Na. DOTTO NKAJA-Mahakakama, Geita
Kampuni
ya Uchimbaji Madini Mkoa wa Geita (Ashanti Geita Gold Mine Limited) hivi
karibuni ilikabidhi nyumba ya kisasa ya kutunzia vielelezo katika Mahakama Kuu Geita
kama sehemu ya kurejesha huduma kwa jamii.
Kitendo
hicho pia ni kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Geita,
hasa katika utoaji haki kwa wakati na kupunguza malalamiko katika jamii.
Mradi
huo uliokabidhiwa kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Geita, Mhe. Kevin Mhina ulijengwa na kampuni hiyo katika mwaka wa fedha (2024/2025)
baada ya Mahakama kukabiliwa na ufinyu wa nafasi ya kutunzia vielelezo.
Makamu
Rais wa kampuni hiyo barani Afrika, Bw. Simon Shayo, ambaye aliambatana na Meneja
Mwandamizi eneo la Mahusiano ya Jamii, Bw. Gilbert Mwulia, Mkuu wa Kitengo cha Wanasheria,
Bw. David Nzaligo na Maofisa wengine ndiye aliyekabidhi nyumba hiyo kwa Jaji
Mfawidhi.
Wakati
akikabidhi nyumba hiyo yenye vyumba vitatu, Makamu Rais huyo alisema kuwa msaada
wa ujenzi wa nyumba hiyo ni sehemu ya majukumu ya Kampuni yao kurejesha
wanachokipata kwa jamiii.
Alisema
pia kuwa hawatoishia kujenga nyumba hiyo bali wataendelea kuwezesha kama
uhitaji utajitokeza kwa sababu Kampuni yake inatambua mchango wa Mahakama
katika kutatua changamoto za utoaji haki mkoani Geita.
Naye
Wakili Mwandamizi wa Sheria wa Kampuni hiyo alieleza kuwa moja ya thamani kubwa
katika kampuni yao ni jamii kunufaika kupitia wanachokizalisha, hivyo wameona
ni vyema wajenge nyumba ya kuhifadhia vielelezo kwa sababu mchakatoa mzima wa
utaoji haki unahitaji pia utunzaji salama wa nyaraka.
Jaji
Mfawidhi aliwashukuru kwa jambo kubwa walilolifanya na kueleza kuwa jengo hilo
litasaidia kutatua tatizo la sehemu ya kutunzia vielelezo. Aliongeza kuwa nyumba
hiyo itatumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA kuhifadhi vielelezo ili kwenda na dhima ya Kanda ya Geita ya
matumizi sahihi ya TEHAMA na kuacha matumizi ya karatasi.
Tukio hilo la kukabidhi nyumba lilishuhudiwa na Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Geita, Mhe. Griffin Mwakapeje, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Fredrick Lukuna Viongozi wengine.
Makamu wa Rais wa Kampuni ya Geita Gold Mine Barani Afrika, Bw. Simon Shayo akikabidhi funguo ya nyumba ya kuhifadhia vielelezo kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina
akizungumuza na Viongozi wa Kampuni la Uchimaji Madini Mkoa wa Geita.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina akitoa
shukrani kwa niaba ya watumishi wote wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita kwa
wawakilishi kutoka Kampuni hiyo.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni