Mtendaji Mkuu, Mahakama
ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga amefanya ziara ya ukaguzi wa ukarabati unaoendelea
wa jengo la Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga.
Ukaguzi huo umefanyika
Agosti 06, 2019, mbali na ukaguzi wa ukarabati wa Mahakama Kuu katika Kanda
hiyo, Mtendaji Mkuu ambaye aliambatana na baadhi ya Maafisa mbalimbali wa
Mahakama alipata fursa pia ya kutembelea Mahakama ya Mwanzo Laela na kukagua
ujenzi huo.
Mtendaji Mkuu
alionyesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mahakama hiyo ya mwanzo na kuwataka
Wakandarasi wa miradi hiyo kuzingatia mikataba ya miradi hiyo na kumaliza kwa
wakati uliopangwa.
Vilevile aliwataka kuwa
makini katika hatua za mwisho za umaliziaji ‘finishing’ wa majengo hayo.
Katika utekelezaji wa
Mradi wa maboresho wa huduma za Mahakama (CCP) Mahakama ya Tanzania inaendelea
na maboresho kadha wa kanda ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya majengo yake
kwa kufanya karabati mbalimbali pamoja na kujenga majengo mapya lengo likiwa ni
kuwawezesha wananchi kupata haki katika mazingira bora zaidi.
Mtendaji Mkuu-Mahakama
ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga (wa pili kulia) akiwa katika ukaguzi wa jengo
la Mahakama Kuu-Sumbawanga lililopo katika ukarabati.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama (wa pili kushoto)pamoja na baadhi ya Watendaji na Maafisa wengine wa Mahakama walipata fursa ya kutembelea mradi wa ujenzi wa
Mahakama ya Mwanzo Laela-Sumbawanga. Mtendaji alionyesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi
wa mahakama hiyo.
Muonekano wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Laela lililopo katika ujenzi.
(Picha na Mayanga Someke, Mahakama Kuu-Sumbawanga)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni