Na
Lydia Churi-Mahakama
Mahakama ya Tanzania
inatarajia kukamilisha miradi ya ukarabati na ujenzi wa majengo 70 ya Mahakama katika
kipindi cha miaka miwili ili kusogeza karibu huduma ya utoaji haki kwa
wananchi.
Ili kusogeza huduma hiyo
kwa wananchi, majengo ya Mahakama kuu katika mikoa tisa yanatarajiwa kukamilika
katika kipindi cha miaka miwili, Mahakama za Mikoa sita zitajengwa ndani ya
miezi 6-12 wakati Mahakama za Wilaya 19 na za Mwanzo 36 zinatarajiwa kukamilika
ifikapo Desemba 2017.
Akizungumza wakati wa
Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika hivi karibuni, Kaimu Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma alisema Mahakama kwa kushirikiana na Wakala
wa Majengo (TBA), Chuo Kikuu cha Ardhi, Baraza la Ujenzi la Taifa, Benki ya
Dunia na wadau wengine wanaendeleza na kukamilisha miradi ya ujenzi wa Mahakama
Kuu katika mikoa tisa nchini.
Aliitaja mikoa ambayo
majengo ya Mahakama Kuu yatafanyiwa ukarabati na mengine kujengwa ndani ya kipindi
cha miezi 24 kuwa ni Mbeya, Kigoma, Mara, Tanga na Dar es salaam. Mikoa mingine
ni Arusha, Morogoro, Mwanza na Dodoma.
Alisema nia ya
Mahakama ni kuwa na Mahakama Kuu katika kila Mkoa ili kusogeza huduma za
Mahakama kwa wananchi.
“Tunapaswa kuwa na
Mahakama Kuu 26 kwenye kila ngazi ya Mkoa, kwa sasa tunazo Mahakama Kuu kwenye
kanda 14 tu”, alisema Kaimu Jaji Mkuu.
Aidha, mikoa 12
isiyokuwa na Mahakama Kuu ni pamoja na Songwe, Katavi, Njombe, Lindi, Kigoma na
Mara. Mikoa mingine ni Singida, Morogoro, Pwani, Simiyu, Geita na Manyara.
Kaimu Jaji Mkuu
alisema kuwa wakati huo huo, Mahakama ya Tanzania inatarajia kukamilisha ujenzi
wa Mahakama za Hakimu Mkazi katika mikoa sita ya Manyara, Geita, Simiyu,
Njombe, Katavi na Lindi katika kipindi cha kati ya miezi 6 na mwaka mmoja.
Kwa upande wa
Mahakama za Wilaya na zile za Mwanzo, Kaimu Jaji Mkuu alisema wanakusudia
kujenga Mahakama za Wilaya 19 na za Mwanzo 36 ambazo zitakamilika ifikapo
Desemba 2017.
Alisema hatua hii ya
ujenzi wa Mahakama hizi si tu kwamba itasogeza karibu huduma za Mahakama kwa
wananchi bali pia italeta mabadiliko makubwa ya miundombinu ya mahakama na
kuweka historia ya upatikana wa miundombinu kwa wingi na kwa kifundi
kifupi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni