Na Tawan Salum-Mahakama, Lushoto
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt.
Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Mahakimu kujiepusha na vitendo vya rushwa na
badala yake wawe mstari wa mbele katika kuielimisha jamii madhara yanayotokana
na vitendo hivyo.
Jaji Kiongozi ameyasema hayo wakati akifungua rasmi
Mafunzo kwa Mahakimu wapya walioapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma Novemba 27 mwaka huu, yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania
kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa lengo la
kuwajengea uwezo Mahakimu hao.
“Rushwa ni adui
wa haki, ikataeni na kuiogopa kama ukoma na mkawe mabalozi wazuri wa kutoa
elimu juu ya madhara ya rushwa kwenye jamii zetu kwa kuwa nina imani ndiyo
mmeapishwa hivi karibuni mnajua kuwa rushwa ni mbaya”, alisema Jaji Kiongozi.
Alisema Mahakama ya Tanzania iko katika mapambano
dhidi ya vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili kwa watumishi wake kama ambavyo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambavyo
amekuwa akiifananisha na ugonjwa wa Saratani na kupambana nayo kwa nguvu zote.
Aliwataka Mahakimu hao kuichukia rushwa kabla
haijajipenyeza na kupata makao ili kulinda heshima yao, ya Mahakama na hata
Taifa kwa ujumla. “Ninaamini hata ninyi hampendi kukosa haki zenu au ndugu na
jamaa zenu kutokana na vitendo vya rushwa”, alisema Jaji Kiongozi.
Alisema hategemei Mahakimu kufanya Makosa hasa katika
maeneo ambayo Sheria iko wazi kwa kuwa Hakimu anatakiwa kujitayarisha kwa kuwa
na uelewa wa Sheria na taratibu zote za shauri lililo mbele yake kabla ya kuingia
mahakamani, hivyo Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo ili waweze kuwa na
utayari huo.
Akizungumzia mafunzo hayo, Dkt. Feleshi aliwaambia
Mahakimu hao kuwa kupatiwa mafunzo kama hayo ni fursa muhimu na historia kwa kuwa
ni mwanzo mwema kwa Maadhimisho ya miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania yatakayozinduliwa
hivi karibuni na Jaji Mkuu. Aliongeza kuwa uzinduzi huo utatanguliwa na Maadhimisho
ya Miaka ishirini (20) ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Katika hatua nyingine Jaji Kiongozi ameipongeza Tume
ya Utumishi wa Mahakama na Jaji Mkuu kwa kuweka mfumo madhubuti wa kuhakikishia
Tume inaajiri Mahakimu mahiri na kwa ushindani wa haki. Alisema Mahakimu 39
waliapishwa Ijumaa ya Novemba 27, 2020.
Naye Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Kevin Mhina
alimshukuru Jaji Kiongozi kwa kutoa muda wake na kukubali kufungua mafunzo hayo
kwa Mahakimu waliapishwa hivi katibuni. Aliwataka Mahakimu hao kuzingatia maadili
katika utekelezaji wa majukumu yao na kuzingatia mambo yote mengine muhimu
waliyoaswa na Jaji Kiongozi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akifungua Mafunzo kwa Mahakimu 39 waliopishwa hivi karibuni. Mafunzo hayo yamefanyika katika chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa lengo la kuwajengea uwezo. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na wa pili kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Kevin Mhina. Kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu Mhe. Sharmilla Sarwatt na wa kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Edward Nkembo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto mara baada ya kufungua kwa Mafunzo kwa Mahakimu 39 waliopishwa hivi karibuni.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu mara baada ya kufungua rasmi mafunzo yao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni