Na
Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa suala la mapambano dhidi ya rushwa
linahitaji utashi wa kisiasa ‘political will’ pamoja na uongozi madhubuti kwa
kila nchi ya Afrika ili kufikia azma inayokusudiwa.
Akizungumza na Wajumbe
wa Bodi ya Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa
Afrika (African Union Convention on Preventing and Combating Corruption-AUCPCC)
mapema Septemba 11, 2019 walipomtembelea Ofisini kwake, Mahakama ya Rufani-Dar
es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa hayo yatapelekea kufikia mafanikio ya mapambano
dhidi ya vitendo vya rushwa barani Afrika.
“Utashi wa Kisiasa
pamoja na Utawala madhubuti ikiwemo Uwazi katika utoaji huduma ni mambo muhimu
yanayohitajika kwa nchi zote za Afrika katika mapambano dhidi ya rushwa,”
alisisitiza Mhe. Jaji Prof. Juma.
Aidha; Mhe. Jaji Mkuu
aliueleza Ujumbe huo kuwa Mahakama ya Tanzania ni moja ya Taasisi iliyopo mstari
wa mbele katika kupambana na vitendo vya rushwa ambapo alisema mapambano hayo yanafanyika
kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia Mpango Mkakati wa Mahakama ambapo nguzo zote
tatu (3) za Mkakati huo zinagusia mapambano dhidi ya rushwa.
“Nguzo hizo tatu ambazo ni Utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa
rasilimali, Upatikanaji na utoaji haki kwa
wakati na Kurejesha imani ya jamii na ushirikishwaji wa wadau zinalenga
katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya haki kwa umma na kwa gharama nafuu,”
alieleza Mhe. Jaji Mkuu.
Hali kadhalika; Mhe.
Jaji Mkuu aliongeza kuwa katika mwendelezo wa Mapambano dhidi ya Rushwa,
Mahakama pia imesambaza mabango maalum ya ujumbe wa mapambano dhidi ya rushwa (yenye
namba za simu) ambayo yamebandikwa katika Ofisi za Mahakama zote nchini na
katika ofisi za Wadau.
Hata hivyo; Mhe. Jaji
Mkuu alikiri kuwepo na changamoto ya wananchi kutojitokea hadharani kutaja
mtu/mhusika anayetuhumiwa na kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Naye; Mwenyekiti wa Bodi
ya Ushauri ya Kupambana na Kuzuia Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika
(African Union Convention on Preventing and Combating Corruption-AUCPCC), Mhe. Miarom
Begoto alimshukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kuwakubalia kumtembelea na kusema kuwa
lengo la Bodi hiyo kutembelea Mahakama ni pamoja na kujua jinsi gani Mhimili
huu unashiriki katika mapambano dhidi ya Rushwa.
“Naamini mapambano
dhidi ya rushwa yatafanikiwa endapo kuna Mahakama imara na Watumishi imara
wafanyao kazi ndani yake,” alisema Mwenyekiti huyo.
Ujumbe wa Bodi hiyo upo
nchini kwa sasa na tayari umefanya mikutano kadhaa ya majadiliano ya
kubadilisha uzoefu kuhusu rushwa na Taasisi mbalimbali nchini ikiwemo Mahakama
na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
(AG), Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na nyinginezo.
Kwa sasa Bodi hii ambayo
makao yake makuu yapo Arusha-Tanzania ina jumla ya nchi uachama 37 za Afrika, Tanzania
ikiwa mojawapo ya nchi mwanachama ambapo iliridhia rasmi uanachama wake mnamo Februari 22, 2005.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Profesa Ibrahim Juma (katikati) akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
katika nchi za Umoja wa Afrika (AUCPCC) mara baada ya kumtembelea mapema
Septemba 11, 2019 ofisini kwake Mahakama
ya Rufani (T) jijini Dar es Salaam na
kuzungumza naye kuhusiana na suala la
mapambano ya rushwa katika mhimili wa Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Profesa Ibrahim Juma akizungumza na
wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika mara baada ya
kumtembelea ofisini kwake leo, jijini Dar es Salaam ambapo alizungumzia kuhusu suala la mapambano ya rushwa katika mhimili wa
Mahakama.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
katika nchi za Umoja wa Afrika wakimsikiliza Mhe. Jaji Mkuu alipokuwa
akizungumza nao walipomtembelea ofisini kwake.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Profesa Ibrahim Juma akiwa na wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa Afrika mara baada ya
kumtembelea ofisini leo, jijini Dar es
Salaam.
Mwenyekiti wa wajumbe
wa Bodi ya Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za Umoja wa
Afrika, Mhe. Miarom Begoto akizungumza
jambo na Mhe.Jaji Mkuu mara baada ya kumtembelea.
Jaji Mkuu akiwaonesha wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
katika nchi za Umoja wa Afrika, bango maalum la mapambano
dhidi ya rushwa la Mahakama ya
Tanzania, wakati alipokuwa akizungumza
nao ofisini kwake leo,jijini Dar es
Salaam.
Katibu wa Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Adrian Kilimi akiwaonyesha kwa karibu bango maalum la mapambano
dhidi ya rushwa la Mahakama ya Tanzania wajumbe hao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni