Jumatano, 9 Julai 2025

TUSIVUKE MWAKA NA MASHAURI YA MLUNDIKANO; JAJI NDUNGURU

 Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Iringa

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan Ndunguru ameongoza Kikao cha Menejimenti ya Kanda hiyo  na kutoa rai kwa Mahakimu wa Kanda hiyo kutovuka mwaka huu na mashauri ya mlundikano kwenye vituo vyao  hasa Mahakama za Mwanzo.

Akizungumza katika Kikao cha Menejimenti cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika jana tarehe 08 Julai, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, Mhe. Ndunguru ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kikao hicho alisema uwepo wa mashauri ya mlundikano hauleti tija kwa Mahakama hizo.

Aidha, Mhe. Ndunguru aliwataka wajumbe wa kikao hicho kufanya kazi kwa bidii na uadilifu pamoja na kuwatia moyo watumishi walio chini yao wanaofanya kazi ndani ya Mikoa ya Iringa na Njombe.

“Ni vema kuwasimamia watumishi na kuwaongoza katika utendaji wa majukumu ya kila siku pamoja kuwakumbuka watumishi ambao wapo chini yenu kwa mambo mazuri ili waweze kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu,” alisema Jaji Ndunguru.

Vilevile, Mhe.Ndunguru aliwataka wajumbe hao kufanya kazi kwa ubunifu ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utendaji wao wa kazi na kuhakikisha chochote kinachokwamisha utendaji kazi kinatatuliwa kwa kubuni mbinu mbadala.

Lengo la kufanyika kwa kikao hicho ni kutathmini  utendaji kazi wa Mahakama za Mikoa ya Iringa na Njombe inayounda Kanda ya Iringa.

Wajumbe wa kikao hicho walipokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za kimahakama  na utawala ambazo maazimio mbalimbali yaliwekwa  kwa ngazi zote za Mahakama za Mkoa wa Iringa na Njombe ili kuhakikisha huduma za haki zinawafikia wananchi kwa wakati.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Dunstan  Ndunguru ambaye ni Mwenyekiti wa Kikao cha Menejimenti  akizungumza jambo na wajumbe wa kikao hicho tarehe 08 Julai, 2025. Kulia ni Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Iringa, Bw. Noel Shayo na kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe.Bernazitha Maziku.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa,  Mhe.Japhet Manyama ambaye ni mjumbe wa kikao hicho akifafanua jambo mara baada ya kusomwa kwa ajenda na taarifa za Mahakama za Mkoa wa Iringa na Njombe.

Kaimu Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bi. Happy Merere akiwasomea wajumbe walioshiriki kwenye kikao cha menejimenti taarifa ya utekelezaji wa kazi za utawala kwa Mkoa wa Njombe.

Picha ya juu na chini ni sehemu ya wajumbe wa kikao cha Menejimenti ya Kanda ya Iringa wakisikiliza kwa makini taarifa zinazotolewa wakati wa kikao hicho.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni