Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemueleza Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza
Mengistu kuwa uongozi imara ni moja ya chachu ya maboresho yaliyofikiwa na
Mahakama ya Tanzania katika utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya huduma za
Mahakama nchini.
Mhe. Jaji Mkuu aliyasema
hayo wakati akizungumza na Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Mengistu aliyemtembelea mapema
Februari 17, 2020 ofisini kwake, Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam kwa
lengo la kupata uzoefu wa Mahakama ya Tanzania juu ya suala zima la maboresho
na muundo wa utendaji kazi wa Mahakama.
“Mchakato wa maboresho
ya Mahakama umekuwa shirikishi kwa kuhusisha ngazi zote za Watumishi mpaka
ngazi ya Mahakimu, Majaji pamoja na Wadau, suala la maboresho limekuwa
likitamkwa na watumishi mbalimbali, hii ni kulingana na ukweli kuwa uongozi
umekuwa shirikishi katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano
2015/2016-2019/2020,” alieleza Mhe. Jaji Prof. Juma.
Aidha; Mhe. Jaji Mkuu
aliongeza kuwa suala la maboresho ya Mahakama linaenda sambamba na utekelezaji
wa Sera ya Taifa ya Maendeleo.
Mhe. Jaji Mkuu alimueleza
Mhe.Jaji Mengistu kuwa maboresho ya Mahakama yameenda sambamba na mabadiliko ya
Sheria ya Uendeshaji wa huduma za Mahakama ya 2011 ‘Judiciary Administration
Act No.4 of 2011’, hali kadhalika kubadili mitazamo ya kitamaduni miongoni mwa watumishi wa Mahakama.
Hata hivyo; Prof. Juma
alitaja baadhi ya changamoto ambazo Mahakama inakabiliana nazo ikiwemo baadhi ya sheria kutokuwa rafiki kwa mwananchi wa kawaida, changamoto
ya kiteknolojia na nyinginezo.
Kwa upande wake, Jaji
Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Mengistu alimpongeza Mhe. Jaji Mkuu kwa hatua ya
maboresho iliyopigwa na Mahakama ya Tanzania.
Mhe. Jaji Mkuu huyo
alisema kuwa baadhi ya changamoto za Mahakama zipo katika Mahakama zote na si
tu kwa upande wa Tanzania hivyo ni kuendelea kuzifanyia kazi.
Aidha; katika mazungumzo baina ya pande zote
mbili, Tanzania na Ethiopia walidokeza juu ya matumizi ya Usuluhishi ‘mediation’
hivyo ni muhimu kuongeza nguvu katika kutilia mkazo suala hili.
Mara baada ya
mazungumzo hayo, ujumbe kutoka Ethiopia ukiongozwa na Jaji Mkuu wa nchi hiyo,
waliwasilishiwa mada ya safari ya maboresho ya Mahakama iliyowasilishwa na Mkuu
wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma.
Jaji Mkuu huyo yupo
nchini kwa siku tatu lengo likiwa ni kujifunza na kubadilishana uzoefu wa
Maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania. Nchi hiyo ipo
katika Mpango wa Maboresho wa Huduma za Mahakama wa miaka mitatu.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma (aliyeketi mbele) akiwa katika mazungumzo ya pamoja na mgeni wake Jaji Mkuu wa Ethiopia Mhe.
Meaza Ashenafi Mengistu (wa nne kulia), pamoja na Viongozi wa Mahakama ya
Tanzania na( wa pili kulia) ni Mtaalam kutoka Bank ya Dunia, Waleed
Malik.
Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe.
Meaza Ashenafi Mengistu (kushoto) akisisitiza jambo.
Mhe. Jaji Mkuu akimkabidhi zawadi Mhe. Jaji Mkuu wa Ethiopia.
Mhe .Jaji Mengistu wa Ethiopia akimkabidhi zawadi Mhe.
Jaji Mkuu wa Tanzania.
Picha ya pamoja, katikati ni Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza Ashenafi Mengistu, kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, kulia ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, waliosimama ni sehemu ya Majaji,Watendaji Waandamizi wa Mahakama, Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia pamoja na Ethiopia.
Ujumbe kutoka Ethiopia ukiwasilishiwa Mada ya Maboresho ya Mahakama ya Tanzania, mada hiyo imewasilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma.
(Picha na Innocent Kansha, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni