Jumatano, 23 Septemba 2020

ZINGATIENI TARATIBU STAHIKI UTOAJI HAKI KESI ZA UCHAGUZI: JAJI KIHWELO

 Na Ibrahim Mdachi, IJA-Lushoto

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Jaji. Dkt. Paul Kihwelo amewakumbusha Mahakimu Wakazi Wafawidhi nchini kuzingatia taratibu madhubuti za kimahakama zinazofuata misingi ya kidemokrasia kama nguzo muhimu ya kutatua migogoro ya uchaguzi.

Akifungua awamu ya pili ya mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Wahe. Mahakimu hao yanayofanyika katika Chuo hicho, Mhe. Jaji Kihwelo aliwataka kutokupendelea au kukandamiza upande wowote unaoshindana katika siasa na katika uchaguzi mkuu.

 “Lengo kubwa la Mahakama kutayarisha Mafunzo haya ni kuwaweka Maafisa wa Mahakama ambao wanaweza kupangiwa majukumu ya kusikiliza mashauri ya uchaguzi, kwenye hali ya utayari wa kuyasikiliza mashauri hayo kwa weledi, kwa wakati na kwa uwazi na haki.” alisema.

Mkuu huyo wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliwataka pia Mahakimu hao kuzingatia Ibara ya 113A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayotoa marufuku kwa maafisa wa mahakama ya kutojiunga na Chama chochote cha siasa, ila tu kuwa na haki ya kupiga kura.

Aidha, aliwaomba kuipitia kwa undani sehemu ya pili ya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura ya 292 ya Sheria za Tanzania ambayo imeainisha makosa kadhaa ya kijinai ambayo wanatarajia kuyapokea, kuyasikiliza na kuyatolea maamuzi bila kusubiri siku ya Uchaguzi.

 Alitaja kuwa miongoni mwa makosa hayo ni pamoja na kujiandikisha katika maeneo zaidi ya moja, kugushi nyaraka mbali mbali, hongo, rushwa, matumizi ya vitambulisho vya watu wengine na mengineyo.

Aliwasisitiza pia kujisomea zaidi sheria, kanuni, kesi za mahakama za juu, Kanuni za Maadili za Uchaguzi n.k vinavyohusiana na uchaguzi ili waweze kuwa bora zaidi na kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima ambayo yanaweza kutokana na utoaji wa maamuzi ambao hauzingatii maadili ya kazi ya uhakimu.

Mpaka sasa mafunzo haya yamewahusisha Waheshimiwa Majaji wa Rufani na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao walishiriki kwa makundi mawili, Wasajili kutoka Mahakama ya Tanzania pamoja na Warajisi kutoka Mahakama Kuu ya Zanzibar vile vile Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi nchini.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji.Dkt. Paul Kihwelo akifungua rasmi mafunzo ya siku tatu kwa Wahe. Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya juu ya namna bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi.

  Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Robert Makaramba akiwasilisha mada katika mafunzo hayo.


Baadhi ya Waheshimiwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya katika picha ya pamoja na meza kuu mara baada ya Ufunguzi wa Mafunzo hayo.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni