Jaji Mkuu wa Kenya Mhe. Dkt. Willy
Mutunga (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuipongeza Mahakama ya
Tanzania kwa utendaji wake wa kusikiliza na kuamua mashauri mengi yanayopelekwa
mahakamani. Kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman na
Kulia ni Jaji Kiongozi Mhe. Shaan Lila.
Jaji Mkuu wa Kenya
ametoa pongezi hizo mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam mara
baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama
ya Rufani wa Mahakama ya Tanzania kufuatia mwaliko alioupata wa kuhudhuria
maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yatakayofanyika Februari 4 mwaka huu.
Mhe. Dkt. Mutunga
amesema kuwa nchi ya Kenya mpaka sasa ina mashauri yapatayo 300,000
ambayo bado hayajaamuliwa na kuongeza kuwa asilimia 5 ya wananchi wa Kenya ndio
hupeleka mashauri yao Mahakamani huku asilimia 95 iliyobaki wakitafuta ufumbuzi
wa kesi zao nje ya Mahakama.
“Ni kweli Tanzania
mnafanya vizuri katika katika kusikiliza mashauri kwa haraka, asilimia 95 ya
Wakenya hutafuta ufumbuzi wa kesi zao kwa viongozi wa kidini na Kimila kutokana
na baadhi yao kukosa fedha za kutosha za kufuatilia na kugharamia kesi zao”
Amesema.
Ameongeza kuwa Mahakama
ya Kenya kwa mwaka huu 2016 imejipangia malengo ya kuhakikisha kuwa
inasuluhisha mashauri yote ndani ya mwaka mmoja ili kuongeza ufanisi na imani
kwa wananchi.
Ameeleza kuwa Tanzania
ina jambo la kujifunza kutoka Kenya kufuatia mageuzi ya Katiba iliyoyafanya mwaka
2010 hususan kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo na nafasi ya Mahakama kwenye
Katiba Mpya ambayo Tanzania inaendelea na mchakato wake.
Akizungumzia mageuzi
hayo ambayo tayari Kenya imeyafanya kufuatia kuwepo kwa Katiba mpya Mhe.
Mutunga amesema kuwa ni pamoja kupungua kwa madaraka ya Rais katika kuteua
Majaji, na nafasi za Majaji kutangazwa na watu kupeleka maombi na sifa zao
kujadiliwa ambapo wananchi huruhusiwa kutoa maoni kwa Tume ya Mahakama ya Kenya
kuhusu majaji hao kabla ya kuapishwa.
Aidha, ameeleza kuwa
Watanzania wana kila sababu ya kujivunia umoja na mshikamano uliopo ambao
umesababishwa na waasisi wa taifa hilo huku akibainisha kuwa majadiliano na
upatikanaji wa Katiba Mpya nchini Tanzania utafanywa na Watanzania wenyewe kwa
ufanisi mkubwa kwa kuwa Watanzania ni walimu na mfano wa kuigwa katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki na Bara la Afrika.
Kwa upande wake Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akizungumzia ujio wa Jaji Mkuu wa
Kenya amesema kuwa Mahakama ya Tanzania imenufaika na ujio wake kwa kuwa iko
kwenye maadhimisho ya Wiki ya Sheria ambayo huwakutanisha wadau mbalimbali wa
sheria kujadili changamoto na mafanikio ya Sekta ya Sheria nchini.
Amesema kufuatia ziara
ya Jaji Mkuu wa Kenya Mhe. Dkt. Mutunga Mahakama ya Tanzania imejifunza masuala
mbalimbali ambayo ni muhimu katika ufanisi wa shughuli zake ikiwemo uboreshaji
wa Maslahi ya Watumishi wa Mahakama, Jukumu la Mahakama kutafsiri Katiba kwa
kuangalia historia, uchumi pamoja uanzishwaji wa utaratibu wa kuazima baadhi ya
hukumu zilizotolewa nchini Kenya kama ushauri.
Aidha, amesisitiza kuwa
Mahakama ya Tanzania inao wajibu wa kuendelea kuongeza uwazi katika upatikanaji
wa watendaji wenye nia ya kuwatumikia wananchi pamoja na kuboresha njia
za kuwapata majaji wa Mahakama ili kuongeza ufanisi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni