Jumanne, 24 Julai 2018

MAHAKAMA NA TLS KUENDELEZA USHIRIKIANO

Na Magreth Kinabo, Mahakama
Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati  amesema   kuwa Mahakama itaendelea  kutoa ushirikiano  kwa  Chama  cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika  masuala  ya utendaji  kazi kwa kuwa vyombo hivyo vinafanya kazi kwa  kutegemeana.

Kauli hiyo imetolewa leo  na  Msajili Mkuu huyo, wakati  Rais wa TLS,  Fatma Karume   na  baadhi ya viongozi  wa chama hicho, walipotembelea  ofisi za Mahakama Rufani jijini Dar es Salaam.

“Ninashukuru kwa  ushirikiano wenu  mliouonesha kwa kuwa suala la kushirikisha wadau wetu ni miongoni mwa jambo  tunalolipa kipaumbele,” alisema  Revocati.

Aliongeza kwamba Mahakama na TLS ni  kama mtu na dada, hivyo mi muhimu kuendeleza ushirikiano  huo hasa katika Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2015/16 hadi 2019/2020.

Msajili huyo, aliongeza kwamba suala la kuendeleza ushirikiano kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) lipewe kipaumble na TLS ili kuweza kuendana na mabadiliko ya dunia, kama ilivyo Mahakama ya Tanzania inavyolipa msisitizo.

Kwa upande wake Rais wa TLS, Fatma, alisema   aliipongeza  mahakama ya Tanzania kwa kuwasaidia Watanzania kupata haki.

Alisema  TLS ni wadau wa ndani ya Mahakama, hivyo wataendelea kufanya kazi pamoja, kwa kuwa bila Mahakama hawawezi kufanya kazi.

Aidha   viongozi  hao, awali  walipata nafasi ya kumtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania. Pia walielezewa juu ya Mpango Mkakati  wa Miaka Mitano na malengo ya mpango huo na maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama na mfumo  wa kuhifadhi takwimu  kwa njia  ya kielektroniki (JSDS) .
 Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati akimkaribisha Rais wa TLS pamoja na Viongozi wengine TLS alioambatana nao alipotembelea Mahakama ya Rufani mapema Julai 24.

 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akiongea jambo na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bi. Fatma Karume pindi Rais huyo pamoja na Viongozi wengine wa Chama hicho walipomtembelea Mhe. Jaji Mkuu ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam mapema Julai 24, 2018.
 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Bi. Fatma Karume (katikati) na viongozi wengine wa Chama hicho.
 Rais wa TLS na Viongozi alioambatana nao wakifuatilia kwa makini mada kuhusu Mpango Mkakati na Maboresho ya Mahakama ilitolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maboresho-Mahakama, Bw. Sebastian Lacha.
 Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati akifafanua jambo, kushoto ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bi. Fatma Karume.
 Rais wa TLS akifurahia zawadi ya nakala ya Mpango Mkakati wa miaka mitano (5) wa Mahakama ya Tanzania aliozawadiwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati.
 Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bi. Fatma Karume akitoa neno la shukrani mara baada ya majadiliano katika ya TLS na Mahakama, katika majadiliano Viongozi hao wameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano, katikati ni Msajili Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati na kulia ni Mtendaji, Mahakama ya Rufani (T), Bw. Solanus Nyimbi.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni