Jumatano, 18 Septemba 2019

MAHAKAMA KUU- MUSOMA YAKUTANA NA WADAU WA HAKI JINAI


Na Francisca Swai, Mahakama-Musoma

Mahakama Kuu Kanda ya Musoma kwa mara ya kwanza imefanya kikao chake cha kusukuma mashauri (Case Flow) pamoja na wadau wa haki jinai ili kuhakikisha mashauri yanaondoshwa kwa wakati katika Kanda hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho mapema Septemba 17, 2019 kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Jaji John Kahyoza, aliwashukuru wadau wote kwa ushirikiano wanaouonyesha na kuwataka kujitoa zaidi ili kuhakikisha shughuli za usikilizwaji wa mashauri hazikwami. 

“Ofisi zote zinazohusika, Mahakama, Ofisi ya Mashitaka, Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa kuhakikisha kuwa sababu zisizo za msingi zinazopelekea kufuta au kuahirisha kesi zinaondoka, upelelezi ukamilike kwa wakati, hati za wito wa kufika Mahakamani ziwafikie walengwa kwa wakati ili mwananchi apate haki yake bila kucheleweshwa,” alisema Mhe. Jaji Kahyoza. 

Kwa mujibu wa Jaji huyo Mfawidhi alisema hadi sasa, Mahakama kuu Musoma ina jumla ya kesi 457 na katika kuhakikisha mashauri yanasikilizwa kwa wakati, baadhi ya kesi za Mahakama kuu amewapangia Mahakimu wenye mamlaka za ziada (extended jurisdiction).

Aliongeza kuwa ili kuhakikisha hakuna kinachokwama kutokana na kasi hiyo ya ufunguaji wa mashauri, Ofisi ya Mashitaka na Mkuu wa Upelelezi nao wajitahidi kuhakikisha changamoto zilizo upande wao wanawasiliana na kuona namna ya kuzitatua kwa wakati ili kila mmoja atekeleze wajibu wake ipasavyo.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Jaji Zephrine Galeba alisema kuwa, Kanda hiyo inatakiwa kuwa Mahakama ya mfano. 

“Tunatakiwa kuanza vizuri lakini pia tujifunze kwa wenzetu Mahakama zilizotangulia, mazuri yao na mapungufu ili tujiweke imara zaidi. Mahakama ni kama Hekalu la haki (temple of justice), tujitahidi kuepuka rushwa na malalamiko yasiyo na msingi na hapo ndipo hata sisi wenyewe tutaonekana tunaifanya kazi ya haki na tunatenda haki,” alisisitiza Mhe. Jaji Galeba.

Kwa upande wao, Wadau wamefurahishwa na mwelekeo wa Mahakama kuu Musoma hadi sasa, na  wamefurahishwa kwa kuanza kufanyika kwa vikao hivyo ambapo wamepata fursa ya kujadili na kupata ufumbuzi wa masuala mbalimbali kwa pamoja. 

Mbali na hayo, Wadau hao pia wameahidi kutoa ushirikiano kwa Mahakama mkoani humo kwa kutimiza wajibu wao vyema ili wananchi wapate haki zao kwa wakati. 

Mahakama Kuu Kanda mpya  ya Musoma pamoja na Kigoma zilianzishwa rasmi kufuatia tangazo la Serikali Na. 112 la tarehe Februari 01, 2019.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma (aliyesimama mbele) akiendesha kikao cha Wadau wa Haki Jinai (walioketi).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni