Alhamisi, 10 Julai 2025

JAJI MKUU AAHIDI KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA KIMAHAKAMA ZINAZOWAKABILI MAHABUSU, WAFUNGWA

  • Atoa ahadi hiyo alipotembelea Gereza la Isanga Dodoma
  • Apongeza uboreshaji huduma za magereza nchini

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju ameahidi kushughulikia changamoto za kimahakama zinazowakabili mahabusu na wafungwa waliopo gerezani lengo likiwa ni kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.

Mhe. Masaju amebainisha hayo leo tarehe 10 Julai, 2025 wakati akizungumza na Mahabusu na Wafungwa alipotembelea Gereza Kuu la Isanga mkoani Dodoma kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wafungwa na mahabusu waliopo kwenye gereza hilo.

“Kwetu sisi hizi taarifa ambazo tumezipata hapa, malalamiko haya yatatusaidia kutambua tatizo liko wapi, hivyo yatatusaidia kubuni mikakati ya namna ya kushughulikia changamoto hizi ipasavyo na kwa ufanisi,” amesema Mhe. Masaju.

Jaji Mkuu amesema kuwa, moja ya malengo ya kutembelea Gereza hilo ni pamoja na kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati alipomuapisha Mhe. Masaju kushika nafasi hiyo ambapo alimuelekeza kufanyia kazi maoni na mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ikiwa ni pamoja na kuangalia eneo la Magereza.

“Pamoja na kwamba ninapenda kutembelea Magereza mara kwa mara, lakini hii ziara imekuja nikiwa na sababu mahsusi, nilipoapishwa siku ile moja ya maelekezo ambayo Rais aliniambia ni kwamba niyafanyie kazi mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai,” ameeleza Mhe. Masaju.

Ameongeza kuwa, pamoja na kwamba taarifa za Tume hiyo zipo ofisini ni muhimu kuzungumza na wahusika kwakuwa wanatoa picha halisi ya wapi pa kuanzia na kujua ni mikakati gani ya kuweka katika kushughulikia mapendekezo yaliyoainishwa na Tume ya Haki Jinai.

Akizungumzia kuhusu baadhi ya hoja, malalamiko na changamoto zilizotolewa na Mahabusu, wafungwa, Mhe. Masaju amewaahidi kuwa, yatafanyiwa kazi na matokeo yake watayaona. Amewataka pia, Mahabusu na wafungwa hao waendelee kuwa raia wema.

Baadhi ya changamoto zilizowasilishwa na mahabusu na wafungwa kupitia taarifa zao walizowasilisha mbele ya Jaji Mkuu na ujumbe alioambatana nao ni pamoja na ucheleweshaji wa vitabu vya rufani, kukosa nakala za nia, unyanyasaji katika vituo vya Polisi ikiwemo vipigo, mashahidi kutofika mahakamani kwa wakati na kadhalika.

Aidha, Jaji Mkuu amempongeza Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, Jeremiah Yoram Katungu kwa kuendelea kuboresha huduma za magereza nchini.

“Nalipongeza Jeshi la Magereza kwa hatua kubwa za uboreshaji wa huduma kwa kuwa hali haikuwa hivi siku za nyuma, mimi nimekuwa nikitembelea magereza mara kwa mara, nimetembelea sehemu wanapolala wafungwa wenye adhabu za kunyongwa pameboreshwa sana tofauti na ilivyokuwa awali, vilevile nawapongeza kwa kutumia nishati safi kupikia,” amesema Mhe. Masaju.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, Jeremiah Yoram Katungu akitoa taarifa ya hali ya magereza mbele ya Jaji Mkuu amesema, kwa sasa kumekuwa na upungufu wa wahalifu huku akiishukuru Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano inaotoa pamoja na wadau wengine wa haki jinai.

"Jeshi la Magereza lina jumla ya Magereza 129 nchini, na Magereza haya yana uwezo wa kuhifadhi wahalifu 29,902, kwa tarehe 10 Julai, 2025 tumekuwa na wahalifu pungufu ya nafasi zilizopo, tunahifadhi wahalifu takribani 27,000 kwa siku na nafasi zilizopo ni 29,902 tafsiri yake ni kwamba tumekuwa na upungufu wa wahalifu kulingana na nafasi zilizopo," amesema Kamishna Jenerali Katungu.

Kadhalika, Kamishna huyo, amemshukuru Rais Samia kwa kuunda Tume ya Haki Jinai kwakuwa wamefanyika kazi mapendekezo yaliyotolewa na Tume hiyo kuhusu Magereza na manufaa yake yameanza kuonekana kwakuwa kumekuwa na upungufu wa wahalifu. 

Ameongeza kwa kuushukuru Mhimili wa Mahakama kwa kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo hususani katika usikilizwaji wa mashauri ya mahabusu na wafungwa hususani katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano sambasamba na kaguzi za mara kwa mara zinazofanywa na Majaji. 

Mhe. Masaju amepata fursa ya kukagua maeneo kadhaa katika gereza hilo ikiwa ni pamoja na vyumba wanapolala wafungwa wa kunyongwa, jikoni na sehemu nyingine kadhaa.

Gereza la Isanga limekuwa ni Gereza la kwanza kutembelewa tangu Jaji Mkuu, Mhe. Masaju alipoteuliwa kushika nafasi hiyo. Jaji Mkuu ameambatana na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Emmanuel Mrangu, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, Mwakilishi wa Uhamiaji, Watumishi wengine wa Mahakama na wadau.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na Mahabusu na Wafungwa wa Gereza la Isanga lililopo mkoani Dodoma leo tarehe 10 Julai, 2025 alipotembelea gereza hilo. Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, Jeremiah Yoram Katungu.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju akisisitiza jambo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju (mwenye tai nyekundu) akifanya ukaguzi wa Gereza la Isanga leo tarehe 10 Julai, 2025 alipotembelea gereza hilo. Kushoto kwake ni Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, Jeremiah Yoram Katungu.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju (mwenye tai nyekundu) akiwa katika eneo la Gereza la Isanga Dodoma alipofanya ziara katika gereza hilo leo tarehe 10 Julai, 2025.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju (wa pili kulia) akiwa ndani ya kasha maalum la kisasa lililotolewa na Mahakama linalotumika katika gereza hilo kuendeshea mashauri kwa njia ya mtandao bila washtakiwa kufikishwa mahakamani. Kulia kwa Jaji Mkuu ni Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, Jeremiah Yoram Katungu na anayefuata ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani na kulia kwa Mhe. Dkt. Siyani ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju akikagua gwaride maalum aliloandaliwa na Jeshi la Magereza alipotembelea Gereza la Isanga mkoani Dodoma leo tarehe 10 Julai, 2025.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Gereza la Isanga Dodoma kwa lengo la kufanya ukaguzi.


Sehemu ya Maofisa kutoka Mahakama ya Tanzania wakifuatilia kwa makini kilichokuwa kikijiri wakati wa ziara ya Jaji Mkuu katika Gereza la Isanga mkoani Dodoma.Wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, wa pili kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, katikati ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, wa pili kulia ni Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Emmanuel Mrangu na wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ambaye pia ni Msaidizi Binafsi wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju (wa pili kulia) akipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Gereza la Isanga leo tarehe 10 Julai, 2025 alipotembelea gereza hilo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju (katikati) akiwa katika picha za pamoja na Maofisa wa Mahakama na Magereza na wadau wengine wa Haki Jinai. Wa pili kushoto ni Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, Jeremiah Yoram Katungu, wa pili kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo na wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu.

Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, Jeremiah Yoram Katungu (kushoto) akikabidhi zawadi ya begi kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju baada ya kukamilisha ziara ya ukaguzi aliyofanya katika Gereza la Isanga lililopo jijini Dodoma.

Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, Jeremiah Yoram Katungu (kushoto) akimkabidhi zawadi Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (kulia). Anayeshuhudia katikati ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju na wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania, Jeremiah Yoram Katungu.

(Picha na MARY GWERA na ARAPHA RUSHEKE, Mahakama-Dodoma)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni