimiza watumishi wa Mahakama kuendelea kusimamia utoaji wa haki kwa
wakati na kwa wote, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kujiwekea hazina ya
kudumu mbinguni mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake, Mgeni
Rasmi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim
Charles Tiganga, katika hotuba yake alieleza kuhusu maboresho ya kanuni ngumu
yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania kwa lengo la kurahisisha wananchi kupata
huduma za Mahakama na kufanikisha upatikanaji wa haki kwa wote kwa wakati.
Mhe. Tiganga aliongeza
kuwa Mahakama ina mpango wa kuimarisha na kuongeza matumizi ya mifumo ya TEHAMA
ili kurahisisha utoaji wa haki kwa wakati, kupunguza muda wa wananchi kukaa
Mahakamani, na kuwezesha usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao pale
inapowezekana. Aidha, aliwahabarisha wadau na watumishi wa Mahakama kuwa,
kutokana na maboresho hayo, Mheshimiwa Jaji Mkuu anasisitiza kuwa dira ya
Mahakama kwa sasa ni “Utoaji wa haki
kwa wote na kwa wakati zaidi iwezekanavyo.”
Kwa upande wao, Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Mawakili wa Kujitegemea, wote walisisitiza
kuwa kaulimbiu ya Siku ya Sheria kwa mwaka 2026 inaakisi ukweli kwamba hakuna
maendeleo ya kweli bila kuzingatia misingi ya haki, usawa na uadilifu katika
jamii.
Maadhimisho hayo
yalihudhuriwa na watumishi wa Mahakama, viongozi wa dini na jadi, pamoja na
wadau kutoka taasisi mbalimbali wakiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mbeya, Mawakili wa Kujitegemea, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU), Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mbeya, Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji,
na wananchi kwa ujumla.
Mgeni Rasmi na Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim Charles
Tiganga, akisoma hotuba katika maadhimisho ya Siku ya Sheria Mahakama Kuu
Mbeya.
Meza Kuu wakiwa kwenye
picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu Mbeya.
Watumishi na wadau
mbalimbali waliokaa mbele ni Mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya na
Mahakama ya Wilaya, wakiongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Mbeya.
Kwaya ya Mahakama Mbeya
ikitumbuiza wakati wa maadhimisho hayo.
Mgeni Rasmi, Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim Charles
Tiganga, akikagua gwaride maalum la kuashiria kuanza kwa mpya wa kimahakama
2026.
Mgeni Rasmi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim Charles Tiganga, akikagua gwaride maalum la kuashiria kuanza kwa mpya wa kimahakama 2026.
Meza Kuu ikiongozwa na Mgeni
Rasmi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim
Tiganga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa
Mahakama na Serikali, (wa kwanza kushoto) ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya
Mbeya, Mhe. Mussa Pomo, (wa pili kushoto) ni Heshima, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya,
Mhe. Solomoni Itunda (wa kwanza kulia) ni Wakili wa Serikali Mkuu, Bw. Iddi
Mgeni na (wa pili kulia) ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Victoria
Nongwa.
Mgeni Rasmi ambaye ni Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim Charles
Tiganga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa
Mbeya, Wengine (kutoka kushoto walioketi) ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya
Mbeya, Mhe. Mussa Pomo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomoni Itunda (wa pili kushoto), Jaji wa
Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Victoria Nongwa (wa pili kulia) na Wakili wa Serikali Mkuu
kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mbeya.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni