Jumanne, 13 Oktoba 2026

MAHAKAMA KUU NJOMBE, NMB WASHIRIKIANA KUIMARISHA HUDUMA KWA WATEJA

  • Watumishi   wapatiwa mafunzo ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja na namna bora ya kushughulikia malalamiko

 Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe kwa kushirikiana na Benki ya NMB-Tawi la Njombe, imeendesha mafunzo maalum kwa Watumishi wa Mahakama kuhusu utoaji wa huduma bora kwa wateja na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa kuwahudumia wateja.

Mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, yakiwa na lengo la kuongeza uelewa, kubadilishana uzoefu na kuwajengea watumishi uwezo wa kutoa huduma bora mapema ipasavyo na kwa weledi.

Mratibu wa mafunzo hayo, Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Elisha Mwasomola aliwakaribisha watumishi wote waliohudhuria na kuwatambulisha Maofisa kutoka Benki ya NMB waliokuwa wamealikwa kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yalihusisha watumishi wa Mahakama Njombe pamoja na wengine kutoka Wilaya mbalimbali walioshiriki kwa njia ya mtandao, hatua iliyowezesha watumishi wengi zaidi kunufaika na maarifa yaliyotolewa.

Akitoa neno la utangulizi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano alisisitiza juu ya umuhimu wa watumishi kutoa huduma bora kwa wateja wote wanaofika Mahakamani kupata huduma mbalimbali.

Alieleza kuwa, huduma kwa wateja ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa majukumu ya Mahakama na kwamba kila mteja anapaswa kuhudumiwa kwa kiwango cha juu ili kuhakikisha anaridhika na huduma anayoipata.

“Tunawahudumia wateja mbalimbali wanaohitaji huduma za Mahakama. Hivyo, tunapaswa kuhakikisha tunatoa huduma kwa kiwango cha juu ili wateja wetu waridhike. Mahakama inaelekezwa kutoa huduma bora, na msingi wa maelekezo hayo unatokana na mkataba wa huduma tuliojiwekea na wateja wetu,” alisema Mhe. Luambano.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa aliyekuwa mgeni mzungumzaji katika mafunzo hayo, aliwakaribisha Wawezeshaji wa mafunzo hayo na kusisitiza kwamba, mafunzo hayo ni fursa muhimu ya kujifunza na kubadilishana uzoefu katika kuboresha huduma kwa wateja.

 Aidha, alibainisha kuwa, kitengo cha huduma kwa wateja ni kielelezo cha taswira ya taasisi, kwani namna mteja anavyopokelewa inaweza kuathiri mtazamo wake kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa na taasisi husika.

“Ningependa wote tutambue kuwa, huduma kwa mteja ni zaidi ya kujibu maswali badala yake, inahusisha pia namna maswali hayo yanavyojibiwa kwani, wakati mwingine mteja haulizi swali ili apate jibu sahihi pekee, bali anataka kuona shida yake imepokelewa kwa uzito upi na ni kwa namna gani yeye amejaliwa na mtoa huduma. Kwa sababu hiyo, kila mmoja wetu akitekeleza wajibu wake wa kutoa huduma bora kwa wateja, imani ya wananchi kwa Mahakama itazidi kuongezeka,” alisema Mhe. Nongwa.

Aidha, Mhe. Nongwa alieleza kwamba, huduma kwa wateja ni muhimu sana kwa kuwa inajenga imani ya wananchi (wateja) kwa taasisi, inapunguza malalamiko na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi na wadau wake.

Akizungumza kwa niaba ya Benki ya NMB, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NMB, Tawi la Njombe, Bi. Regina Kavishe aliishukuru Mahakama kwa kuwapa nafasi ya kushiriki katika mafunzo hayo na kueleza kuwa, huduma kwa wateja ni jukumu linalohitaji kujituma, uvumilivu na moyo wa kujali mahitaji ya wengine. Kwa sababu hiyo, alieleza, watumishi wanapaswa kutumia Wiki ya Huduma kwa Wateja kutafakari namna wanavyotekeleza majukumu yao na kutafuta njia bora za kuongeza thamani katika huduma wanazozitoa kila siku.

Bi. Kavishe alifafanua kuwa, huduma ina sifa ya kutokushikika, kutokutenganishika na mtoa huduma na kutohifadhika kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Aidha, alisisitiza kwamba, ili kutoa huduma bora mtumishi anapaswa kumkaribisha mteja vizuri, kumsikiliza kwa makini hadi amalize kueleza mahitaji yake, kumuelewa, kutafakari hatua zinazofaa kuchukuliwa, kutekeleza majukumu kwa wakati na kutoa mrejesho kwa mteja.

Naye Mshauri wa Ubora wa Huduma kwa Wateja wa NMB, Tawi la Njombe, Bw. Erick Luhwago, alieleza kuwa huduma bora kwa mteja ni kumhudumia mtu kwa namna ambayo mtumishi mwenyewe angependa kuhudumiwa.

Bw. Luhwago alielezea kwa kina hatua zinazopaswa kufuatwa katika kushughulikia malalamiko ya wateja. Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kupokea malalamiko, kumsikiliza mlalamikaji kwa makini na kumpa muda wa kueleza tatizo lake, kuandika malalamiko, kufanya tathmini, kuwasilisha malalamiko katika Idara/kitengo husika, kufanya uchunguzi, kutafuta suluhisho na kumpa mteja mrejesho kuhusu hatua zilizochukuliwa.

Bw, Luhwago alisisitiza kuwa, mchakato wa kushughulikia malalamiko unapaswa kuzingatia misingi ya uwazi, uharaka, haki na usiri ili kuhakikisha kila mteja anapata nafasi ya kusikilizwa na kushughulikiwa kwa usawa.

Akizungumzia namna ya kuwahudumia wateja wagumu (difficult customers), Bw. Luhwago alieleza kuwa, watumishi wanapaswa kuwasikiliza wateja hao hadi mwisho, kuwatuliza wanapokuwa na hasira, kuuliza maswali ya ufafanuzi, kufanya uchunguzi wa kina, kutafuta suluhisho linalofaa na kuwashukuru kwa kueleza changamoto zao.

Zaidi ya hayo, Mshauri huyo wa Ubora wa Huduma kwa Wateja wa NMB alibainisha kuwa, baadhi ya wateja wanaweza kuhitaji mbinu maalum za mawasiliano kama vile, wanaopaza sauti, wanaolalamika mara kwa mara, walio na hasira, wanaodai kujua kila kitu, wanaotarajia kupata huduma bila malipo na wale wanaotumia lugha ya matusi au vitisho.

Akihitimisha mafunzo hayo, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Njombe, Bw. Richard Mbambe, aliwashukuru Wawezeshaji kutoka Benki ya NMB pamoja na watumishi wote wa Mahakama kwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo na alieleza kuwa maarifa yaliyopatikana yatawasaidia watumishi kuboresha namna ya kuwapokea na kuwahudumia wateja wa aina mbalimbali kwa weledi, utulivu na ufanisi.

Aidha, aliwataka watumishi kuendeleza na kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Mahakama na Benki ya NMB ili kuendelea kujifunza na kubadilishana uzoefu utakaosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha utamaduni wa utoaji wa huduma bora kwa wateja, huku yakisisitiza juu ya umuhimu wa kusikiliza mahitaji ya wateja, kushughulikia malalamiko kwa wakati na kuhakikisha kila mteja anahudumiwa kwa heshima, haki na weledi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa akizungumza na watumishi wa Mahakama Kanda ya Njombe (hawapo katika picha) alipokuwa akifungua mafunzo ya Huduma kwa Wateja yaliyofanyika hivi karibuni.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano (aliyesimama) akitoa pongezi kwa Maofisa wa Benki ya NMB kwa mafunzo ya waliyoyatoa. Aliyesimama kulia ni Mratibu wa Mafunzo, Mhe. Elisha Mwasomola, na aliyeketi wa kwanza (mwenye miwani) ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Njombe. Wengine wanaoonekana ni sehemu ya washiriki wakifuatilia mafunzo hayo.

Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NMB, Tawi la Njombe, Bi. Regina Kavishe (kulia) pamoja na Mshauri wa Ubora wa Huduma kwa Wateja wa NMB, Tawi la Njombe, Bw. Erick Luhwago, wakisikiliza na kujibu maswali yaliyokuwa yanaulizwa na watumishi wa Mahakama Njombe (hawapo katika picha).

Mshauri wa Ubora wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB-Tawi la Njombe, Bw. Erick Luhwago (kushoto) na Ofisa Mikopo ya Watumishi wa Umma wa Benki ya NMB, Tawi la Njombe, Bw. Noel Urio (kulia) wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa na Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB, Tawi la Njombe, Bi. Regina Kavishe (hayupo katika picha).

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Njombe, Bw. Richard Mbambe akizungumza na Washiriki (hawapo katika picha) alipokuwa akifunga mafunzo hayo.

Baadhi ya Watumishi wa Mahakama Njombe, walioshiriki mafunzo ya Huduma kwa Wateja wakiwa ndani ya ukumbi uliotumika katika mafunzo hayo. Walioketi meza ya mbele ni Wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Benki ya NMB, Tawi la Njombe. Na aliyesimama ni Mratibu wa Mafunzo hayo ambaye ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Elisha Mwasomola.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa (wa pili kutoka kulia), Naibu Msajili Mahakama Kuu Njombe, Mhe. Joseph Luambano (aliyeketi kulia kwa Jaji Mfawidhi) pamoja na washiriki wengine wa Mafunzo ya Huduma kwa Mteja wakifuatilia mjadala wakati wa mafunzo hayo. Walioketi meza ya mbele ni Wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Benki ya NMB, Tawi la Njombe.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

Jumatatu, 12 Oktoba 2026

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA; ABDALLAH ULEGA AJITAMBULISHA RASMI KWA JAJI MKUU MASAJU

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega leo tarehe 12 Oktoba, 2026 amekutana na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju kwa lengo la kujitambulisha rasmi baada kuteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu kushika nafasi hiyo.

Akiwa katika mazungumzo mafupi na Jaji Mkuu ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Ulega ameeleza ameomba ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu na Sekta ya Haki kwa ujumla.

Vilevile, Waziri Ulega ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa miundombinu mizuri ya Majengo sambamba na hatua kubwa iliyopiga katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Kwa upande wake Jaji Mkuu, Mhe. Masaju amemuhakikishia Waziri huyo ushirikiano wa dhati kutoka Mahakama na kusema kwamba ushirikiano kati ya Mahakama na Wizara ya Katiba na Sheria ni takwa la Kikatiba.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akimkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 12 Oktoba, 2026.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega wakifurahia jambo wakati Waziri Ulega alipowasili ofisini kwa Jaji Mkuu leo tarehe 12 Oktoba, 2026 kwa lengo la kujitambulisha.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega akisaini kitabu cha wageni alipowasili ofisini kwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 12 Oktoba, 2026.
Mazungumzo kati ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Viongozi wengine kutoka  Mahakama ya Tanzania na Wizara hiyo.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza jambo wakati wa kikao na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (hayupo katika picha).

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (kulia) akifurahia jambo wakati wa mazungumzo na Jaji Mkuu (hayupo katika picha). Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Balozi Baraka Haran Luvanda.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu akichangia jambo wakati wa mazungumzo katika ya Jaji Mkuu na Waziri wa Katiba na Sheria (hawapo katika picha). Kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akimpatia nyaraka mbalimbali za Mahakama Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdalla Hamis Ulega wakati Waziri huyo alipotembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 12 Oktoba, 2026.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (wa tatu kushoto). Wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Balozi Baraka Haran Luvanda (wa kwanza kulia) pamoja na Viongozi wengine kutoka Wizara ya Katiba na Sheria walioambatana na Waziri.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma (wa pili kulia), Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (wa pili kushoto), Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (wa kwanza kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Balozi Baraka Haran Luvanda (wa kwanza kulia).


Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega akitazama picha za Majaji Wakuu ambazo zimebandikwa ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju.


(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)































 

JAJI MKUU WA UGANDA AFANYA ZIARA YA KIKAZI MAKAO MAKUU YA MAHAKAMA

Na HABIBA MBARUKU-Mahakama Dodoma

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija, pamoja na ujumbe wake leo tarehe 12 Oktoba, 2026 ametembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma na kujionea hatua kubwa zilizopigwa katika utoaji haki nchini, ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ujenzi wa miundombinu ya kisasa inayorahisisha utendaji wa Mahakama huku ikitekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.

Alipowasili Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Zeija alipokelewa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akiwa pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. John Jingu pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania.

Katika ziara hiyo, ugeni huo ulipata fursa ya kutembelea ukumbi mpya wa kisasa wa Mahakama ya Tanzania, pamoja na Chumba Maalum cha Usimamizi wa Taarifa za Mahakama (Judiciary Situation Room) kinachotumika kufuatilia na kuratibu shughuli za Mahakama nchi nzima.

Aidha, ugeni huo ulipata nafasi ya kufanya majadiliano na kubadilishana uzoefu juu ya matumizi ya TEHAMA, pamoja na kufahamu mifumo mbalimbali inayotumiwa na Mahakama katika kufanikisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo ambapo Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso, aliwasilisha mada iliyoeleza muundo, dira, na maboresho mbalimbali yanayoendelea kutekelezwa na Mahakama ya Tanzania.

Akiwasilisha Muundo wa Mahakama, Bw. Uisso amebainisha kuwa, mfumo wa Mahakama nchini umejengwa katika ngazi kuu nne kuanzia Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu yenye divisheni maalum ambazo ni Divisheni ya Kazi, Ardhi, Biashara, Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, hadi Mahakama ya Rufani ambayo ndiyo ngazi ya juu kabisa ya Mahakama.

Bw. Uisso ameeleza kuwa, Mahakama inatekeleza azma yake ya kutoa haki sawa kwa wote mapema ipasavyo kupitia teknolojia, ikiongozwa maadili ya msingi, ambayo ni uadilifu, kutokuwa na upendeleo, uwajibikaji, uwazi, na utaalamu kupitia uadilifu, uwazi, na uwajibikaji, huku kipaumbele kikubwa kikiwa ni kuwaweka wananchi mbele (citizen-centric) ili kujenga imani ya umma.

“Tunatazamia kutoa haki kwa wote kupitia teknolojia, na mwelekeo wetu uko kwa wananchi, yaani unaoweka wananchi mbele (citizen-centric). Hilo ndilo lengo letu, kuhakikisha kwamba wananchi wanapata kile wanachokitazamia kutoka kwetu, tunajikita sana katika kujenga imani ya umma, kwa sababu kama huna imani ya umma, basi watu hawawezi kutumia au kupata kile wanachokitazamia kutoka kwetu,” ameeleza Bw. Uisso.

Akizungumza kuhusu mageuzi ya Mahakama, Bw. Uisso ameeleza kuwa mageuzi ya Mahakama yalianza takribani miaka 10 iliyopita, yaani mwaka 2015 ambapo kuanzia mwaka huo Mahakama imemaliza mpango wa mageuzi ya sekta ya sheria, uliokuwa ukijumuisha Taasisi zote za sekta ya sheria kwa kuongozwa na Wizara, jambo ambalo limeonesha mafanikio kwa Mahakama.

Ameeleza kuwa, eneo lililopewa kipaumbele katika mageuzi ni mabadiliko ya kidigitali ambapo Mahakama ilihakikisha inafanya shughuli za ke kidigitali kwa kujenga mifumo kama vile mfumo wa usimamizi wa mashauri, Mahakama Mtandao Pamoja na mfumo wa kufuatilia takwimu za kiutendaji za Mahakama.

Ameongeza kuwa, eneo lingine lililopewa kipaumbele ni mageuzi ya kisheria na kiutaratibu, ambapo kanuni na taratibu zilianza kurahisishwa pia uanzishaji wa kanuni za ufunguzi wa mashauri kwa njia ya mtandao kanuni za uendeshaji wa mashauri kwa mtandao ili kuwezesha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao.

Aidha, kipaumbele cha miundombinu ya Mahakama ambapo Mahakama imefanikiwa kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki, Mahakama za Hakimu Mkazi, Pamoja na ukarabati wa majengo ya Mahakaman nchi nzima, sambamba na kuimarisha rasilimali watu kwa kuanzisha mafunzo ili kukuza ujuzi na kuboresha mazingira ya kazi kwa kutoa vifaa vya kufanyia kazi, kuwezesha usafiri kwa wafanyakazi.

Sambamba na hayo, Bw. Uisso ameyataja mafanikio yaliyofikiwa kuwa ni ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki 15 nchi nzima, ambavyo vinakusanya huduma zinazopatikana katika ngazi zote za Mahakama chini ya pamoja.

Ameyataja Mafanikio mengine kuwa, ni Matumizi ya TEHAMA yanayohusisha matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa usimamizi wa mashauri (e-case management), usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (virtual hearings), na mfumo wa kurecord kumbukumbu kidijiti ili kuongeza uwazi na ufanisi pamoja na kujenga uwezo wa rasilimali watu kupitia mafunzo endelevu kwa watumishi ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.

Bw. Uisso amefafanua kuwa, katika miundombinu ya TEHAMA kuna intaneti ya mkongo wa baharini yenye kasi ya gigabiti 1.28 kwa sekunde pia mtandao wa nyuzi za fiber (fiber cable) ambao sasa umefika zaidi ya kilomita 7,000 na unafika hadi kwenye makao makuu ya kila wilaya kwa sasa, kwa hiyo inapatikana vizuri, lakini pia inaunganisha baadhi ya nchi jirani ikiwemo Uganda.

Akihitimisha wasilisho lake, Bw. Uisso amesema kuwa katika muelekeo wa Dira 2050, Mahakama ina mpango wa maendeleo wa miaka mitano, mfumo wa kimakakati wa Uchumi wa kidigitali ambayo yatalisha sheria za kitaifa za TEHAMA ambapo ipo Sheria ya Serikali ya Mtandao , Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, pamoja na sheria nyingine zinazosimamia sekta hiyo, ambazo zitaielekeza Mahakama, kufaidika na mipango hiyo, hasa mpango mkakati, pamoja na sera ya TEHAMA huku akiongeza kuwa maboresho haya ya Mahakama yanaingiliana kwa karibu na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi imara na jamii yenye haki, amani na utawala bora.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA-Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock, ameelezea mifumo mbalimbali ya Mahakama na namna inavyofanya kazi kieletroniki ikiwa ni pamoja na mifumo ya e-Case Management, Virtual Court pamoja na namna Chumba Maalum cha Usimamizi wa Shughuli za Mahakama (Judicial Situation Room) kinavyofanya kazi kama Data Hub.

Katika ziara hiyo ambayo Mhe. Dkt. Flavian Zeija, ameambatana na baadhi ya Viongozi wa Mahakama Uganda ambao ni pamoja na Maureen Kasande, Ssinabulya Joseph pamoja na Oryema Brian.

Ziara hiyo imethibitisha ushirikiano madhubuti wa kisheria na kimahakama kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku Uganda na Tanzania zikishirikiana kubadilishana uzoefu katika uboreshaji wa mifumo ya utoaji haki kwa wananchi.

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kulia) pamoja na ujumbe wake leo tarehe 12 Oktoba, 2026 ametembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma na kupokelewa na mwenyeji wake, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju pamoja na Viongozi Waandamizi wa Mahakama.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyesimama mbele kushoto) akimuonesha Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija picha za Majaji Wakuu waliopita hadi wa sasa. 

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija akisaini Kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili ofisini kwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha). 

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija, (kulia kochi mbele) akiwa anateta jambo mara baada ya kuwasili ofisini kwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kushoto) kwa ziara ya kikazi. 

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija mara baada ya kuwasili ofisini kwake jijini Dodoma leo tarehe 12 Oktoba 2026.

Mkurugenzi wa TEHAMA-Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock akitoa maelezo kuhusu (Judiciary Situation Room).

Majadiliano yakiendelea.

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija, pamoja na ujumbe wake wakiwa ndani ya Ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) ili kufuatilia mawasilisho ya taratibu za ujenzi wa mifumo ya TEHAMA  na Miundombinu.

Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso (kulia), aliwasilisha mada iliyoeleza muundo, dira na maboresho mbalimbali yanayoendelea kutekelezwa na Mahakama ya Tanzania. 


Mkurugenzi wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso (kulia), aliwasilisha mada iliyoeleza muundo, dira na maboresho mbalimbali yanayoendelea kutekelezwa na Mahakama ya Tanzania. 

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija akifuatilia wasilisho kutoka kwa Mkurugenzi wa TEHAMA Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock (hayupo katika picha).

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (wa pili kushoto), pamoja na ujumbe wake wamepata pia fursa ya kutembelea Ujenzi wa Nyumba ya Makazi ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju. 

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija, pamoja na ujumbe wake wamepata pia fursa ya kutembelea Ujenzi wa nyumba ya Makazi ya Jaji Mkuu Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju. 

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija pamoja na ujumbe wake wamepata pia fursa ya kutembelea Ujenzi wa nyumba ya Makazi ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju. 

(Picha na MARY GWERA & INNOCENT KANSHA, Mahakama-Dodoma)



Ijumaa, 9 Oktoba 2026

DKT. MAMBI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MKUU WA MKOA WA MANYARA

Na CHRISTOPHER MSAGATI - Mahakama, Manyara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella ofisini kwake jana tarehe 08 Oktoba, 2026 kwa ajili ya kujadiliana masuala mbalimbali ambayo yanahusu ushirikiano wa kikazi kati ya Mahakama na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Mhe. Dkt. Mambi alimshukuru Mhe. Shigella kwa kumkaribisha ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo, kufahamiana na kujadiliana juu ya utendaji kazi na ushirikiano unaopaswa kuwepo baina ya Ofisi hizo.

Aidha, Mhe. Dkt. Mambi alimuomba Mkuu wa Mkoa huyo aweze kusaidia katika suala la upatikanaji wa viwanja kila Kata za Mkoa wa Manyara kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo.

“Kwa kuwa huduma za Mahakama zinaendelea kukua kila siku, tunaomba utusaidie katika michakato mzima wa kupata viwanja pamoja na hati za umiliki katika Kata ambazo hamna huduma za Mahakama ili tuweze kujenga Mahakama hizo na kusogeza huduma karibu na wananchi,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.

Kwa upande wake, Mhe. Shigella alimuahidi Mhe. Dkt. Mambi kutekeleza jukumu hilo kwa kuwasiliana na mamlaka zilizopo chini yake ili viwanja hivyo vipatikane ili kukidhi adhima ya Mahakama ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi.

“Ninatambua kuwa, Mkoa wetu wa Manyara una changamoto ya uhalifu na hususan mashauri ya kijinsia, na migogoro ya ardhi na kwa sababu hiyo ni kweli kila mahali panahitaji kufikiwa na huduma hizi za Mahakama. Kwa sababu hiyo Mhe Jaji nitajitahidi kuwasiliana na viongozi wa Mamlaka nyingine ili tufanikiwe katika upatikanaji wa viwanja na hati hizo,” alisema Mhe. Shigella.

Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi hawa wawili kukutana na kufanya mazungumzo tangu ambapo Mhe Shigella alipohamishiwa kufanya kazi katika Mkoa wa Manyara ambapo awali alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita mnamo Mwezi Septemba, 2026 akichukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga aliyehamishiwa Mkoani Morogoro.

Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Mambi aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava, Naibu Msajili anayefanya kazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Mhe. Mariam Lusewa na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemed.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama alioambatana nao kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella (katikati).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (kulia) akizungumza na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella mara baada ya kumtembelea ofisini jana tarehe 08 Oktoba, 2026.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava akifuatilia mazungumzo kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella.

Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemed (kushoto) akifuatilia mazungumzo kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella. Wengine ni Mhe. Ashery Stanley (katikati) na Mhe. Kuruthumu Mkundawatu (kulia) ambao skwa pamoja ni Mahakimu Wakazi na Wasaidizi wa Sheria wa Jaji.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella mara baada ya kumtembelea katika ofisini kwake.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Mhe. Mariam Lusewa akifuatilia mazungumzo kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha & James Busanya - Mahakama)