Jumapili, 21 Juni 2026

CHAMA CHA MAHAKIMU NA MAJAJI TAWI LA KILIMANJARO WAKUTANA

  • Wafanya Mafunzo na Kikao Kazi
  •       Jaji Mongela asisitiza utaratibu wa mafunzo ya mara kwa mara

Na JAMES KAPELE, Mahakama-Moshi

Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Kilimanjaro kimefanya kikao kazi cha robo ya kwanza tarehe 19 Juni 2026 kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Tawi hilo Mhe,  Elibahati Petro kwa kujumuisha wanachama kutoka katika Wilaya zote za Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Moshi kwa kufanya mafunzo na kikao kwa lengo la kujijengea uwezo katika masuala ya kisheria na kubuni mikakati mbalimbali ya kimaendeleo katika Tawi hilo.

Awali akifungua mafunzo hayo, Mlezi wa Tawi hilo ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Moshi,  Mhe. Dkt. Lillian Mongella aliwapongeza Wanachama na Viongozi wa Tawi hilo kwa kazi kubwa wanayofanya ya kujitolea kulijenga Tawi lao na kuwa na utaratibu wa kukutana kufanya mafunzo ya kujijengea uwezo katika majukumu ya utoaji haki.

“Nawapongeza sana Viongozi wetu wa Tawi pamoja na Wanachama wote kwa umoja wenu, Tawi hili ni letu mambo tunayopanga lazima tuyatekeleze kwa pamoja, tukifanya hivyo Tawi letu litazidi kuwa imara zaidi. Mmefanya vizuri sana kufanya kufanya kikao kwa kuanza na mafunzo nitafurahi kama mtajenga utaratibu wa kukutana mara kwa mara kujijengea uwezo katika masuala mbalimbali ya kisheria,” alisema Jaji Mongella.

Kikao hicho kilitanguliwa na  Mafunzo yaliyohusishwa mada mbalimbali ikiwemo utoaji wa adhabu mbadala katika mashauri ya jinai, utekelezaji wa amri za Mahakama katika mashauri ya madai pamoja na namna bora ya kupokea ushahidi wa kielektroniki katika Mahakama za Mwanzo.  

Akifunga kikao hicho, Jaji wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Moshi, Mhe. Adrian Kilimi aliwapongeza Wanachama na Watoa Mada kwa kushiriki kikao hicho na kufanya mafunzo ya kujijengea uwezo.

Mhe. Kilimi aliwasisitiza Washiriki kujenga utamaduni wa kufanya hivyo mara kwa mara kwa kuwa, jambo hilo linawajenga katika shughuli zao kila siku pamoja na kupata muda wa kujumuika pamoja.

Alitoa rai kwa Wanachama kupenda kushiriki katika michezo mbalimbali ili kuimarisha afya zao pamoja na kujenga utaratibu wa kujumuika pamoja kwa lengo la kuongeza ufanisi katika majukumu yao ya kila siku. 

Mafunzo na kikao hicho vilihitimishwa kwa tafrija fupi ya kuwapongeza Waheshimiwa Ally Mkama na Jasmin Athuman ambao wameteuliwa hivi karibuni kuwa Naibu Wasajili.

 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Moshi na Mlezi wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Kilimanjaro, Mhe.Dkt. Lillian Mongella  (aliyesimama) akifungua mafunzo na kikao hicho kilichofanyika tarehe 19 Juni, 2026. 


Picha ya pamoja ya Wanachama wa Tawi la Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Kilimanjaro.

Katika picha ni sehemu ya washiriki wakiendelea na majadiliano katika mafunzo hayo. Aliyesimama ni Mwenyekiti wa TMJA Tawi la Kilimanjaro, Mhe. Elibahati Petro akichangia hoja katika kikao hicho.

Wakili wa Kujitegemea Desderius Hekwe aliyealikwa kutoa mafunzo kuhusu Ushahidi wa Kielektroniki katika mafunzo hayo.

Aliyeketi kulia ni Mhe. Aden Kanje, Hakimu Mkazi aliyewasilisha Mada ya Matumizi ya Adhabu Mbadala katika mafunzo hayo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Moshi, Mhe. Adrian Kilimi  (aliyesimama) akifunga kikao hicho.


 (Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni