Na
Festo Sanga, Mahakama ya Hakimu Mkazi- Kigoma
Mahakama kuu Kanda ya
Kigoma imeendesha kikao chake cha kwanza cha mashauriano na wadau (caseflow
management) tangu kuanzishwa kwake rasmi na Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Tanzania
kwa tangazo la Serikali namba 112 la Februari 1, 2019.
Akifungua kikao hicho
mapema Agosti 6, 2019 kilichofanyika katika Jengo la Hakimu Mkazi Kigoma, Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Ilvin Mugeta aliwasilisha maeneo makuu matatu katika
kuhakikisha Kanda ya Kigoma inakuwa ya mfano kwa kumaliza mashauri kwa wakati
ili kuondokana na mrundikano na kupunguza Idadi ya Mahabusu katika Magereza.
“Baadhi ya maeneo yenye
changamoto ni pamoja na baadhi ya Wadau wetu kutotimiza wajibu ipasavyo, mawasiliano
yasiyoridhisha baina ya mtu na mtu, Taasisi kwa Taasisi pamoja na uwezo mdogo
wa wadau wetu katika upelelezi imekuwa ni changamoto inayokwamisha adhima yetu
ya upatikanaji wa haki kwa wakati” alieleza Mhe. Jaji Mugeta.
Mhe Jaji huyo Mfawidhi alitoa
maelekezo juu ya kuwa na mwelekeo sahihi
wa kanda na namna bora itakayoleta matokeo chanya kwa kuwaeleza wajumbe
kuhahakikisha wanaweka mfumo wa uwajibikaji wa pamoja na kuweka maazimio ya
pamoja ikiwa sambamba na kuweka viwango vya kupimika katika utendaji kazi wa
kila siku.
Aidha aliwasisitiza
wajumbe kufungua milango ya mawasiliano ili kuhakikisha wanafikiana kwa wakati
na kupeana taarifa stahiki ikiwa ni pamoja na kila mjumbe kutambua wajibu wake
na kuongeza kuwa upelelezi unapochukua muda mrefu hupelekea kupotea kwa haki za
watu.
Akisoma taarifa ya Kanda hiyo, naye Naibu Msajili wa Kanda
hiyo, Mhe. Hussein Mushi aliwaeleza wajumbe kuwa tangu kuanzishwa kwake mapema
mwezi February, 2019 hadi mwezi Julai, 2019 masjala ya Mahakama kuu kanda ya Kigoma imesajili
jumla ya mashauri 59 ya jinai pekee, mashauri 12 yaliamuliwa na mashauri 47
yamebaki.
Kamati ya kusukuma
mashauri kanda ya Kigoma kwa pamoja walikubaliana kushirikiana katika
kuhakikisha wanaondokana na mlundikano wa mashauri na Mahabusu kwa kila mjumbe
kutimiza wajibu wake kikamilifu.
Aidha baada ya kikao
wajumbe walipata fursa ya kutembelea Jengo la Mahakama Kuu lililopo katika eneo
la Bangwe mkabala na shule ya Sekondari Kigoma ambako liko katika hatua za
mwisho za ujenzi wake.
Wajumbe waliohudhuria
kikao hicho ni pamoja na Jaji Mfawidhi wa Kanda, Naibu Msajili, Mtendaji wa Mahakama-Kigoma,
Hakimu Mkazi Mfawidhi(M), Mkuu wa Mashtaka Kigoma (M), Mkuu wa Magereza Mkoa wa
Kigoma, Wawakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Polisi, Mkuu wa Upelelezi, Mkuu wa
Gereza la Bangwe. na Katibu wa Jukwaa la Mawakili wa kujitegemea Kigoma (M).
Naibu msajili wa
Mahakama Kuu Kanda Kigoma, Mhe. Hussein Mushi (Aliyesimama) akimkaribisha Jaji
Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Kigom, Mhe. Jaji Ilvin Mugeta(katikati) kwa ajili ya
kufungua kikao cha kusukuma mashauri.
Wadau wa kikao cha
kusukuma mashauri Wakipitia kwa umakini moja ya mashauri ya jinai
yaliyowasilisha katika kikao hicho kilichoketi mapema Agosti 6, 2019.
Picha ya pamoja ya
wajumbe wa kikao cha kusukuma mashauri mara tu walipotembelea Jengo la Mahakama
Kuu Kanda ya Kigoma kujua matumizi ya vyumba na mifumo mbalimbali iliyopo
katika Jengo.
Mandhari ya Jengo jipya
la Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma lililopo katika hatua za mwisho ya
ukamilishwaji ‘finishing’
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni