Jumatano, 16 Septemba 2020

MAHAKAMA KANDA YA ARUSHA YAMPONGEZA MWANAFUNZI ALIYEONGOZA HGL KITAIFA 2020

 Na Catherine Francis- Mahakama kuu Arusha

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna amempongeza kijana Joseph Masangula, mwanafunzi bora kutoka shule ya Sekondari Kisimiri mkoani Arusha aliyeongoza katika masomo ya Lugha na Sanaa kufuatia mitihani ya kidato cha sita ya mwaka huu.

Mwanafunzi huyo amepongezwa na Jaji huyo akiwakilisha uongozi wa Mahakama kuu Arusha kwakuwa kijana huyo alikuwa Mwenyekiti na Mwanachama wa “Judiciary Club” katika shule aliyohitimu.

Akitoa pongezi zake hivi karibuni, Mhe. Jaji Mzuna alisema ni jambo jema kwa kila mwanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao kwakuwa inaleta chachu na hamasa kwa wengine wanaobaki shuleni kuendelea kufanya vizuri.

“Uongozi wa Mahakama unapenda kumpongeza Joseph na shule kwa ujumla wake kwa kuwa ya kwanza kitaifa katika mitihani ya kidato cha sita 2020, hivyo pongezi zangu nazitoa pia kwa walimu ambao wamefanya jukumu la kipekee na ziada katika kuwalea  na kuwaongoza wanafunzi wao kuweza kufikia malengo yao kimasomo na hatimaye kuibuka kidedea kitaifa,” alisema.

Naye, Mkuu wa shule ya sekondari Kisimiri, Mwl. Valentino Tarimo aliushukuru Uongozi wa Mahakama Arusha kwa ushirikiano na kuweza kutambua umuhimu na mchango wao katika kuwalea wanafunzi hao.

Alisema kuwa ufaulu wa mwaka huu ni hali ya juu kwani kati ya wanafunzi 52 waliofanya mitihani ya kidato cha sita 2020 walifaulu wote kwa kupata daraja la kwanza na kuahidi kuwa shule itaendelea kuwahimiza wanafunzi hao kuendelea kufanya vizuri zaidi na kwa wale wanachama wa “Judiciary Club” kuiga mfano mzuri wa mwenzao Joseph Masangula.

“Napenda kushukuru kwa ushirikiano unaoendelea baina ya Mahakama na shule  yetu ambapo kwa pamoja tunaweza kufikia malengo kwa urahisi na kutekeleza  jukumu la kutengeneza watumishi wa umma walio bora na wenye maadili,” alisema.

Shule ya Sekondari Kisimiri ni mojawapo  ya shule ambazo zipo chini ya uangalizi wa Mahakama Kimaadili,hivyo Mahakama Kuu Arusha ina jukumu la kuilea na kuiongoza shule hiyo kimaadili ili kuweza kupata watumishi wa Mahakama wenye maadili mazuri na hata kwa Taasisi nyingine.

                    Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Moses Msuna akimkabidhi   Mwanafunzi Joseph Masangula cheti cha pongezi.
 
     Mwl. Valentino Tarimo kutoka Shule ya Kasimiri Sekondari akipokea zawadi ya                                           shule toka kwa Mhe Jaji Mzuna.
     Mhe. Jaji  Mzuna akizungumza jambo.
Picha ya pamoja na Mwanafunzi bora Joseph Masangula (wa tatu kushoto)  na viongozi wa Mahakama Kuu Arusha.
 Picha ya pamoja ya Viongozi wa Mahakama Kuu Arusha na Waalimu na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kisimiri.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni