Mhe. Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania Mhe. Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Waandishi wa Habari
wote mliopo hapa Kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania na kwa niaba yangu
binafsi napenda kuwakaribisha na kuwatakia Heri ya Mwaka mpya 2015. Kama
mnavyofahamu, kila mwaka Mahakama huadhimisha Siku ya Sheria ambayo
inaashiria mwanzo wa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika. Kwa mara ya
kwanza, Mahakama ya Tanzania itafanya Maonesho ya Wiki ya Sheria kama
sehemu ya Maadhimisho ya siku hiyo muhimu. Maonesho hayo yanatarajiwa
kuanza rasmi tarehe 30.01.2015 na kufikia tamati tarehe 03.02.2015
katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Aidha, Maonesho
haya yanalenga kutoa elimu kwa wadau wa Sheria na kutoa huduma za
kisheria kwa wananchi. Katika kuleta maboresho endelevu Mahakama
imedhamiria kutoa elimu kwa Umma kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo
yafuatayo:- Ufunguaji na uendeshaji wa Mashauri mbalimbali hasa ya
mirathi. Utatuzi wa migogoro kwa njia ya suluhu muafaka (Alternative
Dispute Resolution). Mfumo mpya wa kulipia tozo mbalimbali za
Kimahakama kwa njia ya benki. Katika kufanikisha Maadhimisho haya,
Mahakama kama mwenyeji wa shughuli hii itakuwa ndio mratibu Mkuu wa
kuhakikisha kuwa lengo na madhumuni ya kuanzisha Wiki ya Maonyesho ya
Sheria yanafanikiwa ipasavyo, kwa kuwashirikisha wadau wengi
wanaojihusisha na masuala ya Sheria, haki za binadamu pamoja na
wataalamu na wanafunzi wa Sheria. Wadau wakuu katika Wiki ya Maonesho ya
Sheria ni pamoja na; • Mahakama • Tume ya Utumishi wa Mahakama • Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu Wa Serikali • Ofisi ya Mkurugenzi Wa Mashitaka •
Chuo Cha Uongozi Wa Mahakama-Lushoto • Taasisi ya Mafunzo Ya Uanasheria
Kwa Vitendo Tanzania (The Law School Of Tanzania) • Tume ya Haki Za
Binadamu na Utawala Bora • Taasisi Zinazotoa Msaada Wa Kisheria (Legal
Aid) • Takukuru • Polisi • Magereza • Chama Cha Mawakili Tanganyika •
Tume ya Kurekebisha Sheria Katika Maonesho hayo kutakukwepo pia huduma
mbalimbali zitakazotolewa kama: • Kutolewa vyeti vya Mawakili • Msaada
Wa Kisheria (Legal Aid) • Kupokea malalamiko na kuyatafutia ufumbuzi.
Pamoja na Maonesho haya, kutakuwa na Matembezi maalum ya kuadhimisha
Wiki ya Sheria tarehe. 01.02.2015 ambayo yataongozwa na Rais Mstaafu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Ali Hassan Mwinyi. Matembezi haya
yataanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kupitia barabara za,
Serena-Ohio, Gymkhana-Obama Road, Ikulu, Mahakama ya Biashara, Barabara
ya Kivukoni, Sokoine, Railway, Nkrumah, Lumumba, Mkunguni hadi Mnazi
Mmoja ambapo Mhe. Rais Mstaafu atafanya uzinduzi rasmi wa Maonesho hayo.
Aidha Maudhui ya Maadhimisho ya wiki ya sheria na siku ya sheria nchini
kwa mwaka huu ni: ‘’Fursa ya kupata haki: wajibu wa Serikali, Mahakama
na Wadau.’’ Sherehe za kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini
zitafanyika tarehe 04.02.2015, katika viwanja vya Mahakama vilivyopo
mtaa wa Chimala jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Sherehe hizo zitaanza rasmi kuanzia saa 03:00 asubuhi. Napenda kutoa rai
kwa wananchi na wadau wote wa sheria kutembelea Maonesho hayo kwa ajili
ya kujifunza na kupata huduma mbalimbali za kisheria.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni