Na Mayanga Someke- Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga Mhe. David Mrango amesema uzuri wa majengo ya Mahakama yanayojengwa hivi sasa hauna budi kuambatana na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akizindua majengo mawili mapya ya Mahakama ya Mwanzo Msanzi iliyopo wilayani Kalambo mkoani Rukwa na Mahakama ya Mwanzo Mtowisa iliyopo Sumbawanga, Jaji Mfawidhi amesema ujenzi wa majengo hayo ni matokeo ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania katika mkoa huo.
Jaji Mrango alisema katika mwaka wa fedha wa 2018/2019, mkoa wa Rukwa ulipata miradi mitatu ya ujenzi wa Mahakama za mwanzo za Msanzi (Kalambo), Mtowisa na Laela zilizopo Sumbawanga.
“Uzuri wa majengo haya uambatane na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi, watumishi wa Mahakama wanapaswa kubadili mienendo na tabia zinazokiuka miiko na maadili ya kazi na Utumishi wa Umma ili waweze kutoa huduma kwa ubora unaostahili”, alisema.
Jaji Mfawidhi alitoa rai kwa viongozi kuhakikisha kuwa watumishi wote wa Mahakama wanatoa huduma nzuri zinazoendana na uzuri wa majengo. “tujiepushe na lugha zisizofaa kwa wateja wetu ambao ni wananchi na wadau, tujiepushe na vitendo vya rushwa kwani rushwa ni adui wa haki”, alisema.
Alisema Mahakama haitasita kumchukulia hatua kali za kinidhamu mtumishi yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa. Aidha, alimwomba Mkuu Wilaya kupitia Kamati ya Maadili ya Mahakimu kuwaelimisha wananchi kutumia kamati hizi kuwasilisha malalamiko ya mienendo isiyofaa kwa baadhi ya Mahakimu na watumishi wanaokiuka maadili wanapotekeleza majukumu yao ya msingi ya utoaji haki.
Jaji Mfawidhi alisema Kujengwa kwa jengo la Mahakama ya Mwanzo Msanzi na lile la Mtowisa ni faida kwa wananchi wa Kata hizo na maeneo ya jirani. Aliwashauri wananchi kutumia huduma ya Mahakama hizo kutatua migogoro inapotokea. Huduma za Mahakama ni muhimu kama ilivyo huduma nyingine za Umma.
“Napenda kusisitiza kuwa, majengo haya yamesaidia kusogeza huduma karibu na wananchi, na Mahakama siku zote huwa ni mali ya wananchi, hivyo naomba haki itendeke kwa wote wakati wa kusikiliza mashauri katika majengo haya bila kujali hali zao, alisema.
Mhe. Mrango alisema majengo hayo yawe msaada kwa wananchi kusikilizwa mashauri yao na kusitokee changamoto tena ya kuchelewa kusikilizwa mashauri katika eneo husika.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe.David Mrango akikata utepe kuzindua jengo jipya la Mahakama ya mwanzo Msanzi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe.David Mrango akifungua pazia kuashiria uzinduzi wa jengo jipya la Mahakama ya mwanzo Msanzi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga Mhe. David Mrango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga na Viongozi wa Serikali mara baada ya uzinduzi wa jingo la Mahakama ya Mwanzo Mtowisa.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Mtowisa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni