Alhamisi, 9 Juni 2016

JAJI MKUU WA TANZANIA AFANYA ZIARA YA KUKAGUA MIRADI YA UJENZI WA MAHAKAMA ZA WILAYA NA MWANZO ZILIZOPO KIBAHA NA KIGAMBONI




 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Hussein Kattanga akimwelezea jambo  Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman alipokuwa akikagua ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Dar es Salaam. Kushoto ni Mhe. Jaji  Mteule wa Mahakama ya Rufani, Shabani Lila  aliyekuwa Jaji Kiongozi na Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman leo amefanya ziara ili kukagua miradi ya ujenzi wa Mahakama za Wilaya na Mwanzo zinazojengwa mjini Kibaha na Kigamboni.


Aidha, katika ziara hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Hussein Kattanga alimweleza Jaji Mkuu kuwa Mahakama ya Tanzania imeamua kutumia Teknolojia ya kuongeza ufanisi kwa ubora wa hali ya juu na gharama nafuu iitwayo Moladi.
Alisema kupitia Teknolojia hiyo, jengo huweza kukamilika ndani ya siku 45 mpaka 70 huku ikiokoa gharama za ujenzi kwa kati ya asilimia 40 na 45.

Alisema kutokana upungufu mkubwa wa Mahakama nchini Mahakama ya Tanzania iliunda timu iliyokishirikisha Chuo Kikuu cha Ardhi na Baraza la Ujenzi la Taifa (National Construction Council) ili kutafiti teknolojia itakayotumia muda mfupi na yenye gharama nafuu kujenga majengo ya Mahakama nchini. 
 
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, ujenzi unaoendelea sasa katika maeneo ya Kibaha, Kigamboni, Mkuranga, Bagamoyo, Kinyerezi, Kawe na Ilala ni sehemu ya utafiti wa teknolojia hiyo ili baadaye itumike kwenye ujenzi wa mahakama nyingine katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema Mahakama ina upungufu wa majengo katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kuna majengo 960 tu wakati mahitaji ni kuwa na majengo 3963 katika kila kata nchini. Aliongeza kuwa kupitia teknolojia hii mahakama itajenga majengo bora na mengi kwa kipindi kifupi.

Moladi ni teknolojia inayotumika kujenga nyumba bora kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu iliyoanzishwa nchini Afrika ya Kusini mwaka 1986 ambapo ukuta unaojengwa kwa kutumia teknolojia hii hukauka kwa siku moja ili kupisha hatua nyingine ya ujenzi kuendelea.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Hussein Kattanga akimwonesha Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman ramani ya jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Kigamboni, Dares Salaam.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman (mbele) akiwa ameambatana Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Engi. Evarist Ndikilo (aliyepo nyuma mwenye suti ya brown), Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani (T) Mhe. Shaban Ali Lila, (aliye nyuma ya Mhe. Jaji Mkuu), pembeni  ya Mhe. Lila ni Mhe. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania wakikagua jengo la Mahakama lililopo kwenye ujenzi mapema leo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman akifafanua jambo alipokuwa eneo la ujenzi 'site' mapema leo, wa kwanza kushoto ni Eng. Evarist Ndikilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, kulia (mwenye miwani), ni Mhe. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Mhe. Hussein Kattanga, akifafanua jambo kwa Mhe. Jaji Mkuu kuhusiana na teknolojia iliyotumika katika ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mtendaji Mkuu ameeleza kuwa teknolojia inayotumika inaitwa Moladi.

Mafundi wakiendelea na kazi katika ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Kigamboni unaotumia teknolojia ya Moladi.

Mhe. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania akifafanua jambo kuhusiana na mradi wa ujenzi wa Mahakama kwa  gharama nafuu kwa teknolojia ijulikanayo kwa jina la Moladi Mahakama ya Mwanzo Kigamboni pamoja na Mahakama ya Wilaya Kibaha zote zinajengwa kwa teknolojia hii.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni