Jumanne, 20 Oktoba 2020

GRAMU 351.99 ZA MADAWA YA KULEVYA ZATEKETEZWA TANGA

Na Amina Ahmad, Mahakama Kuu-Tanga

Mahakama Kuu Kanda ya Tanga kwa kushirikiana na wadau wake imeteketeza kiasi cha gramu 351.99 za madawa ya kulevya aina ya ‘Heroin Hydrochloride.’

Hatua hiyo imetokana na maamuzi ya shauri la uhujumu uchumi namba 4 la mwaka 2019 kati ya Jamhuri na Mshtakiwa Mussa Sembe ambapo baada ya hukumu kutolewa Mwezi julai mwaka huu, Mahakama ilithibitisha kuwa mshitakiwa hakuwa na hatia katika kesi hiyo iliyosikilizwa na Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania Kitengo cha makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, Mhe. Lilian Mashaka.

Akizungumza na Waandishi wa habari walioshiriki kushuhudia zoezi hilo lililofanyika hivi karibuni katika eneo la kiwanda cha saruji cha Tanga Cement Jijini Tanga, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Francis Kabwe alisema mara baada ya hukumu kutolewa Mahakama  iliamuru madawa hayo yateketezwe.

“Ndugu Waandishi kilichofanyika leo ni utekelezaji wa amri ya Mahakama ya kuteketekeza madawa ya kulevya aina ya Heroini, baada ya mshitakiwa kutokuwa na hatia, Mahakama aliamua kutoa amri hii,” alisema Mhe. Kabwe.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali Mwandamizi ambaye pia ni Mkuu wa  Mashtaka  Mkoa wa Tanga, Pius Hila amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kutosha kupambana na watu wote wanaojihusisha na madawa ya kulevya ili nguvu kazi ya taifa isiathirike.

Naye Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Tanga,  Inspekta Jeremia Ouko ametoa rai kwa wafanyabiashara na watuamiaji wa dawa za kulevya kuacha tabia hiyo kwani hawataachwa salama.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Francis Kabwe (katikati) na wenzake Mkuu wa  Mashtaka  Mkoa wa Tanga (kushoto), Mhe. Pius Hila, Wakili wa Kujitegemea wakiwa katika zoezi maalumu la uteketezaji wa madawa ya kulevya aina ya ‘Heroine’. Zoezi hilo lilifanyika hivi karibuni katika eneo la kiwanda cha saruji cha Tanga Cement Jijini Tanga.

Wadau wa Mahakama wakiwa kwenye msafara kuelekea eneo lililoandaliwa kwa ajili ya uteketezaji wa Madawa ya kulevya lililopo Kiwanda cha Saruji- Tanga Cement 'Tanga Cement.'

        Mtaalam kutoka Kiwanda cha Saruji Tanga akiteketeza Madawa ya kulevya.



 

 




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni