Alhamisi, 10 Julai 2025

MENEJIMENTI KANDA YA MBEYA YAFANYA KIKAO CHA ROBO YA NNE YA MWAKA 2024/2025

Na Daniel Sichula – Mahakama, Mbeya

Menejimenti Kanda na Mahakama Mkoa wa Mbeya imekutana na kufanya kikao cha robo ya nne mwaka 2024/2025 ikiwa ni mwendelezo wa vikao vya menejimenti kwa kila robo ya mwaka kutathmini utendaji kazi wa Mahakama Kanda na mkoa Mbeya.

Aidha, vikao hivyo vilivyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na kuongozwa na Mwenyekiti wa vikao hivyo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga, huku katibu wake akiwa Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda Mbeya Bi. Mavis Miti.

Akisoma taarifa ya maazimo ya kikao kilichopita cha robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 katibu wa kikao hicho Bi. Mavis Miti aliwasilisha maazimio na utekelezaji wa maazimio hayo kwa wajumbe ikiwa ni ushughulikiaji wa mashauri ya mirathi, matumizi ya TEHEMA kwa watumishi wa Mahakama hasa katika uendeshaji wa mashauri kwa njia ya mtandao na kusajili mashauri kwa njia hiyo.

Vilevile, Mtendaji wa Mahakama Kuu Mbeya Bi. Mavis Miti na Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Songwe Bw. Sostenesi Mayoka walitoa taarifa ya hali ya majengo ya baadhi ya Mahakama kuwa katika hali ambayo siyo nzuri ambayo inahatarisha usalama wa watumishi, pia hali ya ukosefu wa watumishi katika Mahakama za Mwanzo za Kanda hiyo ya Mbeya.

Kwa upande wake, Mhe. Joachim Charles Tiganga aliwapongeza wajumbe kwa kufanyaji kazi mzuri katika vipaumbele walivyoazimia hasa katika kushughulikia mashauri ya mirathi kwa wakati na kuwahimiza wanaodai mirathi kurudi kufunga mashauri yao ya mirathi pamoja na matumizi ya Mahakama mtandao katika kusajili na kuendesha mashauri kwa njia hiyo.

Mhe. Tiganga aliwataka wajumbe waendelee kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana kwa kila ngazi katika kutekeleza majukumu na maazimio waliyojiwekea ili kufikia malengo ya kile tunachokifanya.

“Ningependa kutoa rai kwa wajumbe tuliopo hapa tufanye kazi kwa bidii na weledi na kuongeza ubunifu ili kukabiliana na changamoto katika sehemu zetu kazi”

Mhe. Tiganga pia aliwapongeza kwa jitihada wanazofanya Mahakimu katika utoaji wa hukumu na kupunguza mahabusu magerezani ikiwa ni malengo yaliyowekwa toka kikao cha robo ya kwanza ya Mwaka 2024/2025.

Wajumbe wa vikao hivyo walipokea taarifa za Mirathi kwa ngazi zote za Mahakama na taarifa za utekelezaji wa shughuli za kimahakama na kiutawala na kupitia maazimio mbalimbali yaliyowekwa kwa robo ya tatu na kufahamu utekelezaji wa maazimio hayo hasa katika kupunguza mashauri ya mlundikano, kutovuka na madeni ya wazabuni, na utoaji wa mafunzo kwa watumishi wa Mahakama.

Miongoni wa wajumbe walioshiriki vikao hivyo ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Tanzania kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu, Hakimu Mfawidhi Mahakama Mkoa Mbeya Mhe. Zawadi Laizer na Hakimu Mfawidhi Mahakama Mkoa wa Songwe Mhe. Francis Kishenyi pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim C. Tiganga (katikati), Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe.Aziza Temu (Kulia) na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Bi. Mavis Miti Kushoto wakiongoza vikao vya Menejimenti Kanda na Mkoa wa Mbeya. 

Sehemu ya wajumbe wakifuatilia kikao cha menejimenti kanda

Sehemu ya wajumbe wakifuatilia kikao cha menejimenti kanda

Hakimu Mfawidhi Mahakama Mkoa wa Songwe Mhe. Francis Kishenyi (kulia) na Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Songwe Bw. Sostenesi Mayoka wakifuatilia kikao hicho.

                 Sehemu ya wajumbe wakifuatilia kikao cha menejimenti kanda


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni