Na Innocent Kansha – Mahakama Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani amewataka Naibu Wasajili
wa Mahakama ya Tanzania kuamua mashauri yatakayotokana na Uchaguzi Mkuu kwa
uwazi, utulivu na kujiamini.
Akifungua awamu ya pili
ya mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa baadhi ya Wasajili na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Siyani amesema kuwa mashauri
ya Uchaguzi yana maslahi kwa Umma na hivyo yanapaswa kushughulikiwa kwa haraka
na umakini kwa kuwa lengo la Mahakama ni kuhakikisha kuwa haki za wananchi
ikiwemo haki ya kuchagua kiongozi wanayemtaka inalindwa.
“Uchaguzi ni miongoni mwa
mambo yanayotumia rasilimali nyingi za Taifa katika kulitekeleza jukumu hilo la
kidemokrasia, hivyo ni imani yangu kuwa mafunzo haya yatachangia kuleta matokeo
chanya katika kupokea na kusikiliza mashauri yatakayohusu uchaguzi muda
utakapofika”, alisema.
Alisema ili uchaguzi uwe
huru na wa haki ni dhahiri Mahakama haiwezi kujitenga na mchakato mzima, siyo
tu kwa maisha ya kila mwananchi bali pia kwa ustawi wa nchi na hivyo Mahakama ni mdau na muhimu katika mchakato mzima wa uchaguzi
ujao.
“Mahakama ndicho chombo
kilichokasimishwa mamlaka ya kutoa haki kwa mujibu wa Ibara ya 107 ya Katiba ya
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama hutumika kutafsiri sheria
mbalimbali, miongoni mwa sheria hizo ni sheria zote zinazosimamia masuala
uchaguzi”, aliongeza Jaji Siyani.
Alisema mara nyingi
wakati wa uchaguzi mkuu, huwa kuna joto la uchaguzi na nyakati hizo mashauri
mbalimbali ya uchaguzi hufunguliwa mahakamani, kwa kuzingatia umuhimu wa
mashauri hayo ni wajibu wa Mahakama kuyapa kipaumbele na uharaka unaostahili. “Ni
lazima tuwe wazalendo kwa kiasi kikubwa pindi tunapoliendea jambo hili muhimu
kwa mustakabali wa nchi yetu”, alisisitiza.
Jaji Siyani aliongeza
kuwa Mahakama inao wajibu wa kuona mashauri yanayohusu uchaguzi yanayofunguliwa
mahakamani yanaisha kwa wakati na haki inapatikana bila uvunjifu wa amani.
Mafunzo haya ni
muendelezo wa mafunzo yaliyoanza kutolewa kwa Majaji wafawidhi na Majaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusu namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya Uchaguzi
Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani akifungua mafunzo ya
namna bora ya uendeshaji mashauri ya uchaguzi kwa Wasajili na Naibu Wasajili
wa Mahakama Kuu ya Tanzania yanayofanyika katika ukumbi wa Jengo la Takwimu
Jijini Dodoma.
Mkufunzi wa mafunzo Jaji Mstaafu
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Robert Makaramba akitoa ufafanuzi wa jambo
wakati wa mafunzo hayo.
Wakufunzi wa mafunzo ya
namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Wasajili na Naibu
Wasajili wa Mahakama ya Tanzania. Kushoto ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Mhe. Robert Makaramba na kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Mr. Emmanuel Kawishe.
Wasajili na Naibu
Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa kwenye Mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi yanayofanyika katika ukumbi wa Jengo la
Takwimu Jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni