Alhamisi, 10 Julai 2025

TANZIA; NAIBU MSAJILI MAHAKAMA KUU KANDA YA ARUSHA, MHE. FRANCIS KABWE AFARIKI DUNIA


Marehemu Francis Jacob Kabwe enzi za uhai wake.

 TANZIA

Mahakama ya Tanzania inasikitika kutangaza kifo cha Mtumishi wake aliyekuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Francis Jacob Kabwe. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 10 Julai, 2025 na Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Amir Msumi, marehemu Kabwe alifikwa na umauti Siku ya Jumanne tarehe 08 Julai, 2025 katika Hospitali ya KCMC Moshi mkoani Kilimanjaro alipokuwa akipatiwa matibabu.

Mhe. Msumi amesema kuwa, taratibu za mazishi zinaendelea kufanyika na marehemu Kabwe anatarajiwa kuzikwa Siku ya Jumapili tarehe 13 Julai, 2025 katika eneo la Mamba Miamba Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Marehemu Kabwe alizaliwa tarehe 20 Novemba, 1976 mkoani Kilimanjaro na kupata elimu katika Shule ya Sekondari Bulima mwaka 1995 na Shule ya Sekondari Ikizu mwaka 1998.

Aidha, Mhe. Kabwe alihitimu katika Chuo Kikuu cha Tumaini-Iringa mwaka 2002 ambapo alisomea taaluma ya Sheria.

Marehemu Francis Kabwe aliajiriwa na Mahakama tarehe 19 Mei, 2003 na kuanza kufanya kazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi mkoani Kilimanjaro na kufanya kazi katika vituo mbalimbali vya Mahakama nchini. Aliteuliwa kuwa Naibu Msajili mwaka 2009.

Mhe. Kabwe alianza kuugua mwaka 2021 ambapo amekuwa akipata huduma ya matibabu katika hospitali mbalimbali ndani na nje ya nchi hadi alipofariki dunia tarehe 08 Julai, 2025. Marehemu ameacha Mke na Watoto wawili.

Mahakama ya Tanzania inaungana na ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba huo mzito wa kuondokewa na Mpendwa wetu.

BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA, JINA LAKE LIHIMIDIWE. 

 

 


 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni