Jumatatu, 24 Januari 2022

PROF. JUMA AHAIDI KUENDELEZA USHIRIKIANAO WA KARIBU NA MAHAKAMA ZANZIBAR

Na Innocent Kansha – Mahakama Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemuhakikishia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na Mahakama ya Zanzibar katika maeneo mbalimbali ikiwemo kubadilishana uzoefu, mafunzo na uboreshaji wa huduma hususani matumizi ya teknolojia ili kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini leo tarehe 23 Januari, 2022 katika Viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma, Mhe. Prof. Juma alisema, katika eneo la kubadilisha uzoefu, kumbukumbu zinaonyesha mahusiano hayo yalianza mwaka 1965 hadi 2000 ambapo baadhi ya Mahakimu na Majaji kutoka Bara waliazimwa kufanya kazi huko visiwani Zanzibar.

“Upo umuhimu wa kurudisha ubadilishanaji huo wa uzoefu baina ya Mahakama za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mahakama ya Zanzibar ili kuimarisha mahusiano yenye tija katika kuwahudumia wananchi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema Jaji Mkuu.

Mhe. Prof. Juma, alimpongeza Rais Mwinyi kwa hatua zake madhubuti za kutumia rasilimali ya bahari na faida ya umbo la kijiografia la Zanzibar, kujenga Uchumi wa Bluu kwa faida na manufaa ya wananchi ambapo uchumi wa bluu hugusa sekta mbalimbali, ambazo zinaingiliana na kutegemeana na sekta hizo zinaongozwa na kuratibiwa na sheria mbalimbali. Amesema kuwa baadhi ya sheria hizo zitahitaji kufanyiwa mabadiliko ili zifanikishe uchumi wa bluu na kusimamia ustawi wa rasilimali hizo.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, kama Wanasheria wakizielewa sera na mipango ya ujenzi wa uchumi wa bluu, watakuwa katika nafasi nzuri ya kushauri na kushughulikia aina mpya kabisa ya mashauri ambayo yanaweza kuibuka na kuhitaji ujuzi na maarifa tofauti na yaliyozoeleka.

Akizungumzia Wiki ya Sheria nchini inayoadhimishwa kitaifa Jijini Dodoma, Jaji Mkuu Prof. Juma alisema kuwa kuna wananchi wachache kutoka nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania wanaofahamu kuwa Sheria inasimamia na kuongoza mambo mengi katika maisha yao ya kila siku, mahusiano miongoni mwao na baina yao na serikali, hivyo Mahakama ya Tanzania hutumia nafasi katika Wiki ya Sheria kuwakumbusha wananchi baadhi ya sheria na taratibu za kimahakama ambazo ni muhimu katika maisha yao ya kila siku.

“Hebu tujaribu kujiuliza swali, maisha yatakuwaje endapo kwa siku moja,tutakuwa hatuna sheria, polisi, Mahakama, Magereza, na vingine vya mfano huo. Jibu ambalo tutapata ni kuwa, kazi kubwa ya sheria ni kuondoa yale yote yanayoweza kutokea endapo nchi itakuwa haina sheria au imepoteza utulivu,Aamani udugu na mshikamano”, Jaji Mkuu alisema.

Akifafanua kuhusu kauli mbiu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini, Mhe. Prof. Juma alisema, katika kwenda sambamba na mapinduzi ya Nne ya Viwanda, Mahakama ya Tanzania imeazimia kupata mfumo wa akili bandia

utakaosaidia kuchukua mwenendo na ushahidi mahakamani, kuweka katika mfumo wa maandishi na kutafsiri kwa lugha ya kingereza au kiswahili pale inapohitajika “transcription and translation software”.

“Akili Bandia hii inalenga kumaliza changamoto kubwa uchukuaji na uandishi wa mwenendo na ushahidi kwa mkono pamoja na kutafsiri mwenendo au ushahidi huo kwa kuwatumia Majaji na Mahakimu” aliongeza Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu akaongeza kuwa programu mpya ya Akili Bandia itaondoa changamoto zinazowakabili Mahakimu na Majaji kwa kutumia muda mwingi kuchukua na kuandika ushahidi kwa mkono, itapunguza gharama za usikilizaji wa mashauri na itaongeza uwazi na hivyo kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama.

Kwa upande wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Jaji Mkuu akasema, "Mahakama ya Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA sio tu katika shughuli za utoaji haki, bali katika kutoa huduma nyingine. Wananchi wanakaribishwa katika Wiki ya Sheria kujionea namna Mahakama ya Tanzania ilivyowekeza katika mifumo ya TEHAMA ambayo yamefanikisha maboresho makubwa."

Katika mabanda ya maonesho, wananchi watajionea mfumo wa Usajili, Usimamizi na Utambuzi wa Mawakili (Mjue Wakili Wako - eWakili), mfumo huu unawapambanua mawakili wenye leseni hai na hivyo kustahili kutoa huduma za uwakili.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba kwenye uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini Jijini Dodoma leo tarehe 23 Januari, 2022. Kulia aliyesimama ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi akiwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, taasisi na Mahakama ya Tanzania, akiwemo Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto kwa Rais Mwinyi) wakipasha moto misuli kabla ya kuanza rasmi matembezi ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini Jijini Dododma.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi (katikati) akiwa na Viongozi mbalimbali wa serikali, Taasisi na Mahakama ya Tanzania wakipoza moto misuli kwa kufanya mazoezi mepesi ya viungo mara baada ya kuhitimisha matembezi ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini Jijini Dododma.

Meza Kuu wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimba wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini Jijini Dododma.

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)

 

Jumapili, 23 Januari 2022

ONDOENI KESI ZISIZO NA USHAHIDI MAHAKAMANI

 

Na Magreth Kinabo- Mahakama

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Lubigija Ng’wilabuzu, ameiomba Mahakama ya Tanzania kuondoa kesi zisizokuwa na ushahidi mahakamani, isipokuwa zile zenye mazingira ya kiusalama, mfano kuua au kubaka ili kuweza kupunguza mlundikano wa mahabusu gerezani.

Bw. Ng'wilabuzu, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, ametoa ombi hilo leo tarehe 23 Januari, 2022 baada ya kushiriki katika matembezi ya uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria, ulioandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Ameviomba vyombo husika kushirikiana na Mahakama kuziondoa kesi hizo kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza idadi ya mahabusu katika magereza.

‘‘Uondoshaji wa mashauri haya yasiyokuwa na ushahidi mahakamani utasaidia kupunguza idadi ya mahabusu magerezani, pia utasaidia Serikali kupunguza gharama za kuwahudumia. Hatua hii itawapa fursa Majaji au Mahakimu kupata fursa ya kusikiliza mashauri mengine,’’ alisema Ngw’ilabuzu.

Aliongeza kuwa njia nyingine ya kupunguza mlundikano huo ni vyema mtuhumiwa kupelekwa mahakamani wakati ushahidi ukiwa umeshakamilika.

Kaimu Mkuu wa Mkoa huyo alisema siku za nyuma walikuwa wanapokea malalamiko mengi kuhusu mashauri kukaa muda mrefu mahakamani au kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama, lakini hivi sasa malalamiko hayo hayapo.

Hata hivyo, alisema kuwa changamoto iliyopo ni mashauri ya ardhi, hivyo alishauri wanasheria wa Serikali, Mawakili na Mabaraza ya Ardhi kushirikiana ili kuweza kutatua suala hilo. Pia alisema Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama ili kuboresha miundombinu chakavu.

Aliwaomba wananchi kufika katika viwanja hivyo, ambapo maadhimisho hayo yameaanza leo tarehe 23 Januari, 2022 na yatamalizika tarehe 29 Januari, 2022, ili kupata elimu ya mambo mbalimbali kuhusu masuala ya kisheria. Kauli mbiu ya maashimisho hayo ni ‘Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho kuelekea Mahakama Mtandao’.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma alisema Kanda hiyo imeweza kusajili zaidi ya mashauri 1,871 kati ya mashauri 2,225 yalisajiliwa kwa njia ya mtandao ambayo ni sawa na asilimia 84. Aidha alisema kwa kipindi cha mwezi Desemba pekee jumla ya mashauri 798 yalisikilizwa kwa njia ya ‘Video Conference’ katika ngazi zote za Mahakama.

Alifafanua kuwa Kanda hiyo iliongoza kwa kusikiliza mashauri mengi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mwezi Desemba, ambapo ilisikiliza mashauri 6,352.

‘‘Kanda ya Dar es Salaam katika ngazi zote za Mahakama iliingia na jumla ya mashauri 13, 448 yaliyokuwa yamebakia kipindi cha mwaka 2020, huku jumla ya mashauri 39,031 yalifunguliwa na mashauri 40,146 yalisikilizwa na kubakiwa na mashauri 12, 333. Kati ya mashauri yaliyobakia hadi kufikia mwaka 2021 ni asilimia 15,’’ alisema Jaji Mruma.  

Jaji Mruma alisema ufanisi huo wa kazi umetokana na malengo ya kusikiliza mashauri ndani ya muda uliopangwa.

 

RAIS MWINYI AZINDUA RASMI BENDERA NA NEMBO YA MAHAKAMA

Na Mary Gwera, Mahakama

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi amezindua rasmi Bendera na Nembo ya Mahakama ya Tanzania katika sherehe za uzinduzi wa Wiki ya Sheria zilizoanza leo tarehe 23 Januari, 2022 jijini Dodoma.

Mahakama ya Tanzania kama ilivyo mihilimi mingine imepata Bendera na Nembo yake, hatua ambayo itasaidia kuitangaza na wadau kuijua zaidi Mahakama.

Akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa upatikanaji wa Bendera na Nembo ni sehemu ya mafanikio ya uboreshaji wa huduma mbalimbali unaoendelea mahakamani.

“Mahakama ya Tanzania imefanya uboreshaji wa huduma mbalimbali ukilenga wananchi na wadau. Mojawapo ya uboreshaji wa huduma za Mahakama ni pamoja na kupatikana kwa Bendera na Nembo yake ili kuendelea kuutangaza vyema Mhimili huu,” alisema Mtendaji Mkuu.

Aidha, Prof. Ole Gabriel alieleza kuwa Mahakama imepitia hatua nyingi za kiserikali kuandaa Bendera na Nembo yake ikiwa ni pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali katika usanifu, kutoa maoni na hatimaye kupitishwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na kutolewa kwenye Tangazo la serikali (GN) Na. 787 la tarehe 26 Novemba, 2021.

Aliongeza kuwa mchakato uliowezesha Mahakama kupata Bendera yake ulianza mwaka 2003, yapata miaka 19 hadi sasa ambapo Mwaka 2004 Mahakama ilianza kutengeza sanamu ya Nembo ya Mahakama na kuikamilisha Septemba 2006 na baabaye mchakato wa Bendera ukaendelea kwa kusimamiwa na Majaji Wakuu waliokuwepo kwa nyakati tofauti na kukamilishwa na Mhe. Prof. Ibrahimu Juma, ambaye ni Jaji Mkuu wa sasa.

Alibainisha kuwa Sanamu ya nembo ya Mahakama ipo kwenye jengo la Mahakama ya Rufaa, Dar es Salaam. Nembo ya Mahakama ni yenye alama ya “Lady Justice” aliyeshikilia Kitabu na Mzani. Kitabu kina maana ya matumizi ya sheria katika maamuzi ya haki; na Mzani una maana ya upimaji na ulinganifu wa ushahidi kwa nia ya kutoa haki sawa kwa watu wote.   

Kwa upande mwingine, Bendera ya Mahakama ina alama ya Duara ya Bendera ya Taifa na katikati ina Nembo ya Mahakama. Nje ya duara kuna maneno “The Judiciary of Tanzania” na chini yake kuna maneno “Mahakama ya Tanzania.”

Rangi ya Bendera kwa ujumla wake ni “nyekundu” ikiwa ni alama ya mamlaka yenye maamuzi ya mwisho ya utoaji Haki.

Upatikanaji wa Bendera na Nembo ya Mahakama vitatumika kuitangaza na kiutambulisha mahakama. Nembo itatumika kwenye nyaraka mbalimbali za kiofisi kama barua (Letter heads), ‘Dairy’, Kalenda, ‘notebooks’ ‘minute sheets’ na fulana ‘T-shirts’.  

Kabla ya zoezi la uzinduzi, Rais Dkt. Mwinyi alizindua Wiki ya Sheria kwa kuongoza matembezi maalum yaliyoanzia Mahakama Kuu-Kanda ya Dodoma na kuhitishwa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini humo.

Katika matembezi hayo Rais Mwinyi aliambatana na Mwenyeji wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, baadhi ya Majaji wa Mahakama,  Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Mhe. Jacobs Mwambegele, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi na wadau wengine wanaoshiriki katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoanza kuanzia leo tarehe 23 Januari, 2022 hadi tarehe 29 Januari, 2022.

Mbali na Mahakama, Wadau wengine wanaoshiriki katika Maonesho hayo yanayobebwa na kaulimbiu ya Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho Kuelekea Mahakama Mahakama Mtandao’ ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) na wengine.

Hafla za kilele cha Siku ya Sheria nchini itafanyika kitaifa katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2022 ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi akipandisha bendera ya Mahakama ya Tanzania kuashiria uzinduzi rasmi. Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika leo tarehe 23 Januari, 2022 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma. Wanaoshuhudia uzinduzi huo ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto), Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (wa tatu kulia) na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansansu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi (kulia) akifunua kitambaa kuashiria uzinduzi rasmi wa Nembo ya Mahakama ya Tanzania. Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika leo tarehe 23 Januari, 2022 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma. Anayeshuhudia zoezi hilo kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi akizungumza na Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria ulioenda sambamba na uzinduzi wa Bendera na Nembo ya Mahakama ya Tanzania.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria ulioenda sambamba na uzinduzi wa Bendera na Nembo ya Mahakama katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi (katikati) pamoja na baadhi ya Viongozi wa Serikali, Watumishi na Wadau wa Mahakama wakifanya mazoezi kabla ya kuanza kuongoza matembezi ya uzinduzi wa  Wiki ya Sheria yaliyoanzia katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)-Dodoma hadi Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.