Na Magreth Kinabo na Lydia
Churi-Mahakama
Mahakama ya Tanzania leo imeingia
Mkataba na Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) utakaowezesha Mahakama
kuingizwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
ambapo majengo 157 ya Mahakama nchini yataunganishwa.
Akizungumza kabla ya kusainiwa kwa Mkataba
huo, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama ya
Tanzania, Bw. Kalege Enock, alisema mkataba
huo wenye thamani ya Sh. bilioni 4.1 utawezesha kuunganishwa kwa majengo ya
Mahakama kuanzia Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Mahakama
za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na baadhi ya Mahakama za Mwanzo zenye
majengo ya kisasa.
Alizitaja Mahakama ambazo zitaunganishwa kwenye mtandao huo kuwa ni
Mahakama ya Rufani 1, Mahakama Kuu 16,
Mahakama Kuu Maalumu (Specialized Division 4, Mahakama za Mkoa 29, Mahakama za
Wilaya 112 na Mahakama za Mwanzo 10.
‘Lengo kuu ni kuunda mtandao mpana wa Mahakama utakao unganisha Mahakama
zote nchini pia kuunganishwa pamoja na mtandao wa serikali yaani
(Government Network (Gov Net) ili kuhakikisha huduma zote za serikali mtandao zinapatikana
kwa urahisi pia kuiwezesha Mahakama kutoa huduma kwa wakati na wakati umadhubuti,’ alisisitiza.
Bw. Enock alisema faida ya mkongo huo ni kurahisisha
upatikanaji wa huduma za mahakama kwa kupitia mifumo yake ya kielektroniki kama vile Mfumo wa kuendesha na
kuratibu Mashauri (JSDS2) na Mfumo wa kuratibu Mawakili (TAMS), mazingira
wezeshi ya kubadilishana taarifa kati ya Mahakama na Taasisi, wadau katika
mfumo mzima wa utoaji haki nchini.
Aliwataja wadau hao kuwa Magereza, Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka,
TAKUKURU, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Chama cha
Mawakili(TLS).
Faida nyingine ni kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi/haraka
kupitia mifumo ya kielektroniki ya Mahakama wakati wote na kutoka mahali
popote, kurahisisha upatikanaji wa taarifa mbalimbali hasa mwenendo wa mashauri
na shughuli za Mahakama kwa wananchi na wadau wengine kwa ujumla.
Aliongeza kuwa faida nyingine ni kupunguza gharama za uendeshaji wa
shughuli za Mahakama, mfano, shahidi anaweza kuwasilisha ushahidi bila
kulazimika kufika Mahakamani, wakili au wananchi anaweza kufungua shitaka au
shauri kwa njia ya mtandao, na kuimarika kwa shughuli za kila siku za Mahakama
kwa kuongeza ufanisi na weledi hivyo kuwezesha upatikanaji wa Haki kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw, Waziri Waziri Kindamba alisema
Shirika lake litahakikisha wanafanya kazi kwa bidii ili kuwezesha Mahakama kuingia
kwenye mtandao.
“Tutafanya kazi usiku na mchana ili tuweze kutekeleza hili kwa wakati, tena
ikibidi kumaliza kabla ya muda uliopangwa katika mkataba wetu, alisisitiza Bw. huo.
Alisema tayari vifaa vimeshasambazwa katika baadhi ya Mahakama na ujenzi
umeshaanza, hivyo watajitahidi kumaliza kazi kabla ya muda.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Bw. Hussein Kattanga alisema mkataba huo utakuwa ukiendeshwa kwa
hatua, ambapo utaanza na wiki 14 za usambazaji wa vifaa na utakuwa endelevu kwa
kipindi cha miaka miwili.
Mahakama ya Tanzania imesaini mkataba huo, ikiwa inatekeleza Mpango Mkakati
wake wa Miaka Mitano ( Julai 2015 hadi
Juni 2020), ambapo moja ya malengo
yake ni kuongeza ufanisi katika mtiririko mzima wa shughuli za Mahakama
na hatua hii itafikiwa kwa kupanua matumizi ya Tehama katika ngazi zote za
Mahakama ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati na pia kusogeza huduma za
Mahakama karibu zaidi na wananchi .
Mahakama ya Tanzania
leo imeingia mkataba na Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) utakaowezesha
Mahakama kuingizwa kwenye mkongo wa Taifa. Pichani ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania Bw. Hussein Kattanga (katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Waziri Kindamba (kulia)wakisaini Mkataba huo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Bw. Mohamed Mtonga.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Hussein Kattanga na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Waziri Kindamba wakikabidhiana Mkataba huo mara baada ya kuusaini.
Wakionesha Mkataba huo kwa wajumbe wa kikao cha Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania mara baada ya kusaini.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Hussein Kattanga (katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Waziri Kindamba (wa pili kulia) wakionesha kwa furaha Mkataba huo mara baada ya kuusaini. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Bw. Mohamed Mtonga. Wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mhe. Kifungo Kiriho Mrisho na wa kwanza kulia ni Mwanasheria wa TTCL.
Wajumbe wa Kikao cha Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Hussein Kattanga (katikati waliokaa), Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Waziri Kindamba (kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Bw. Mohamed Mtonga (kulia) mara baada ya kusainiwa kwa Mkataba huo leo jijini Dar es salaam.
Wajumbe wa Kikao cha Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakiwa katika ukumbi wakisubiri kusainiwa kwa Mkataba kati Mahakama ya Tanzania na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania Bw. Kalege Enock akielezea kuhusu Mahakama kuingia kwenye Mkongo wa Taifa wakati wa Hafla ya kusainiwa kwa Mkataba kati ya Mahakama ya Tanzania na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) leo jijini Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni